loader
Picha

Fuga mende utajirike

Mende ni mdudu anayechukiwa na watu wengi katika jamii kwa kuwa anahusishwa na uchafu sambamba na kusambaa kwa maradhi mbalimbali licha ya wadudu hawa kuwa na manufaa makubwa kwa binadamu ambayo hayajajulikana kwa wengi.

Lucius Kawogo ni mkazi wa wilayani Njombe akijishughulisha na ujasiriamali wa namna tofauti ukiwemo wa kufuga samaki, kuku, sungura, nyuki na pia, anafuga mende kwa ajili ya chakula cha samaki na kuku anaowafuga sambamba na mende kwa ajili ya biashara (kuuza).

Kawogo anayefanyia ufugaji wake wa mende katika Kijiji cha Igawisega, Kata ya Wino wilayani Madaba mkoani Njombe, anasema japo amefanya shughuli hiyo kwa takribani miezi sita iliyopita, anaona ufugaji wa mende ni kazi ndogo na rahisi, lakini yenye faida.

“Nimeanza kuongeza uzalishaji wa kuku na samaki kwa kufuga mende kwa ajili ya chakula cha mifugo hao kwa kuzingatia lishe na matunzo ya wadudu hao ambao bado kwa watu wengi hawafamu kuwa ni chakula kizuri… Mende wana kiasi kikubwa sana cha protini.” anasema.

“Kwa kweli, watu hawajajua tu, lakini ufugaji wa mende ni biashara inayolipa sana na ndiyo maana ninatamani wengi waifanye kazi hii ili hata ninapokuwa na oda nyingi kiasi cha mimi kupungukiwa, wateja wangu wasikose mzigo, bali nichukue kwa wafugaji wengine na kutimiza mahitaji ya wateja wangu huku pia, nikiwa nimesaidia biashara kwa wafugaji wenzangu.”

Anapozungumza katika mafunzo kwa wajasiriamali 1,000 yaliyoandaliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) mjini Njombe hivi karibuni, Kawogo anasema anajuta kuchelewa kurasimisha miradi yake hali ambayo ingemwezesha kupata mtaji mkubwa na mapema zaidi.

“Kuchelewa kurasimisha miradi yangu kumenikosesha fursa nyingi maana siwezi hata kupata mkopo na kama ningekuwa nimerasimisha, ningepata soko na wateja wengi na ningetambulika na kujitangaza zaidi.” anasema.

“Nimewaomba Mkurabita wanisaidie kuniunganisha na benki ili benki inikopeshe mtaji wa kufanya ufugaji wangu mkubwa wa samaki, kuku, mende na vingine, lakini kwa masharti nafuu; yaani, nipewe muda wa kutosha kuanza marejesho tofauti na hali ilivyo kwa taasisi nyingi, unapewa leo mkopo, wiki hii hii unatakiwa uanze marejesho sasa unajiuliza kama sijaanza uzalishaji, hayo marejeso nitayatoa wapi, labda nikate pesa zilezile walizonipa, niwarejeshee…” anasema.

Mratibu wa Kitaifa wa Mkurabita, Seraphia Mgembe anasema: “Baada ya kumsikia akisema anatafuta namna ya kupata mkopo benki ukiwa na masharti nafuu, tuliwasiliana na kumuunganisha na benki ya CRDB, Tawi la Njombe nao wakasema, wako tayari kumsikiliza aende wazungumze.”

Meneja Urasimishaji Biashara wa Mkurabita, Harvey Kombe, anasema walipomtembelea Kawogo kuona namna anavyofanya shughuli zake hivi karibuni, walibaini maendeleo katika ufugaji wa samaki sambamba na ufugaji wa memde anaotumia kulishia samaki na kuonesha manufaa makubwa. Mintarafu mazungumzo na CRDB kuhusu mkopo huo, Kombe anasema: “Bado wapo kwenye mazungumzo…”

Kawogo amekiri kuwa katika mazungumzo hayo na CRDB. Anasema: “Bahati nzuri Mkurabita hao hao, wamenikutanisha pia na SIDO ambao wamekubali kunikopesha Sh 5,000,000 ili marejesho yaanze baada ya miezi 12….”

Mjasiriamali huyu anasema alianza na mtaji wa mende wa Sh 150,000 aliponunua boksi moja la mende wazazi 100 kutoka Kenya na sasa anafuga takriban mende 50,000 katika maboksi matano yenye takriban mende 10,000 kila moja na anakusudia kuongeza mengine.

Anasema asili ya wazo la ufugaji mende ni picha ya video aliyoona katika mitandao ya kijamii na kisha, akafuatilia na kusoma kwenye mitandao kwamba kuna uwezekano wa kufuga mende na funza ndipo akabaini uwezekano huo na manufaa yake. “… Nilikwishauza mende zaidi ya 600. Mende mmoja anauzwa kwa Sh 500 na yai moja la mende, linatoa watoto takriban 50…”.

Anabainisha kuwa, wateja wake wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Dodoma, Mwanza, Bukoba (Kagera), Mkuranga (Pwani), Dar es Salaam na Kigoma na kwamba, hajawahi kupata mteja kutoka Njombe.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam, Judica Losai anasema amevutiwa na bidhaa hiyo ya mende na kuweka oda ya mende 50 na maboksi mawili kwa mfugaji huyo ili kulishia bata anaowafuga.

Losai anasema: “Nitamshauri hata mwanangu Enoth Lyimo anayefuga pelege (samaki) na kuku huko Mlandizi (mkoani Pwani) ili naye aanzishe ufugaji wa mende kulishia samaki wake.”

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Menardy Mlyuka anampongeza Kawogo kwa ubunifu wa kufuga vitu (mende) ambavyo faida zake hazijafahamika vema kwa jamii.

Kawogo anasema ili mende wasisambae na kuwa kero kwa wakazi na maeneo jirani, huwajengea maboksi yasiyoruhusu hata mende mdogo kutoka, lakini akizingatia kuwaacha mianya ya kupitisha hewa ili wasife.

“Hapo ninapowafugia, pia kuna kuku wengi hivyo, ikitokea mende akatoroka, hawezi kufika mbali maana atagombaniwa na kuku. Unajua kuku wanapenda sana kula mende,”anasema.

MANUFAA Anapozungumzia manufaa aliyokwisha yapata katika ufugaji wa mende, Kawogo anasema:

“Mende ambao nimewauza, nimefanikiwa kutumia fedha kuchonga maboksi mengine, nimenunua sungura ninaowafuga na wengine nimekuwa nikiwatumia kukausha na kuwasaga kwa ajili ya kutengeneza chakula cha samaki na kuku ambao tangu waanze kula mende, wamekuwa na afya bora na uzalishaji mayai umeongezeka maradufu… wanataga sana”.

Anapoulizwa kama wateja au walaji wa kuku na samaki anaowafuga hawachukii wanaposikia wanakula chakula kinacholishwa kwa mende,

Kawogo anasema: “Wateja wanaposikia hivyo, wanafurahi kweli maana kwanza wanajua mende wanaprotini nyingi, na pia hawana chemikali kwa hiyo wanakula vyakula ambavyo havijalishwa kemikali. Watu hawataki kula kuku waliokuzwa kwa kulishwa kemikali…”

UBORA NA CHANGAMOTO

Anasema: “Tangu nianze ufugaji wa memde, sijapata changamoto ya kuuguliwa mende.”

“Kwa kweli mende ni rahisi sana kufuga na gharama za uendeshaji ni ndogo maana ninawawekea bakuri la maji kwenye banda, bakuri la unga lenye mchanganyiko wa mabaki kama mashudu na kiporo cha vyakula mbalimbali.”

Anasema: “Unajua hawa siyo mende wale wanaotoka chooni, au kwenye takataka, hawa wanatunzwa na ni wasafi wanazaliwa na kutunzwa kwenye boksi maalumu hadi wakati wa kuvunwa…”

Kawogo anaongeza: “Mende wanaliwa ingawa sisi hatujaanza kuwala moja kwa moja, lakini wana protini nyingi zinazohitajika mwilini na hizo, tunazipata kupitia kuku na samaki tunaowalisha ndiyo maana watu wanawachangamkia sana…”

Kuhusu malengo ya baadaye katika ufugaji huo, Kawogo anasema ni pamoja na ni kupanua ufugaji huo ili umsaidie kwa ufugaji wa samaki na kuku kwani mende wanafugwa kwa gharama nafuu na wana manufaa makubwa kwa samaki na kuku wanaolishwa.

FAIDA ZA MENDE KWA BINADAMU

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), linaandika katika mtandao likisema mende wana manufaa mengi kwa binadamu.

Linasema: “Wanasayansi huwafurahia sana mende na kuwatumia kwa manufaa ya binadamu. Mwaka 1999, mende walitumiwa na Profesa Robert Full katika Chuo Kikuu cha California, Berkley, kumpa wazo la kuunda roboti ya miguu sita iliyosonga upesi na kwa urahisi.”

Chapisho hilo la kimtandao linasema: “Wanaweza kusaidia katika kutengeneza dawa za kusaidia binadamu kukabiliana na bakteria zinazohangaisha sana watu kwa mfano E. Coli na MRSA ambazo zimekuwa hazisikii dawa.”

“Mwanahabari Lafcadio Hearn karne ya 19 alipitia maeneo ya Kusini mwa Marekani na kuripoti jinsi watu wenye pepopunda walivyokuwa wakipewa chai iliyotengenezwa kwa kutumia mende…

Katika hospitali Uchina, krimu inayotengenezwa kwa kutumia ungaunga wa mende waliosagwa hutumiwa kutibu vidonda vya moto na pia humezwa kutibu vidonda vya tumbo.

Linasema: “Mende wanahitajika sana hivi kwamba Wang Fuming aliamua kufungua biashara ya ufugaji mende eneo la Shandong, Mashariki mwa Uchina. Huwa anafuga mende 22 milioni kwa wakati mmoja.

Tangu 2010, bei ya mende waliokaushwa imepanda mara kumi.” Mwaka 2016 iliripotiwa kuwa, wanasayansi nchini India wanasema huenda mende wakatoa tumaini kwa binadamu, katika lishe kwani maziwa ya mende ni chanzo bora cha protini kwa kuwa chembe za protini za maziwa kwenye mende zina virutubisho "vingi ajabu”.

Wanasayansi katika Taasisi ya Sayansi ya Seli katika mji wa Bengaluru nchini India, walifanya ugunduzi huo baada ya kutafiti muundo wa chembe za protini zinazopatikana katika utumbo wa aina ya mende wajulikanao kama ‘diploptera puncata’, ambao ndio pekee wanaojifungua.

Chembe moja ya protini hiyo inakadiriwa kuwa na kiwango mara tatu cha nguvu ya mwili ikilinganishwa na kiasi sawa cha maziwa ya nyati; na zina nguvu mara nne ya maziwa ya ng’ombe.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi