loader
Picha

JPM kupokea Air Bus A220-300 ya pili leo

RAIS John Magufuli leo atawaongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kupokea ndege ya pili ya kisasa aina ya Air Bus A220-300, itakayowasili nchini leo, ikitokea kiwandani Canada.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Menejimenti ya Shirika la Ndege nchini (ATCL ) kwa vyombo vya habari jana, sherehe za mapokezi ya ndege hiyo itaanza saa sita mchana katika kiwanja cha ndege cha zamani maarufu kama Terminal 1, pembezoni mwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam. Ndege hiyo ya pili aina ya Airbus A220-300, itafanya idadi ya ndege mpya zilizonunuliwa na Serikali ya Awamu ya tano kufikia sita.

Mara baada ya kuingia madarakani, Serikali ya Rais John Magufuli iliahidi kuifufua Kampuni ya Ndege nchini (ATCL) kwa kununua ndege mpya saba. Mpaka sasa ndege tano zilizonunuliwa na Serikali zilishawasili nchini. Miongoni mwa ndege hizo, zimo Bombardier Dash 8 Q400 tatu zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Boeing 787-8 Dreamliner moja yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132 moja.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamuriho aliliambia gazeti hili jana kuwa ndege hiyo, itawasili jioni leo na kulakiwa na viongozi mbalimbali, watakaoongozwa na Rais Magufuli. Juzi Rais Magufuli akiwaapisha viongozi mbalimbali, aliowateua hivi karibuni Ikulu jijini Dar es Salaam, alisema kuwa alikesha juzi akifuatilia ndege hiyo.

Alitoa kauli hiyo baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumwomba Rais awaruhusu mawaziri waende liikizo, kwa kuwa nyuso zao zinaonekana kujaa uchovu kutokana na pilikapilika za kazi. Akijibu ombi hilo la Spika, Rais Magufuli alisema hata yeye hajaenda likizo na juzi alikesha akiwasiliana na watu walioifuata ndege hiyo ya pili aina ya Airbus.

Alisema viongozi hao, walimweleza kuwa ndege ilikuwa inaendelea vizuri na majaribio na wakati huo ilikuwa angani kwa muda wa saa nne. Akizungumzia safari za ndege ya Air Bus A220-300, iliyowasili nchini wiki mbili zilizopita, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ATCL, Josephaat Kagirwa, alisema mbali na safari ya kwenda Mwanza, ndege hiyo kesho itaanza kufanya safari kwenda Mbeya.

Alisema mbali na safari hiyo, wakati wowote wa Februari ndege hiyo Air Bus A220-300 inatarajiwa kuanza safari kwenda katika miji ya Harare, Zimbabwe na Lusaka nchini Zambia. Aidha, Kagirwa alisema kuanza safari kwa ndege hizo, kunatarajiwa kutoa fursa ya kupatikana kwa wateja wa kutosha, watakaowezesha safari za ndege kubwa ya Dreamliner, inayotarajiwa kuanza safari zake kwenda Bombay (India), Ghounziouh (China) na Bangkok Thailand ndani ya miezi miwili ijayo.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi