loader
Picha

Sakata la polisi wa ‘dhahabu’ latua kwa DCI

SAKATA la askari polisi wanane wanaodaiwa kujihusisha na kashfa ya utoroshaji dhahabu jijini Mwanza, limetua rasmi kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Boaz.

Askari hao ambao Januari 4, mwaka huu, waliwakamata watu waliotaka kutorosha kilo 323.6 za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30 na fedha taslimu Sh milioni 305, walitaka wapewe Sh bilioni 1 kutoka kwa watuhumiwa hao. Baada ya mpango wao huo kukwama kutokana na mamlaka za nchi kuingilia kati na watuhumiwa kutiwa mbaroni na askari wenzao, kinachoendelea kwa sasa ni uchunguzi wa suala hilo ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani.

DCI Boaz, katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, alisema ofisi yake itakamilisha upelelezi wa jambo hilo hivi karibuni. Alisema kuwa upelelezi unaoendelea, utawasaidia kujua ni makosa ya aina gani watuhumiwa hao wanane, wanakabiliwa nayo ili mashitaka dhidi yao yaweze kufunguliwa. Alisema kwa kuwa watuhumiwa hao ni askari, watapelekwa kwanza kwenye Mahakama ya Kijeshi kwa ajili ya mashitaka ya kinidhamu na kama kutakuwa na jinai yoyote dhidi yao, ndipo watakapopelekwa kwenye Mahakama za Kiraia.

Wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, akiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, katibu tawala mmoja na makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Rais John Magufuli aliwaeleza Watanzania mpango mzima ulivyokuwa. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, askari hao baada ya kuwakamata watuhumiwa, waliwafikisha Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, lakini hawakushushwa kwenye gari, badala yake walichokifanya ni kuwataka watuhumiwa wawepe Sh bilioni 1.

Baada ya majadiliano yao, watuhumiwa katika mkupuo wa kwanza, waliwapatia askari hao Sh milioni 300, mkupuo wa pili wakawapa Sh milioni 400 na kuahidi kumaliza mkupuo wa tatu wa Sh milioni 300 watakapofika wilayani Sengerema. Wakiwa njiani kuelekea Sengerema, ndipo walipokutana na kizuizi cha polisi njiani na watuhumiwa wote wakiwemo askari hao wanane wakatiwa mbaroni. Kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na jeshi hilo, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwa kazi nzuri iliyofanyika.

Ili kufanikisha kazi hiyo ya kufuatilia utoroshaji wa dhahabu na madini mengine nchini, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda Ahmed Msangi, alisema kuwa msingi wao mkubwa wa kufanikisha kazi hiyo ni wananchi. Alisema Jeshi la Polisi litafanya kazi kwa karibu na wananchi, ikiwemo kuwapatia elimu ili wananchi hao waweze kushirikiana na jeshi hilo, kwa kutoa taarifa kuhusu utoroshaji huo.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore iliyopo Kijiji cha ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi