loader
Picha

Mabasi 2,800 nchini yaanza kufuatiliwa mwenendo wake

ZAIDI ya mabasi 2,840 yanayokwenda mikoa mbalimbali nchini yamefungwa mfumo maalumu wa ufuatiliaji wa mwenendo wake (VTS) na umeanza kutumika rasmi jana.

Mfumo huo ulioanza Januari mwaka juzi kwa majaribio kwa baadhi ya njia, ni maalumu kubaini madereva wanaoendesha zaidi ya kasi ya mwendo wa 80 kwa saa ili kuepusha ajali zinazotokana na mwendokasi. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na nchi kavu (Sumatra), Gilliard Ngewe alisema wakati majaribio yalihusisha mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, hivi sasa mabasi 2,840 yote nchini yameunganishwa. Ngewe alisema utafiti mbalimbali uliofanyika, umebainisha upo umuhimu kutafuta njia za kudhibiti ajali hizo.

Alisema miongoni mwa utafiti ni pamoja na uliofanywa na Sumatra kwa kupitia taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unaoonesha asilimia 76.4 za ajali hizo zilitokana na makosa ya kibinadamu. Kwa mujibu wa meneja wa mradi huo, Godfrey Nsato mfumo huo wa VTS ni muhimu kudhibiti madereva nchini na kupunguza ajali za barabani.

Alisema mfumo huo utatoa hadhari iwapo dereva atatanua njia kwa lengo la kuwahi na akiwa kwenye mwendo wa kasi itampigia ishara ya kumjulisha kuwa amezidisha mwendo, itaonesha pia iwapo dereva alikuwa akienda hovyo barabarani, kutoa taarifa ya ajali na itamtambua dereva wa basi. Alitaja faida nyingine za mfumo huo kuwa umesaidia kupunguza matukio ya ajali, kupunguza athari za ajali na kupunguza matumizi ya mafuta kwenye mabasi. Hata hivyo Nsato alisema baadhi ya madereva wamekuwa wakihujumu mfumo huo na kusababisha athari za ufanisi.

Alisema pia kuna uhitaji wa maboresho ya elimu, udhibiti na usimamizi wa sheria kwa madereva na watumiaji wengine wa barabarani. Hii ni kutokana na utafiti huo kubaini kuwa baadhi ya madereva hawapatiwi mafunzo ya kutosha. Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Isack Kamwele ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alisema wadau wote nchini waungane kuhakikisha wanamaliza tatizo la ajali barabarani.

Kamwele ameagiza kila mmiliki wa basi kuwa mwaminifu na kufunga mabasi yake mfumo huo na iwapo itabainika kuwa kuna waliokiuka, Sumatra iwachukulie hatua kali kwa mujibu wa sheria. Kamwele ameshauri pia magari yote ya serikali na daladala kufungwa VTS na kwamba serikali inaunga mkono juhudi za kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua zaidi kama sio kumalizika.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi