loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utalii wa ndani ni haki, mali yetu; tuuchangamkie

KATIKA kukuza sekta ya utalii nchini, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeanzisha chaneli ya utalii inayoitwa ‘Tanzania Safari Channel’, iliyoanzishwa kwa ushirikiano na wadau wengine wa utalii.

Wadau hao ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) na Bodi ya Utalii Tanzania. TBC ilianza kurusha vipindi vya majaribio kuanzia Desemba 15, 2018 ilipozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TBC, Edna Rajab, mwaka 2016 Tanapa waliishirikisha TBC katika wazo la kuanzisha Chaneli hiyo ili kutangaza utalii nchini na nje ya nchi.

Tanapa walisema wao wasingeliweza kuanzisha Chaneli ya Televisheni peke yao kwa sababu uendeshaji wa chombo cha habari haikuwa moja ya majukumu ya shirika hilo. Baadaye wazo lao likapata msukumo mkubwa kutoka kwa Rais John Magufuli, alipozuru ofisi za TBC Mei 16, 2017 na kuelekeza uongozi wa TBC uangalie uwezekano wa kuanzisha Chaneli ya Utalii kwa kushirikiana na Tanapa. Kisha wakuu wa taasisi ambazo ni wadau wa utalii (Tanapa, NCAA, TTB na TBC) wakasaini mkataba wa kuanzisha Chaneli ya Utalii, jijini Dodoma Juni 21, 2017.

Hata hivyo, kwa kuwa milango ilikuwa wazi kwa wadau wengine kujiunga, wadau wengine kama Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Idara ya Uvuvi, Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Tawa), Wakala wa Misitu (TFS), Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) pia wakajiunga. Ili Tanzania Safari Channel ifanye kazi kwa ufanisi, wadau wa utalii wamekubaliana kutoa bajeti ya Sh bilioni tano ili kufanikisha uendeshaji wa chaneli hiyo mahususi kwa kutangaza utalii na vivutio vyake hapa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Chaneli hiyo aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustin Kamuzora, alisema jijini Dar es Salaam mwishoni mwa 2018. Katika mazungumzo hayo, Profesa Kamuzora anabainisha kuwa fedha hizo zitatumika ndani ya miezi sita kununua vifaa, kuweka wataalamu na kununua vipindi. Anaweka wazi kwamba, kwa sasa chaneli hiyo haijafikia maudhui ya kutosha kama wanavyokusudia, lakini wadau wamejipanga kuhakikisha ndani ya miezi sita suala hilo linapatiwa ufumbuzi tarajiwa.

“Wadau wakubwa wote wameonesha utayari na wamekubali kwamba kwenye miezi sita iliyobakia ya bajeti hii ya sasa watatenga fedha ya kutosha na kwenye bajeti inayofuata ya 2019/2020 kwa ajili hiyo,” anaeleza. Hatua ya kuanzisha chaneli ya utalii imekuja wakati sahihi kuhamasisha utalii wa ndani, kwani Watanzania wengi hawatembelei vivutio vya utalii, kwa kudhani wageni kutoka nje ya nchi (Wazungu), ndio wanaopaswa kutembelea hifadhi za wanyama na kuangalia kumbukumbu na vivutio mbalimbali.

Septemba 2008 aliyekuwa Daktari Mkuu wa Wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Tanapa, Dk Titus Kamani alisema Watanzania wengi hawana uelewa wa vitu na faida inayopatikana endapo watatembelea hifadhi ya taifa, hivyo ni wakati sahihi kuchangamkia fursa za utalii zilizopo. Dk Kamani aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi katika Awamu ya Nne, na sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema mfumo wa Watanzania kutotembelea hifadhi za wanyama ulijijenga tangu awali, serikali ilipotenga maeneo maalumu ya hifadhi kwani hawakuwashirikishwa vya kutosha.

Anasema upo umuhimu mkubwa kwa wananchi kuwa watalii katika nchi yao ili wajue tabia mbalimbali za wanyamapori ambao wengine tabia zao hufanana na zile za kibinadamu. “Unajua watu hawajui tabia za wanyama kwa sababu hawatembelei hifadhi, wanyama kama sokwe, huweka matanga, ikitokea katika familia kuna mmoja amekufa… Sasa kitu kama hicho Watanzania wengi hawajui,” anasema.

Dk Kamani anasema, changamoto iliyopo kwa Watanzania ni kwamba, lazima wawe wadau muhimu wa utalii, kwani wanapotembelea sehemu hizo hujifunza tabia mbalimbali za wanyama na kujua aina zao tofauti. Kwa mantiki hii, naamini ndiyo maana pia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania limekuja na wazo la kuanzisha ‘Tanzania Safari Channel’ ili kuonesha umuhimu wa utalii wa ndani kwa Watanzania wasioelewa umuhimu wa kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio vya utalii. Kwa miaka mingi Watanzania wengi wamekuwa hawana utaratibu wa kutembelea vivutio katika maeneo mbalimbali kama vile hifadhi, sehemu za kihistoria, makumbusho, na sehemu nyingine zinazovutia.

Mara nyingi wengi wanaposikia masuala ya utalii, huwa wanajitoa kabisa na kuona kuwa hawastahili kuwa kwenye kundi la watalii. Wengi wanaamini kimakosa kuwa, utalii upo kwa ajili ya watu kutoka nje ya nchi tu, hususan Wazungu. Utamaduni walionao katika mambo ya utalii hausaidii hata kidogo kukuza utalii wa ndani.

Ndiyo maana ninasema, jamii inapaswa kubadilika kabisa mintarafu suala hili; iachane na mambo yasiyo na tija katika maisha na taifa. Jamii iingie katika utalii, watu wawe watalii wa ndani ya nchi yao, ili waburudike, wajifunze na wachangie pato la taifa na kubwa zaidi, kwa kushiriki utalii wa ndani, Watanzania watavutia zaidi watalii kutoka nje ya nchi. Tuache kusubiri Wazungu ndio tuwaone watalii, wakati sisi wenyewe ni watalii na hatua ya kwanza ni kuanza kufanya hivyo kwa vitendo kabisa, tujenge utamaduni huu mzuri. Kwa kufanya hivi tutakuwa tunajivunia vya kwetu; tutajivunia kwa vitendo na uhalisi urithi wetu, kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na vitu vingi ambavyo wengi wanataka kuviona nje ya nchi.

Tunaposema utalii wa ndani, tunamaanisha kuwa wageni au watalii wanaotakiwa kutembelea vivutio mbalimbali tulivyo navyo ni Watanzania wenyewe, hasa wazawa. Watanzania, hatuwezi kusingizia kwamba hatuna sehemu ya kwenda kutalii au sehemu za kwenda kutembelea vivutio. Nchi yetu imejaa tele, nchi yetu imebarikiwa, nchi yetu ina vivutio vyote, vya kihistoria na vya kiasili. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, tunayo maeneo yasiyopungua 16 ya hifadhi za taifa zikiwemo hifadhi za Ruaha, Katavi, Rubondo, Ziwa Manyara na Mikumi. Kadhalika, yapo mapori ya akiba yapatayo 28 yakiwemo mapori ya Selous, Rungwe, Swagaswaga, Uwanda, Biharamulo, Lukwati na Ibanda. Tanzania kuna zaidi ya kilomita 804 za fukwe za bahari zenye mandhari nzuri na za kuvutia.

Maeneo haya hayajaathiriwa na athari mbaya za uharibifu wa mazingira, pia kuna Visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia ambavyo ni maarufu kwa utalii, hasa utalii wa ufukweni. Kama hiyo haitoshi, yapo maeneo mengi ya kihistoria, ukianzia makumbusho hadi kwenye miji mikogwe ya Zanzibar na Kilwa Kisiwani. Maeneo haya ni kama Oldupai Gorge, Bagamoyo, Kilwa, Zanzibar n.k. Ukizungumzia milima, Tanzania tumebarikiwa kuwa na milima yenye mandhari za kuvutia kama Usambara, Meru, Udzungwa, Uluguru na Rungwe.

Mlima mrefu kuliko yote barani Afrika wa Kilimanjaro unaofahamika sana duniani, upo Tanzania. Bila kusahau, Tanzania imezungukwa na maji kila upande. Kaskazini kuna ziwa kubwa na la pili kwa ukubwa duniani la Victoria ambalo limeunganishwa na mto mrefu kuliko yote barani Afrika, Mto Nile. Kusini kuna Ziwa Nyasa, wakati upande wa Magharibi kuna Ziwa Tanganyika lenye kina kirefu zaidi duniani lenye historia na mandhari nzuri kwa utalii. Huu ndiyo urithi wetu Watanzania tunaotakiwa kuuenzi, kuutunza na kuutumia.

Ni wazi kila Mtanzania anaweza, kwa nafasi yake, angalau mara moja kwa miaka miwili kufanya jambo hili muhimu kwenye maisha na nchi yetu. Tutembelee hifadhi na mbuga za wanyama, tutembelee fukwe za bahari, tutembelee sehemu za kihistoria, tuitembelee Tanzania yetu wenyewe. Mali ni zetu wenyewe, wanyama ni wetu wenyewe, misitu ni yetu wenyewe, nchi ni yetu wenyewe, lakini kwa nini watu kutoka nje ndio wafurahie vitu tulivyo navyo kuliko sisi wenyewe? Kwa nini tuwategemee watalii wa nje kukuza pato la ndani? Tuukatae kwa vitendo usemi kuwa: “Penye miti hakuna wajenzi”.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi