loader
Picha

China, Ujerumani za kwanza kutambua Mapinduzi ya Z’bar

NCHI mbalimbali ziliunga mkono Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12 mwaka 1964 na hivyo kukamilisha uhuru wa Wazanzibari.

Baada ya kufanyika kwa mapinduzi hayo, dola kubwa duniani ziliyaunga mkono Mapinduzi hayo na kuahidi kusaidia maendeleo ya wananchi wazalendo wa Zanzibar katika miradi mbalimbali. Ushawishi wa mapema ulijitokeza katika kila kundi ambapo kwa wakati ule Zanzibar ilikuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Urusi, Ujerumani ya Mashariki pamoja na Cuba.

Ali Sultani aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Abeid Karume, anasema Mapinduzi ya Zanzibar yalitambuliwa kwa mara ya kwanza haraka na nchi mbili ambazo zilichukua jukumu la kusaidia maendeleo ya Zanzibar. Nchi hizo ni China, iliyokuwa Ujerumani Mashariki pamoja na Urusi ambapo katika kipindi cha harakati za ukombozi za Wazanzibari kudai uhuru, tayari vijana wa Chama cha Afro Shirazi walikuwa wakipelekwa katika nchi hizo kwa ajili ya mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kijeshi.

“China na Ujerumani Mashariki, Urusi na Cuba ndiyo nchi za kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar... Nchi hizo pia zilijitolea kwa kiasi kikubwa kutupatia misaada na wataalamu wakiwemo wa kijeshi katika vikosi vyetu vya ulinzi, usalama wa taifa na kikosi cha wanamaji cha KMKM,” anasema Sultani. Sultani anasema hadi kufikia Aprili 26 mwaka 1964 ambapo Zanzibar iliungana na Tanganyika na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari jumla ya nchi 18 zilishayatambua Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha anasema jumla ya nchi tisa zilifungua ofisi za ubalozi kamili Zanzibar yakiwemo mataifa makubwa ya Marekani, Urusi, Ujerumani Mashariki pamoja na China na Uingereza na Ghana, ambapo mara baada ya kuzaliwa kwa Muungano, ofisi hizo zilifungwa na nyingine kubaki balozi ndogo. Akifafanua zaidi, Sultani anasema katika bara la Afrika nchi ya kwanza kuyaunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa Ghana tarehe 28, Januari, 1964 na baadaye kufungua ubalozi kamili.

Anazitaja sababu iliyopelekea Ghana kuyatambua mapema Mapinduzi ya Zanzibar ni uhusiano wa asili wa viongozi wakuu wa nchi hiyo na Tanzania katika kupigania uhuru akiwemo Mwalimu Nyerere, Karume pamoja na Kwame Nkrumah. Kwa mfano, anasema Ghana ilikuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kupata uhuru wake kutoka kwa Muingereza mwaka 1957 ambapo Rais Kwame Nkrumah aliwaalika baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kuwapa mbinu na ujanja wa kudai uhuru.

“Nakumbuka kabisa mzee Karume walialikwa kwenda Ghana na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya Zanzibar kwa ajili ya kupewa mbinu za kujenga mikakati ya kudai uhuru kutoka kwa Muingereza,” anasema. Aidha mikutano ya wapigania uhuru wa Afrika Mashariki na Kati (Pan- African Freedom Movement of East and Central Africa-PAFMECA) kwa kiasi kikubwa ilisaidia kuwakutanisha viongozi hao ambao kwa wakati huo walikuwa katika harakati za kupigania uhuru, mikutano ambayo ilikuwa kwa ajili ya kudai uhuru.

Sultani anasema viongozi wa Afrika hasa Mwalimu Nyerere, Kwame Nkrumah wa Ghana na Abeid Amaan Karume wa Zanzibar walikuwa na mawazo ya pamoja ambayo lengo lake ni kuhakikisha kwamba bara la Afrika linakuwa huru na kwa wakati ule Nkrumah alikuwa na mwelekeo wa mapema katika kupiga vita harakati za ukoloni wa Kiingereza.

Pia viongozi hao walikuwa na maono ya kuunganisha nchi za Afrika kuwa nchi moja. Rais Nkrumah katika kuwaunga mkono wana wa Afro Shirazi alimleta wakili Swanzi kwa ajili ya kuwatetea wana ASP ambao walishtakiwa kwa mauaji katika fujo zilizotokea Juni mwaka 1963. Kuanzia hapo marais na viongozi wakuu wa nchi mbalimbali duniani walikuwa na hamu kubwa ya kuitembelea Zanzibar na kujionea harakati zake za kupigania uhuru. Miongoni mwa viongozi mashuhuri waliotembelea Zanzibar alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China wakati wa uongozi wa Mwenyekiti Mao Tsetung, Chou En Lai ambaye alizuru Zanzibar tarehe 5/6/1965.

Alipofika uwanja wa ndege wa Zanzibar na kulakiwa na Rais wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume na Makamu wa Pili wa Rais Rashid Mfaume Kawawa. Wengine ni Rais wa Liberia, Tubman, Mfalme Haille Selassia wa Ethiopia, Rais wa Misri, Gamal Abdell Naseer na Rais wa Yugoslavia, Broaz Tito. Ujerumani Mashariki ilisaidia ujenzi wa kwanza wa nyumba za maendeleo za kupigiwa mfano zilizopo Kikwajuni mjini hapa, ambazo mafundi wazalendo walipata ujuzi uliosaidia kujengwa kwa nyumba nyingine za maendeleo ziliopo Michenzani, Kilimani na sehemu nyingine za vijijini na Pemba.

Kadhalika, kumbukumbu zilizopo zinaonesha kwamba Ujerumani walileta meli kubwa ambayo ilibeba kila kitu kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Kilimani ikiwemo saruji na vifaa vingine. Kadhalika walikupatia misaada ya vifaa mbalimbali kikosi cha majini cha KMKM. China kwa upande wake ilisaidia maendeleo ya Zanzibar kwa kujikita zaidi katika kusaidia ujenzi wa viwanda mbalimbali vya uzalishaji wa bidhaa, kikiwemo kiwanda cha ngozi na viatu kilichopo Maruhubi. China pia ilisaidia ujenzi wa kiwanda cha Sigara, kiwanda cha sukari kilichopo Mahonda kwa ajili ya kupunguza tatizo la kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi. China pia inatajwa kusaidia ujenzi wa kiwanja cha mpira cha Amaan ambacho katika miaka ya 1972 kilikuwa ndicho kiwanja kikubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati. Kiwanja hicho kilifunguliwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1971.

Ali Sultani aliyepata kuongoza Wizara ya Elimu na baadaye Afya anasema China ilitia saini makubaliano na Zanzibar kubadilisha wataalamu na madaktari katika fani mbalimbali kuja Zanzibar kufanya kazi. Anasema madaktari wa kwanza wa Kichina walifika Zanzibar katika mwaka 1965 na kuanza kusaidia kutoa tiba kwa wananchi wa Zanzibar ambapo kwa wakati huo madaktari bingwa wazalendo walikuwa watano tu. Anasema utaratibu huo wa madaktari bingwa wa China kuja Zanzibar umekuwa ukiendelezwa ambapo madaktari hao wapo katika hospitali zote kuu za Unguja na Pemba. Kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 2013 zaidi ya madaktari wa China waliokuja Zanzibar kwa ajili ya matibabu wamefikia 200.

Mwandishi wa kitabu cha historia ya Abeid Amaan Karume na Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Shaaban, anasema Mapinduzi ya Zanzibar yalizusha mivutano kwa mataifa makubwa huku kila mmoja akitaka ‘kujipendekeza kwa Zanzibar’ na kukubalika. Shaaban anasema hata hivyo Karume aliliona hilo mapema na kuchukua tahadhari ambapo katika juhudi za kukata mzizi wa fitina alitangaza kufungwa mara moja kwa kituo cha upelelezi cha kijeshi cha Marekani kilichokuwa Tunguu wilaya ya kati Unguja. Kituo hicho kilichojulikana kwa jina la “Mercury project” kwa ajili ya mawasiliano ya anga za juu kilifungwa rasmi Aprili 7, mwaka 1964. Aidha Karume alitangaza kufukuzwa kwa Balozi wa Marekani nchini Zanzibar, Frank Calucci na Ofisa wa Ubalozi Robert Gordon Februari 16 mwaka 1964 ambao walituhumiwa kufanya njama za upelelezi na kutaka kuipindua Serikali halali ya wananchi wa Zanzibar ikiongozwa na Karume.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi