loader
Picha

Mbarawa asifu mnara kuongozea ndege Pemba

WAZIRI wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa Mradi wa Ukarabati Mnara wa Kuongozea Ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Pemba, kutaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kuongozea ndege na usalama wa sekta.

Mradi huo umegharimu Sh.milioni 3.1 zilizotolewa na serikali kupitia Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo ina jukumu la kisheria la kusimamia sekta ya usafiri wa anga, ikiwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza majukumu ya Muungano. Mbarawa alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kukabidhi mradi huo, ikiwa ni maandalizi ya Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Profesa Mbarawa alisema hatua hiyo, itasaidia kuongeza imani ya watumiaji wa uwanja huo na anga ya Tanzanaia, hivyo kuvutia wawekezaji wengi. “Wito wangu ni kwa wadau wote wa sekta ya usafiri wa anga kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili kuhakikisha tunafikia malengo ya serikali ya kuifanya Tanzania nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025, hili linawezekana endapo kila mmoja wetu atafanya wajibu wake,” alisema.

Alisisitiza kuwa shughuli hiyo ya kukabidhi mradi huo wa ufungaji vioo mnara wa kuongozea ndege, inachangia ustawi wa sekta ya usafiri wa anga na uchumi wa nchi hasa sekta ya usafirishaji na utalii. Alisema kupitia mradi huo, zimefanyika kazi kubwa ikiwemo kubadilisha vioo vyote vinavyozunguka mnara wa kuongozea ndege pamoja na kurekebisha paa na kuzuia kuvuja. Pia kumewekwa vizuizi vya usalama, mfumo mpya wa viyoyozi, mfumo wa umeme, mfumo wa simu na data, ceiling upya na kupaka rangi.

“Hafla hii inafanyika ikiwa ni miezi minne tu tangu kuzinduliwa kwa mradi wa Mfumo wa Kuongoza Ndege Kutua Salama yaani Instrumental Landing System- ILS kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA). Naambiwa mandalizi ya utekelezaji wa mradi huu wenye thamani ya shilingi bilioni 4.6 yanaendelea vizuri na ujenzi utaanza muda wowote kutoka sasa. “TCAA inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ufungaji mfumo wa rada nne za kuongozea ndege ambao unatekelezwa kwa thamani ya shilingi bilioni 67.3.

Tayari rada ya kwanza kati ya nne zinazotarajiwa kufungwa, imefungwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA),tayari rada itakayofungwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, imewasili nchini na imeshasafirishwa kwenda Mwanza. Rada nyingine zinatarajiwa kufungwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Songwe,” alisema.

Alisema mbali na uimarishaji wa miundombinu ya kutoa huduma za uongozaji ndege unaotekelezwa na TCAA, serikali pia imeendelea kuimarisha Kampuni ya Ndege (ATCL) na wiki chache zilizopita ilipokea ndege mpya kabisa aina ya Airbus A220-300, ambayo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na ndege ya aina hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema kwa mara ya kwanza mnara huo umefanyiwa ukarabati mkubwa tangu ulipojengwa mwaka 1974. Alisema kufanyika ukarabati huo mkubwa, kumeboresha mazingira ya kazi, ufanisi wa utendaji na usalama wa sekta ya usafiri wa anga. Aliongeza kuwa ukarabati huo wa mnara, umefanywa na kampuni ya ujenzi ya Future Century. Mkataba wa ukarabati ulitiwa saini na mkandarasi na Mamlaka ya Usafiri wa Anga mwezi Oktoba 2017 kwa gharama ya Sh.milioni 300.

Aliongeza kuwa idadi ya ndege zinazohudumiwa na uwanja huo wa Pemba, imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, hivyo kuhitaji uboreshwaji wa mazingira ya kufanyia kazi na vitendea kazi. “Kwa sasa kiwanja hiki kinarekodi miruko ya ndege 114, 660 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa safari 9,555 kwa mwezi,” alisema. Johari alisema inakadiriwa abiria 8,844 hutumia uwanja huo kwa mwaka, ikiwa ni wastani wa abiria 737 kwa mwezi. Uzinduzi huo wa mnara wa kuongozea ndege ni mwendelezo wa utekelezaji wa miradi kadhaa inayotekelezwa na TCAA, kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga hapa nchini.

Alisema TCAA imedhamiria kutekeleza azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda, kwa kuboresha miundombinu ya kuongozea ndege, kuweka mazingira yenye ushindani wenye tija kwenye sekta pamoja na kuimarisha wataalam wake wanaosimamia udhibiti wa sekta ya usafiri wa anga, hivyo imeendelea kuimarisha Chuo chake cha Usafiri wa Anga (CATC), kwa kununua mtambo wa kisasa wa kufundishia waongoza ndege.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi