loader
Picha

Vivimbe kwenye mayai ya kike

UVIMBE kwenye ovari unaweza kusababishwa na mambo au magonjwa mbalimbali.

Vivimbe vinavyosababishwa na matatizo ya homoni huleta ugonjwa unaoitwa kitaalamu “Polycystic ovary syndrome” au kwa kifupi PCOS.

PCOS huwapata kinamama walio kwenye umri wa kupata mimba na sifa zake kuu ni kuwa na vivimbe vyenye maji maji kwenye ovari pamoja na mabadiliko mengine ya mwili yanayoletwa na hitilafu katika uwiano kati ya homoni za kike na zile za kiume.

Ovari zinahifadhi mayai ambayo yanapevuka kila mwezi na kuleta mabadiliko ya mwanamke pamoja na kupata hedhi.

Mfumo wa uzazi huratibiwa na uwiano wa homoni mwilini ambapo kwa mwanamke homoni za kike zinakuwa nyingi zaidi na kwa mwanaume zile za kiume zinakuwa nyingi.

Hitilafu katika uwiano wa homoni kwa upande wa mwanamke unaweza kusababisha mayai yasipevuke kwa ukamilifu au yasitoke kwenye mfuko wa ovari pale yatakapopevuka.

PCOS husababisha mzunguko wa hedhi kutokuwa mzuri au hedhi kutotokea kabisa kwenye baadhi ya miezi. Matokeo yake huwa ni ugumba (PCOS ni mojawapo ya sababu ya kushindwa kupata mimba wa wanawake wengi).

Ovari za mtu mwenye PCOS hutengeneza vivimbe vingi vidogo dogo ambavyo vinakuwa na maji. Sababu hasa inayoleta ugonjwa wa PCOS haijulikani na tiba zinaweza zisimalize tatizo moja kwa moja. Hata hivyo watu wenye PCOS wanaishi maisha yao ya kawaida bila kuwa na tatizo lolote.

Dalili kuu za PCOS ni pamoja na kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi (ikiwa ni pamoja na kuruka miezi bila kupata hedhi); kuongezeka uzito; kuwa na nywele nyingi kwenye maeneo ambayo kwa kawaida hayaoti nywele kwa mwanamke; kuwa na chunusi nyingi usoni; kushindwa kupata ujauzito.

Ili mtu awe na PCOS ni lazima angalau aonyeshe dalili katika maeneo mawili kati ya matatu ambayo ni homoni nyingi za kiume, mzunguko wa hedhi unaovurugika vurugika na vivimbe kwenye ovari ambayo honekana kwenye kipimo cha Ultrasound.

Madhara ya PCOS ni pamoja na uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari au moyo, kushindwa kupata ujauzito, mimba kutoka,saratani ya kwenye mfuko wa uzazi na msongo wa mawazo.

Tiba ya tatizo la PCOS hutegemea dalili zilizotokea. Shida kubwa ambayo inasababisha watu wenye PCOS wafike hospitalini ni kushindwa kupata ujauzito.

Zipo aina kuu tatu za matibabu ambayo mtu mwenye PCOS atapatiwa, ambayo ni pamoja na kubadili mfumo wa maisha na matibu ya vidonge.

Kupunguza uzito kwa wale wenye uzito mkubwa paomoja na kula lishe bora husaidia hasa kwa wale wenye uzito mkubwa ua kusukari.

Matibabu ya tatizo la kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi ni pamoja na vidonge ambavyo vinaweza kuweka sawa uwiano wa homoni mwilini.

Tiba kwa ajili ya nywele nyingi kwenye maeneo yasiyotakiwa hufanyika kwa njia mbalimbali (kama tulivyoelezea kwenye Makala zilizopita).

Kwa wanawake wenye PCOS na wanataka kupata watoto, tiba ya kupevusha mayai hutolewa na baada ya kupata ujauzito, mara nyingi inabidi kutoa tiba ya kuongeza homoni inayosaidia kutunza utauzito.

Ni rahisi kugundua dalili za PCOS mapema, hivyo endapo dalili zimetokea ni vema kwenda kwa wataalamu wa afya, hasa madaktari bingwa wa magonjwa ya homoni au magonjwa ya kina mama, ili kupata ushauri.

Ushauri ukipatikana mapema utaepusha usumbufu hasa pale muda wa kutafuta ujauzito unapofika.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi