loader
Picha

Tamasha la Siku ya Ruzinga linavyosisimua elimu wilayani Misenyi

Ruzinga ni miongoni mwa kata 20 wilayani Missenyi katika Mkoa wa Kagera. Kata hii imefanikiwa kuchangia na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika masuala ya elimu kupitia kwa wananchi wake ambao ni wazaliwa wanaoishi ndani na nje ya kata hiyo.

Mafanikio hayo katika elimu yanabainika katika Tamasha la Siku ya Ruzinga (Ruzinga Day) lililoanzishwa miaka13 iliyopita likiwa na kaulimbiu isemayo: “Punguza Michango ya Harusi na Sherehe ili Kuchangia Maendeleo ya Kata Ruzinga”. Tamasha hili hufanyika Desemba 31, kila mwaka. Tamasha la Ruzinga Day limekuwa kivutio kwa wakazi wa Kata ya Ruzinga, kata, wilaya, mikoa jirani na hata sehemu nyingine za nchi hali inayowakusanya hata viongozi mbalimbali wa kitaifa ili kujionea tamasha hili.

Mvuto wa tamasha hili unachangiwa na mambo mengi ukiwamo ubunifu wa kimaendeleo unaowafanya wakazi wa kata hiyo na wengine wenye mapenzi mema, kuhusishwa moja kwa moja kuchangia maendeleo ya kata hususani suala la elimu. Mwenyekiti wa Ruzinga Day, Elizabert Rugenga anasema tamasha lilianza kama sehemu ya kuiunganisha jamii ya waishio ndani na nje ya kata ili kujenga jamii shirikishi inayoweza kutatua changamoto zake kwa mfumo wa kuchangia maendeleo bila kusubiri serikali kuifanyia kila kitu. Anasema kama chachu ya maendeleo, tamasha hilo limefanikiwa kuondoa tatizo la wanafunzi waliokuwa wanapata alama ndogo za ufaulu katika shule za msingi.

Kwa mujibu wa Rugenga, hivi sasa shule zote za msingi zinapata alama ‘B’ na watoto wanaendelea na masomo ya sekondari. “Kitu ambacho kilikuwa kinatuumiza vichwa sisi kama Wanaruzinga, ni kuona watoto ambao wanahitimu elimu ya msingi wanashindwa kuendelea na masomo ya sekondari,” anasema. “Fedha tunazozikusanya kupitia tamasha hili, tunazitumia pia kuajiri walimu na kuwalipa hali ambayo imeongeza ufaulu… Tunanunua vitabu vya kiada vinavyoendana na silabasi ya shule pamoja na kuhimiza wazazi na sisi wadau kuhakikisha watoto wanapata uji ili kuimalishe lishe shuleni,” anasema.

Anasema kupitia tamasha hilo, tayari maabara mbili za Fizikia na Kemia zimekamilika na zinatumiwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ruzinga. Mafanikio mengine yanayoonekana kupitia Tamasha la Ruzinga Day, ni pamoja na ujenzi wa nyumba mbili za walimu na kusaidia changamoto ya upatikanaji wa nyumba za walimu, pamoja na kuweka mfumo wa kompyuta 15 inayofanya vizuri katika shule hiyo ya sekondari ya kata (Sekondari ya Ruzinga) hali inayowafanya wanafunzi kuendana na teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama).

“Miaka iliyopita hakuna mwanafunzi aliyekuwa anafaulu kwa daraja B kutoka shule ya msingi na hakuna mwanafunzi aliyekuwa anafaulu kujiunga na kidato cha tano, lakini kwa sasa imekuwa kawaida katika shule yetu ya kata kupata wanafunzi wengi wanaofaulu hadi kidato cha tano, wanaojiunga katika vyuo,” anasema. “Kutokana na mchango mkubwa wa Tamasha la Ruzinga Day katika maendeleo ya elimu katani Ruzinga, tunataka mwaka huu wa 2019 tuondoe sifuri zilizokuwapo kwa wanafunzi wawili mwaka jana,” anasema Rugenga.

Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Deodorus Kamala ni miongoni mwa wadau wanaojivunia mafanikio ya tamasha hilo. Uchunguzi umebaini kuwa, mwaka 2017 Kamala alitoa motisha kwa Uongozi wa Ruzinga Day na kuwapeleka Dodoma kisha kuwakutanisha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Technolojia. Anasema safari hiyo, iliwawezesha wadau hao kuwasilisha mikakati yao ya kuinua elimu katika kata yao kupitia tamasha hilo na ndipo bweni la wasichana likapatikana. Bweni hilo limekamilika na lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 120. Bweni hili limekuwa mkombozi kwa wanafunzi wengi waliokuwa wanatembea umbali mrefu kufuata elimu katika shule hiyo.

“Nilitoa motisha ya kuwapeleka wajumbe hawa wa tamasha ili kuwasilisha mawazo yao kwa waziri na bahati nzuri, waziri hakututupa; alitupatia bweni ambapo pia wananchi wamechangia nguvu zao,” anasema Kamala. Anaongeza: “… hakuna kisichowezekana serikali iko kazini, lakini ni vema wananchi nao wakaendelea kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo yao, badala ya kusubiri kufanyiwa kila kitu na serikali.”

Anasema angetamani kila kata ianzishe tamasha kama hilo jimboni kwake. Kwa mujibu wa Kamala, kwa sasa kata mbalimbali zikiwamo za Kitobo, Bugandika, Ishozi na Bwanjai wamefuata mfano wa Tamasha la Ruzinga Day kwa kuanzisha matamasha makubwa yanayolenga kuinua elimu katika kata zao. Inaelezwa na watu mbalimbali kuwa, mbunge huyo amekuwa msatri wa mbele kutoa motisha na kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi ili kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele katika jimbo lake hali inayoelezwa kuwa, imechangia kupandisha kiwango cha elimu jimboni humo tangu mwaka 2015. Mwaka 2015 Wilaya ya Missenyi ilikuwa na vyumba 521vya madarasa.

Kwa sasa kuna vyumba 650. Kulikuwa na nyumba za walimu 192, lakini sasa zimefikia 205. Matundu ya vyoo yalikuwa 887 sasa yamefikia 915; madawati yalikuwa 15,269 sasa yamefikia 19,786. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha ufaulu wa darasa la saba mwaka huo kilikuwa asilimia 78.8, lakini sasa kimefikia asilimia 83.7. Wakati ufaulu wa mitihani ya darasa la nne ulikuwa asilimia 86, sasa ni asilimia 88 na ufaulu wa mitihani ya kidato cha pili umepanda hadi asilimia 85 kutoka asilimia 74.

Kadhalika, ufaulu wa kidato cha nne umepanda kutoka asilimia 60 hadi asilimia 86 huku ufaulu wa kidato cha sita nao ukipanda kutoka asilimia 70 hadi asilimia 100. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, mwaka 2015 hapakuwa na maabara iliyokuwa imekamilika, lakini mwaka 2018 zimekamilika na maabara zinazotumika ni 31 kati ya 66 . Maabara zilizobaki ziko katika hatua mbalimbali na zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020. Kamala anasema: “Maendeleo ni hatua ni kweli mtu anaweza asijue lakini mimi kama mbunge ninalipa kipaumbele sana sana suala la elimu; hata katika michango yote na kila kitu nahimiza elimu kwanza maana bila elimu hakuna ambacho kitafanyika.”

Anasema ni vizuri wazazi na jamii waelewe kuwa, bila kuwekeza katika elimu tutakwama hivyo, ni vema tushirikiane kuipenda na kuiendeleza elimu. Afisa Mtendaji wa Kata ya Ruzinga, Mectirida Mushunju anasema yeye kama mtekelezaji wa shughuli za kiserikali, imekuwa kazi rahisi kukusanya wananchi kukusanya michango ya maendeleo kwa hiari. Anasema ameshirikiana na uongozi kukamilisha utayarishaji wa rasimu ya katiba ili kufanya usajili utakaowawezesha shughuli zote za tamasha kwa utaratibu unaojitegemea.

“Mimi kama mtekelezaji wa shughuli za maendeleo, naishukuru serikali na Wizara ya Elimu ambayo kupitia tamasha hili inatukumbuka na inatutumia walimu,” anasema. Mashunju anaongeza: “Hii imetusaidia kupata hosteli ya wasichana ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya elimu katika kata hii maana mwanzoni wengi walikuwa wanatembea kilometa 8 hadi 9 kufuata shule ya sekondari na sasa angalau wanaweza kupata eneo la kukaa kama bweni na kujisomea kwa utulivu katika mazingira mazuri.”

Desemba 31, 2017 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alihudhuria tamasha hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni hilo la wasichana. Shule inaitwa Ruzinga secondary ,kamala alicjowezesha kama mbunge ni kugaharamia safari za viongozi wa ruzinga day kuja Dodoma na kuishi Dodoma ili kuwakutanisha na waziri wa elimu na kuwasilisha mikakati yao ya kuinua elimu katika kata yao kupitia tamasha hilo na bweni la wasichana ndo likapatikana ,bweni la wavulana linaumuhumimu wa kujengwa kwa sababu nao wanatoka umbali mrefu vilevile.

Katika tamasha hilo, Profesa Ndalichako alisema wananchi hao wakikamilisha ujenzi wa bweni hilo la wasichana, serikali itawapatia fedha kujenga bweni la wavulana kwa sababu wapo nao wanaotoka mbali hivyo, linahitajika ili kuwawekea wavulana nao mazingira rafiki ya kujifunzia. Bweni hilo limekamilika na linaendeshwa na nguvu ya wazazi. Tayari wasichana wameanza kulitumia na wazazi ndio wanaolipia gharama za watoto wao wanaoishi shuleni hapo Diwani wa Kata Ruzinga, Mtembei Rutagwerela anasema wadau wa maendeleo katika Kata ya Ruzinga, wamenuia kuendelea kujenga nyumba za walimu wa sekondari kwa mwaka 2019.

Mpaka sasa michoro iko tayari na kupitia Baraza la Madiwani, atawasilisha hoja hiyo ili halmashauri iweze kuunga mkono juhudi za wananchi. “Kuna baadhi ya walimu wakipangiwa huku wakikuta hakuna miundombinu rafiki; wanafikiria kuhama sisi kama viongozi kupitia wananchi waliotuchagua ni vizuri tujenge miundombinu rafiki kwanza ya walimu ili kuifanya elimu yetu kuwa juu muda wote,” anasema.

Mmoja wa waanzilishi wa Ruzinga Day ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu, Aspon Mwijage anatajwa kama mtu muhimu katika tamasha hilo. Mwenyewe anasema, haikuwa rahisi kuwaunganisha watu na kuweka kitu kimoja kinachoweza kuwakutanisha wote wanaoishi ndani nan je ya kata. Anasema kwa sasa wanajivunia mafanikio ya kielimu, kiafya na miradi mbalimbali kutokana na umoja walioujenga wanaoutumia kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali. Anasema sasa imekuwa kama desturi na utamaduni wa kila mtu kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo ya eneo lake huku akisisitiza kuwa lazima vijana wanaojiendeleza kielimu, wanaozaliwa jambo hili lizaliwe ndani yao na kukiendeleza.

Baadhi ya mambo yaliyoazimiwa katika tamasha hilo kwa mwaka 2019, ni pamoja na kujenga chuo cha ufundi kitakachowasaida wanaoshindwa kuendelea na elimu ya sekondari ili wajiajiri. Inalezwa kuwa, walimu wastaafu wa vyuo vya ufundi waliopo katika kata hiyo ndio watakaoanza kwa kujitolea kuwafundisa watakaojiunga na chuo kitakapokamilika.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi