loader
Picha

Biteko aikaribisha kampuni ya urani

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko ameitaka kampuni inayochimba madini ya urani katika mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, Uranium One kutosita kuwasiliana naye pindi wanapokutana na changamoto katika utekelezaji wa mradi wao.

Aliyasema hayo katika kikao chake na watendaji wa kampuni hiyo kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma.

Aidha, Biteko alisema maombi yote ya leseni kubwa za uchimbaji wa madini zinawasilishwa katika Baraza la Mawaziri ili kuridhiwa baada ya wawekezaji kuonesha nia na kuwasilisha maombi ya leseni hizo.

Biteko amekiri kuwa ana uelewa wa kile kinachoendelea katika uwekezaji huo kutokana na ushirikishwaji alioupata kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Madini, Angella Kairuki kupitia vikao mbalimbali alivyoshiriki.

Akizungumzia lengo la ujio wao katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uranium One, Frederick Kibodya amesema ni kuelezea maendeleo waliyofikia katika uwekezaji huo pamoja na kumpongeza Biteko kwa kuteuliwa kuongoza wizara hiyo.

Kibodya amesema, “Uteuzi huo umelenga katika kukuza sekta ya madini ikiwa ni pamoja na mradi wa uchimbaji wa madini ya urani”.

Akizungumzia uwekezaji uliofanyika mpaka sasa katika mradi huo, amesema ni dola za Marekani milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 500) kutoka mradi ulipoanza mwaka 2009.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Kibodya amesema ni pamoja na kusaidia katika kukuza teknolojia nchini. Alisema madini hayo yakichimbwa yanatumika katika kuzalisha umeme ambayo ni teknolojia mpya nchini.

Mradi utasaidia katika kuongeza ajira nchini. Aliendelea kufafanua kuwa kwa kipindi cha ujenzi wa mradi wanatarajia kuajiri Watanzania 1,600 kwa kipindi cha miezi 18.

Alibainisha kuwa kutakuwepo na uzalishaji wa ajira zisizo rasmi kiasi cha watu 4,500 wakati wa ujenzi na 2,300 pindi uzalishaji utakapoanza.

Amesema mradi utasaidia katika kuhamisha utaalamu kutoka kwa wawekezaji kwenda kwa wazawa na mradi umelenga katika kutoa elimu ya ajira na utaalamu kwa wazawa.

Pia Kibodya amesema mradi unatarajia kuliingizia Taifa pato la dola za Marekani milioni 220 kama kodi kwa mwaka, kiasi ambacho kitakuwa kikibadilika kadri uzalishaji unavyoongezeka.

Mradi wa uchimbaji madini ya urani katika mto Mkuju unafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na mbia wa Kampuni ya Mantra anayejulikana kama Rosatom.

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) ni moja ya sekta zilizonufaika ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi