loader
Picha

Wakandarasi mji wa Serikali waongeze bidii

SERIKALI inajenga mji wake mpya Ihumwa ambako ofisi za wizara zinajengwa kwa ajili ya makao makuu mapya.

Katika kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa, Serikali ilitoa zabuni kwa makandarasi kadhaa wakiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Suma JKT.

Mara kadhaa viongozi waandamizi wa Serikali wamekagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya wizara hizo zitakazokuwa mji huo Dodoma na kuagiza makandarasi husika waongeze bidii.

Juzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliungana na viongozi wengine, mawaziri na pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutembelea kazi za ujenzi zinazoendelea katika mji wa Serikali.

Kama viongozi wenzake, aliagiza kasi ya ujenzi kuongezwa na mkandarasi, NHC na wengine pia ili azma ya Serikali kukamilisha ofisi itimie.

Tumekuwa tukifuatilia ziara za viongozi hao na tunaungana nao kuwataka kandarasi waliopewa kazi hiyo kuhakikisha wanajipanga kumaliza kazi zao ndani ya muda na kwa ufanisi mkubwa.

Hatua ya Serikali kuhamia Dodoma ambako sasa kumekuwa ndio makao makuu ya nchi si ya mchezo. Inahitaji maandalizi makubwa ya ofisi za serikali na miundombinu mingine ya kijamii.

Ndio maana tunalazimika kuwataka kandarasi hao wajue wanao wajibu mkubwa kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kukamilisha mji wa serikali wananchi wapate huduma safi. Kuchelewa kwao ni kufanya wizara mbalimbali zilizokwishahamia Dodoma zishindwe kutoa huduma nzuri kwa wananchi au kwa ufanisi mdogo kutokana na kukosa ofisi za kutosha. Sisi tunaamini, wakandarasi hawana sababu ya kushindwa kukamilisha kazi hiyo katika muda kwani wengi wamekamilishiwa malipo na vifaa. Ni kwa msingi huo tunaomba wajipange upya wakijua dhamana waliyobeba kufanikisha ofisi za Serikali kukamilika haraka ni kubwa mno.

Wajipange wakijua wazi kuwa dhamira kuu ya serikali kuhamishia makao makuu ya nchi huko ni kupeleka huduma kwa wananchi karibu zaidi.

Itakuwa si vyema wakishindwa kukamilisha ofisi hizo katika muda muafaka na kufanya wananchi washindwe kuhudumiwa vizuri.

Kuchelewa kumalizika kujengwa kwa ofisi hizo hakuna maana zaidi ya kusababisha ufinyu wa maeneo ya utoaji huduma ukizingatia wizara nyingi zinatumia ofisi za taasisi za chini yao.

Tunaomba wakandarasi watumie muda uliobaki kuongeza raslimali watu ili kasi ya ujenzi huo iendane na malengo ya kumalizika mwezi huu. Wakifanya hivyo, watakuwa wamemtendea haki Rais John Magufuli aliyechagiza kuhamishia Serikali Dodoma lakini pia wananchi wenyewe.

Sisi tuna imani wakandarasi waliopewa kazi hii wana sifa za kutosha kumaliza kazi ndani ya muda kwani walionesha hivyo maeneo mengine.

Ni vizuri basi wakaendelea kuonesha utayari wao katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo ya haraka yatakayowanufaisha wananchi wengi.

MKUTANO wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi