loader
Dstv Habarileo  Mobile
Umuhimu wa Kiswahili katika elimu ya uraia

Umuhimu wa Kiswahili katika elimu ya uraia

Leo katika mfululizo wa kujifunza masuala mbalimbali katika lugha yetu adimu ya Kiswahili na ili kuwawezesha kuweza kuifahamu Tanzania ambayo ni muasisi katika matumizi ya lugha ya Kiswahili na kuwajengea pia uzalendo kwa taifa.

Tutajifunza kuhusu alama za Taifa la Tanzania ili kuwawezesha wageni kufahamu mambo muhimu katika taifa hili lililoasisi lugha ya Kiswahili na ambalo lugha hii inatumika kama lugha kuu ya mawasiliano na kujifunzia katika ngazi za msingi.

Alama za taifa ni vielelezo muhimu kuhusu tabia, historia, hali na msimamo wa nchi. Tunaweza kujifunza mambo mengi kuhusu taifa letu na mataifa mengine kutokana na alama za nchi inayohusika.

Baadhi ya alama za taifa letu ni: Wimbo wa Taifa: Kila taifa lina wimbo unaolitambulisha. Wimbo huo huimbwa katika matukio muhimu ya kitaifa. Nchi yetu inao wimbo wake wa taifa.

Kila mwananchi hana budi kusimama na kutulia wakati wimbo wa taifa unaimbwa. Kusimama na kutulia wakati wimbo wa taifa unaimbwa ni kuonesha heshima kwa wimbo wa taifa. Wimbo wa taifa huimbwa katika nyakati mbalimbali, zifuatazo ni baadhi ya nyakati hizo; • Rais wa nchi yetu, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wanapotembelea nchi za nje.

Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu ni wawakilishi wa nchi yetu wanapokuwa nje ya nchi. Hivyo wanapotembelea nchi za nje, wimbo wa taifa letu huimbwa. Hiyo huwa ni ishara ya heshima ya kuwakaribisha na kuwatambulisha nchi wanayotoka.

(b) Rais wa nchi nyingine anapotembelea nchi yetu Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wa nchi nyingine anapotembelea nchi yetu wimbo wa taifa letu huimbwa, kama ishara ya kumkaribisha mgeni wetu.

Pia wimbo wa taifa wa nchi anayotoka kiongozi huyo wa nchi huimbwa ili kutambulisha nchi anayotoka. (c) Rais anapolihutubia taifa kabla na baada ya kumaliza hotuba.

Kabla rais hajalihutubia taifa kupitia redio na televisheni, wimbo wa taifa huimbwa.

Wimbo wa taifa hutoa ishara ya kuwatayarisha wananchi kumsikiliza rais kwa makini. Pia rais anapomaliza kulihutubia taifa wimbo wa taifa huimbwa kama ishara ya kuwajulisha wananchi kuwa rais amemaliza kutoa hotuba.

(d) Wakati wa kufungua na kufunga matangazo ya Redio Tanzania na Televisheni ya Taifa wimbo huimbwa ikiwa ni ishara ya kuanza na kumalizika kwa matangazo kwa siku husika.

(e) Wakati timu yetu ya taifa inapocheza na timu ya taifa lingine wimbo wa taifa huimbwa kama ishara ya kuiwakilisha nchi yetu katika michezo ya kimataifa. Pia, wimbo wa taifa huimbwa kama ishara ya kucheza kwa amani.

(f) Kunapotokea kifo cha Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wimbo wa taifa huimbwa kama ishara ya kutangazwa kwa kifo cha mkuu wa nchi, Makamu, au Waziri Mkuu wake.

Ujumbe uliomo kwenye wimbo wa taifa Ubeti wa kwanza una ujumbe wa kuombea mambo mema Afrika na viongozi wake. Pia kumwomba Mwenyezi Mungu atupe baraka sisi watoto wa Afrika.

Msisitizo mkubwa katika ubeti huu ni viongozi wawe na hekima katika uamuzi wao ili kudumisha umoja na amani. Katika ubeti wa pili ni dua ya kuiombea Tanzania na watu wake.

Na ubeti huu pia unasisitiza kudumishwa kwa uhuru na umoja kwa Watanzania wote. Ubeti unamalizia kwa kumwomba Mwenyezi Mungu atupe baraka sisi watoto wa Tanzania.

Nembo ya Taifa: Nembo ya Taifa ni kielelezo cha umoja, uhuru na nguvu za taifa katika kujihami na kujilinda. Kuna alama mbalimbali katika nembo yetu ya taifa. Zifuatazo ni alama zilizopo na maana ya kila alama; Mwanaume na mwanamke: Kielelezo cha nguvu itokanayo na umoja wa Watanzania.

Bendera ya taifa: Huelezea utaifa wetu. Shoka: Huwakilisha wafanyakazi Jembe: Huwakilisha wakulima

Mwenge: Ni kielelezo cha Uhuru wa Taifa.

Pembe za ndovu: Kielelezo cha maliasili za taifa letu. Mkuki: Ni kielelezo cha silaha za jadi.

Mawimbi ya bahari; Bahari iliyopo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Karafuu na pamba: huwakilisha mazao ya biashara.

Mlima Kilimanjaro; Mlima mrefu kuliko yote katika Afrika, ni fahari ya Tanzania.

Uhuru na Umoja: Ni maeneo yanayoeleza msimamao wa Tanzania ambao nguvu zake zinaegemea uhuru na umoja wa watu wake. Rangi ya manjano: Ni kielelezo cha madini yetu

Rangi nyekundu: Ni kielelezo cha udongo wenye rutuba uliopo katika nchi yetu. Nembo ya taifa huwepo katika bendera ya rais, gari analopanda Rais, Makamu wa Rais na Ikulu.

Pia huwepo kwenye nyaraka za serikali na fedha. Bendera ya Taifa Kila nchi iliyo huru ina bendera yake ya taifa.

Bendera ya Taifa ni kitambulisho cha kuonesha kuwa nchi hiyo ni huru. Watanzania tuna bendera yetu ya taifa inayotambulisha kuwa tuko huru.

Bendera yetu ya taifa ina rangi nne.

Rangi hizo ni kijani, njano, nyeusi na bluu. Kila rangi katika bendera yetu ya taifa ina maana maalumu. Maana ya kila rangi katika bendera yetu ya taifa ni kama ifuatavyo: •

Kijani: Rangi hii humaanisha uoto na mimea yetu.

• Njano: Humaanisha madini yaliyo nchini mwetu.

• Nyeusi: Huwakilisha rangi ya Watanzania ambao ni waafrika weusi

• Bluu: Rangi hii humaanisha bahari, maziwa na mito iliyomo nchini mwetu.

Tunatakiwa kuiheshimu bendera yetu na kutambua maana ya kila rangi iliyomo.

Fedha za nchi yetu Fedha ni moja ya alama za taifa letu.

Fedha ya nchi yetu ipo katika sarafu na noti. sarafu huanzia shilingi 50 hadi shilingi 500. Noti huanzia shilingi 500 hadi 10,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bb5cf8b6cb3b029564c1033851c7f393.jpg

JUNI 28, 2021 wakati akizungumza ...

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi