loader
Picha

Serikali yaajiri wahitimu wote Chuo cha Bandari

WAHITIMU 196 katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Bandari, jana walijikuta wakisheherekea mahafali hayo kwa furaha za kipekee.

Hali hiyo inatokana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kuagiza wote wapewe ‘ajira mara moja’ katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Akitangaza uamuzi huo katika mahafali hayo jana, Kamwelwe alisema hatua hiyo imelenga kupunguza tatizo la upungufu wa wafanyakazi hao, ambapo alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko kushughulikia suala hilo haraka.

Kamwelwe alisema kutokana na mahitaji makubwa, yanayoendana na uboreshaji wa miundombinu ya bandari hiyo, kundi hilo la watahiniwa litasaidia kupunguza changamoto iliyopo hususani kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli inatekeleza miradi mbalimbali. “Nimesema hivyo kwa sababu kuna nafasi 200 pale Bandari, hakuna haja ya kufanya matangazo katika suala hilo, najua zipo taratibu za kisheria katika hili lakini mimi, Mkurugenzi wa TPA pamoja na Bodi tutaongozana moja kwa moja hadi kwa Waziri Geogre Mkuchika (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) ili kuliweka sawa” alisema Kamwelwe.

Aidha, akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kakoko alisema kimsingi agizo lolote linalotolewa na Waziri linatekelezwa. Alisema kwamba kutokana na hatua hiyo, TPA itaanza utaratibu wa kuwaajiri wahitimu hao kwa awamu kwa ajira za muda kuanzia Februari Mosi mwaka huu. Pamoja na agizo hilo lililopokelewa kwa ‘nderemo na vifijo’ na wahitimu hao, Kamwelwe alisema serikali itaendelea na maboresho ya chuo hicho ili kukifanya kuwa moja ya vyuo bora, vinavyotoa elimu ya masuala ya bandari na bahari.

Alisema maboresho hayo yatafanyika kabla ya mwaka 2025 ambapo uchumi wa dunia utakuwa unaelekea katika matumizi ya bahari. Alisema katika kutekeleza hilo, serikali pia imekuwa ikifanya maboresho mbalimbali, ikiwemo ya upanuzi wa bandari ikiwemo ujenzi wa bandari kavu na uongezaji wa kina katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuziwezesha meli kupakia na kushusha mizigo mbalimbali kwa urahisi.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo hicho, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kakoko, alisema ili kukifanya chuo hicho kuwa na tija, wameanza mpango wa kukiboresha, unaoendana na ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa mtambo wa kupakia na kupakua mizigo bandarini ili kuongeza kiwango cha uelewa kwa wanafunzi. Pamoja na hilo, alisema kuanzia Julai Mwaka huu, chuo kitaanza kujiteemea, hatua ambayo pia itakiwezesha kufanya manunuzi yake mbalimbali. Kakoko alimuomba Waziri kukisaidia chuo hicho kurejesha sehemu ya majengo yake, ambayo yalitolewa kisheria kwa Chuo cha Utalii, ambacho sasa tayari jengo yake lililopo Posta limekamilika.

Alisema hatua hiyo itawezesha chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo yake kama kawaida. Mkuu wa Chuo cha Bandari, Joseph Kakeneno alisema mipango ya chuo hicho ni kukiwezesha kudahili wanafunzi hadi 800 ifikapo Machi mwaka huu ili kufanikisha malengo yake ya kuzalisha wahitimu katika uwakala wa forodha na usafirishaji, usafirishaji na uchukuzi na fani zingine. Nao baadhi ya wahitimu wa mahafali hayo, Alex Ndunguru na Jackline Hussein waliipongeza serikali kwa hatua hiyo. Waliahidi kufanya kazi kwa nguvu zote ili kuendeleza juhudi za kuliletea taifa maendeleo.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imewataka wadau wa habari kufanya utafiti ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi