loader
Picha

Serikali imulike shule zake

Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) wiki hii limetangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Nne kwa mwaka 2018, ambapo shule binafsi, zikiwemo seminari, zimeendelea kutesa kwa kuongoza.

Kwa mfano, shule za Kanisa Katoliki zilizomo katika shule 10 bora kitaifa katika matokeo hayo ni St Francis ya Mbeya, Marian Boys ya Bagamoyo, Marian Girls pia ya Bagamoyo, Maua Seminari ya Kilimanjaro na Precious Blood ya Arusha.

Tunaungana na wadau wa sekta ya elimu nchini, kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu vizuri katika mitihani hiyo. Tunawataka walioshindwa, kutumia fursa hiyo kuangalia walipokosea na kurekebisha.

Kwamba katika mtihani wowote, lazima awepo mshindi na wa mwisho.

Hilo ni jambo la kawaida, lakini kinachogomba ni kiwango cha kutofaulu.

Ni aibu kwa shule za sekondari, kushindwa kupata matokeo mazuri wakati huu ambapo serikali imeamua kuwekeza zaidi katika elimu kwa kutoa elimu bila malipo na kuboresha miundombinu shuleni.

Tulitarajia walimu na wanafunzi wao katika shule, hasa za serikali, wangeunga mkono hatua ya serikali kutumia mabilioni ya shilingi, kutoa elimu bila malipo kuongeza ufaulu maradufu.

Walikuwa na nafasi ya kufanya hivyo, kwa kuwa changamoto nyingi zilizokuwa zinakabili shule nyingi zimeondolewa na utoaji elimu bila malipo ;na kazi iliyobaki ni wanafunzi kusoma.

Iweje basi pamoja na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, kutumia gharama kubwa kuziwezesha shule zake, bado wanafunzi wanashindwa kufaulu.

Ni kutokana na kushindwa kwa shule za serikali kuingia kwenye 10 bora kitaifa, tunalazimika kuitaka serikali ichukue hatua kwa wahusika.

Ilifanya hivyo mwaka jana kwa Shule ya Wasichana Jangwani, kwa kuhamisha nusu ya walimu na kuleta wapya na matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne,yameanza kuonesha nuru.

Ni wazi kupitia Jangwani, jamii inajifunza kuwa baadhi ya walimu wanashindwa kuwajibika vyema, kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu.

Ni vyema basi hatua zaidi zichukuliwe na wizara husika kwa shule nyingine zilizoshindwa kung’ara kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka huu ili walimu na wanafunzi wawajibike.

Bila kufanya hivyo, uwekezaji mkubwa wa fedha za elimu bila malipo, unaofanywa na serikali utakuwa ni kama kucheza pata potea.

Na bahati mbaya elimu haina mchezo wa pata potea, bali inataka umakini katika uwekezaji wake, ufundishaji wa walimu, wanafunzi nao kusoma kwa bidii na wazazi kusimamia maadili.

Kabla ya kuliangamiza Taifa kwa kuandaa wasomi vihiyo, ni vyema hatua stahiki na za haraka, zikachukuliwa kwa shule zilizofanya vibaya na hasa zenye mwendelezo wa kufeli.

Changamoto inayotoka kwa shule binafsi na hasa seminari, ni somo tosha kwa shule za serikali, kuongeza bidii katika masomo na kazi.

Seminari zimeendelea kutesa katika matokeo na kila mara, kwa sababu ya uwekezaji wao katika bidii ya sala, kazi na masomo ambayo yamekuwa msingi mkuu wa kila mwanafunzi.

Kama seminari na shule nyingine za binafsi, zimeweza kufanikiwa kwa kusimamia hayo, vipi shule za serikali zishindwe, kama si uzembe.

MKUTANO wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi