loader
Picha

Upotoshaji huduma za afya ukomeshwe

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema gharama za matibabu nchini hazijabadilika badala yake zimezidi kupungua ili wananchi wengi wamudu.

Imesema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi kukanusha madai yaliyoenezwa kwenye mitandao ya jamii na mwananchi.

Mwananchi huyo, Hamenya Salehe anadaiwa kuandika gharama za kujifungua hospitalini zitakuwa Sh 300,000, kadi ya kliniki Sh 25,000. Pia alidai wagonjwa wa Ukimwi na Kifua Kikuu watakuwa wanajigharamia matibabu na watu kujinunulia dawa za uzazi wa mpango.

Tunaungana na wizara kukemea upotoshaji huu mkubwa uliofanywa na watu wenye nia ovu dhidi ya Serikali na wananchi wake kwa jumla.

Ni kwa msingi huo tunawaomba wananchi wote kupuuza habari hizo kwani hazina ukweli badala yake, waendelee kuiamini Serikali yao makini na kufuata taarifa za afya na miongozo inayotoa.

Tunaomba taasisi za dola zinazohusika na usalama wa nchi hasa mitandaoni kuwachukulia hatua wote waliohusika na upotoshaji mkubwa. Habari hizo si nzuri hata kidogo na zitakuwa zimewaletea wananchi wengi, hasa wagonjwa, mtafaruku na hofu kinyume na hali halisi ilivyo.

Ndio maana tunasema, upotoshaji huu haufai kuachwa uendelee na hivyo iko haja kwa watu wanaohusika na usalama, kuwachukulia hatua kali, waliohusika iwe fundisho kwa wengine.

Tunaipongeza wizara kwa kutoa ufafanuzi huu wa haraka na kuwatoa wananchi hofu ambayo ingewagombanisha bure na Serikali yao sasa. Tunaomba wananchi hasa wagonjwa waendelee kuiamini Serikali yao makini chini ya Rais John Magufuli na mawaziri wanaohusika na afya, Ummy Mwalimu na Dk Faustine Ndugulile.

Wakae wakijua kuwa Serikali hii inayo nia thabiti ya kuondoa changamoto zote za afya nchini kuanzia miundombinu, vitendea kazi, raslimali watu kama madakatri na wauguzi pia.

Ni umakini huo na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi wake, Rais Magufuli amevunja rekodi ya kupeleka fedha za kutosha kujenga vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na za rufaa za mikoa mbalimbali nchini.

Ni ajabu kiongozi makini, mwenye uchungu na watu wake kama Rais Magufuli anayefanya mambo makubwa kama kutoa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kununua dawa kwa ajili ya wagonjwa kukiuka dhamira yake kuwahudumia.

Ni vyema wanaotunga uongo kama huo wakawa wakweli katika nafsi zao na kukubali kazi nzuri anayofanya Rais Magufuli katika kuwaletea watu wote bila ubaguzi, maendeleo makubwa.

Badala ya kuunda uongo kama huo kwa nia ovu, ni vyema wakamuunga mkono kwa kutumia mitandao vizuri kutangaza mazuri anayofanya wakitaarifu wananchi uwepo wa huduma nzuri. Kinyume chake, tutawaona ni wasaliti ambao wameamua kutumiwa na mabeberu kutukwaza.

Na kama hivyo ndivyo, wajue hawatafanikiwa.

MKUTANO wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi