loader
Picha

Namna bora kutunza macho

MACHO ni viungo muhimu katika mwili wa binadamu na hata kwa wanyama na viumbe wengine kutokana na upekee wa kazi yake. Hii ni kwa kuwa macho ndiyo yanawezesha kuona wanapokwenda, wanachofanya na kubaini vitu wanavyotaka ili kuviongeza ubora.

Ni kwa kupitia kiungo hiki katika mfumo wa fahamu, mtu anaona kitu au picha na kufanya uchaguzi au uamuzi maana yanayoyaona, yanaweza kuwa mabaya au mazuri.

Kimsingi, jicho ni kiungo katika mwili kinachohitaji uangalizi makini na wa kipekee katika kukitunza ukiwamo wa kiafya dhidi ya magonjwa na madhara mbalimbali.

Magonjwa ya macho Haya ni matatizo yanayoshambulia macho kwa namna mbalimbali na kwa sababu tofautitofauti kwani licha ya kupata maambukizi, yanaweza kuwa maradhi hayo yametokana na sababu nyingine.

Miongoni mwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na athari za magonjwa ya macho, ni pamoja na kumfanya mtu apungukiwe au akose kabisa uoni. Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, yapo magonjwa mengi ya macho yakiwamo yanayoambukizwa kwa nzi, kama vile trakoma.

Mengine hutokana na mionzi inayoweza kuwa ya jua, runinga na hata tarakilishi (kompyuta) vinasababisha macho kutofanya kazi vizuri, mathalani kushindwa kuona mbali, au karibu na pia kusababisha kichwa kuuma. Kwa mujibu wa chapisho la kimtandao la Wikipedia, magonjwa yote ya macho yanatibika kutegemea hatua ya ugonjwa.

Wikipedia unasema: “Kuona karibu kunaweza kupona kwa kutumia lenzi mbonyeo na kuona mbali unatumia lenzi mbinuko kwenye miwani yako ambapo humsaidia mgonjwa kuona vizuri na kuweza kutofautisha vitu mbalimbali,.”

Unaongeza: “Ukihisi kama macho yako yanauma unaweza ukala karoti kwa sababu ina vitamini A inayoweza kukusaidia ukiwa na ukavu macho.” Kwa jumla, magonjwa ya macho yanatibika ukiwahi hospitali kwa matibabu zaidi.

Kitaalamu, zipo dalili za ugonjwa wa macho ambazo hazipewi kipaumbele kwa kuwekewa uzito katika upatikanaji wa tiba yake japo ni hatari zaidi kiafya kwa binadamu, hivyo jamii inapaswa kuwa na mfumo wa kupima afya ya macho mara kwa mara kubaini dalili hatarishi mapema na hivyo kupata matibabu.

Akizungumzia ugonjwa huo katika Maadhimisho ya Siku ya Macho Duniani, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe, anasema takribani watu milioni mbili nchini wana matatizo ya macho huku 500,000 kati yao, wakiwa na matatizo yanayoweza kusababisha upofu.

Kuhusu dalili, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Macho ya Kimataifa (International Eye Hospital), Profesa Ugurcan Keskin, anasema kumekuwepo kasumba ya jamii kutokuwa makini katika kupima afya zao juu ugonjwa wa macho.

Dk Keskin anasema ni muhimu kupima macho mara kwa mara ili kupatiwa tiba husika itakayotibika mapema kuliko kusubiri hadi ugonjwa unapojitokeza.

Dalili Keskin anazitaja dalili hatari ambazo hazipewi uzito na jamii kuwa ni macho kuwasha, kutoka machozi, kuogopa mwanga, macho kuwa mekundu na kufikicha macho kila wakati.

Anasema kwamba kimakosa, dalili hizo zimekuwa zikichukuliwa na jamii kama vitu vya kawaida na kwamba ni miongoni mwa visababishi vya uoni hafifu.

“Tatizo pia linachangiwa na kasumba ya baadhi ya watu kukimbilia kumeza dawa wanapopata maumivu ya kichwa bila kujua kuwa, hiyo ni dalili ya mamatatizlo mengi ikiwamo ya kuugua macho,” anasema.

Anaongeza: “Watu wengine hukumbwa na matatizo ya kuumwa kichwa, lakini mara nyingi hukimbilia kupima au kunywa dawa za malaria.”

Anasema, wengine ambao hawapati dalili za wazi hadi wanapofikia hatua ya kuwa kipofu kabisa ndipo huenda kwa wataalamu wa macho na kwamba hufika kwa wataalamu, lakini bila mafanikio ya kupona. Ushauri wake kwa jamii Keskin anaihimiza jamii kuepuka kununua miwani kabla ya kuonana na wataalamu waliosomea ili kuwashauri na kuwapima.

Anasema lengo la kuonana na wataalamu waliobobea katika masuala ya macho ni kujiridhisha mintarafu tatizo pamoja na kupatiwa tiba inayostahili tofauti na kumeza dawa kiholela.

“Mtu mwenye tatizo la macho kabla ya kununua dawa, inabidi aonane na wataalamu wa macho au kliniki za macho zinazotambulika ili afanyiwe vipimo na kubaini tatizo,” anasema.

Blogu ya Mkumbohealth inaandika ikisisitiza kuwa, afya nzuri ya macho inatgemea kwa kiasi kikubwa virutubisho vinavyopatikana katika mlo.

Inasema: “Virutubisho kama Omega 3. Lutein, Zinc, na Vitamin C na E husaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya macho yanayoambatana na umri mkubwa ama uzee kama cataracts (ama mtoto wa jicho), macular degeneration (tatizo ambalo husababishwa na kuchoka kwa retina).”

Mtoto wa jicho ni ugonjwa unaotokea lenzi ya jicho inapokuwa na hali ya uwingu. Tatizo hili linaweza kusababisha uoni mfupi (myopia). Ikiwa haitatibiwa kwa upasuaji, baadhi ya aina za mtoto wa jicho zinaweza kusababisha upofu (maana yake huwezi kuona kitu chochote).

Ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kubadilisha lenzi asili na kuweka nyingine ya plastiki kwa njia ya upasuaji mdogo.

Inaongeza: “Lishe salama yenye wanga na sukari kidogo, na vyakula vya mafuta kama nazi, parachichi, samaki, nyama na mayai kwa wingi itakusaidia kukuepusha na kuugua kisukari ambacho ni chanzo mojawapo cha upofu.”

Machapisho mbalimbali ya kitaalamu pia yanasisitiza kuepuka uvutaji wa sigara kama moja ya njia muhimu za kulinda na kutunza macho. Yanaelezeka kuwa, uvutaji wa sigara husababisha kuchoka haraka kwa retina na kushindwa kufanya kazi, na hivyo kusababisha wingu kwenye mboni ya jicho (mtoto wa jicho).

Imeandikwa mtandaoni:“Punguza matumizi makubwa ya kompyuta, televisheni na simu za mwanga mkali kwani husababisha uchovu wa macho, kuona mawengewenge, macho kuwa makavu, ugumu wa kuoana vitu vya mbali na hata maumivu ya shingo, mabega na mgongo.”

Keskin anasema licha ya kuwepo kwa vituo mbalimbali vya afya, lakini pia ni muhimu kwa mwathirika wa magonjwa ya macho kuzifikia hospitali zinazotambulika ikiwemo International Eye Hospital. Hospitali hii inatoa huduma za kibingwa na ina uwezo wa kiwango cha juu katika utaoji wa huduma.

Anasema hospitali hiyo ina vifaa vya kimataifa vinavyotambua dalili hatarishi za ugonjwa kwa urahisi zaidi na kubaini ni tiba ipi inayohitajika kwa mgonjwa husika.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ni vema watu wenye ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, wakaonana na daktari wa macho na kufanyiwa kipimo maalumu mara moja au mara mbili kwa mwaka kubaini athari za magonjwa kabla hayajaathiri jicho katika kiwango cha juu.

Wataalamu wanasema ili kulinda macho dhidi ya dalili na matumizi yanayohatarisha macho, tumia miwani maalumu ya kuzuia athari za miale ya mwanga unaotokana na vifaa hivyo vya elektroniki na vingine vya namna hiyo na weka kioo cha kompyuta ama televisheni chini ya usawa wa macho ili kupunguza miale ya mwanga kufikia macho moja kwa moja.

“Kama unafanya kazi zinazohitaji matumizi makubwa ya kompyuta, hakikisha kila baada ya dakika 20 unapumzisha macho kwa kuangalia pembeni ama juu kwa sekunde 30 hivi. Kisha, kila baada ya saa mbili pumzika kwa takriban dakika 15 bila kutazama mwanga wa kompyuta yako,” linasema chapisho katika blogu hiyo.

Linaongeza:“Macho yako yakiwa makavu, basi fanya mazoezi ya kufumba na kufumbua kwa muda kisha endelea na kazi zako na tatizo likiendelea, onana na daktari.”

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi