loader
Picha

Viongozi jipangeni kusimamia miradi ya maendeleo

KITENDO cha Waziri na Naibu Mawaziri wa Mkoa wa Pwani kujipanga kusimamia miradi mikubwa ya kimkoa na kitaifa hakina budi kiigwe na viongozi wa ngazi zote kote nchini.

Tunashawishika kusema hayo kwa sababu kuna miradi mingi kwa nchi nzima inayoendelea huku ikiwa katika hatua mbalimbali.

Usimamizi wa miradi hiyo muhimu kwa Watanzania, inalenga katika sekta zote ikiwa ni pamoja na miradi ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, reli, anga na majini.

Iko miradi mikubwa inayohusu nishati, maji, kilimo na mifugo, yote ikihitaji usimamizi uliotukuka kutoka kwa viongozi wa ngazi zote, kuanzia kata, tarafa, wilaya, mikoa hadi taifa.

Halmashauri zote nchini zimekabidhiwa miradi mingi ambayo kwayo ikikamilika, tutaiona Tanzania mpya mbayo Serikali ya Tano chini ya Rais John Magufuli inasimamia na kwa kiasi kikubwa kwa fedha za ndani.

Kwanza ili miradi hiyo ikamilike si tu kwa wakati lakini iwe pia imetekelezwa kwa umakini mkubwa.

Tunashawishika kuwapongeza mawaziri wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega. Hawa wameamua kwa udhati wao kusimamia miradi yote ambayo imetengwa katika mkoa wao huo ili kuiwezesha Serikali ya Tano kutimiza malengo yake.

Tunaamini kwamba uthubutu huo ndio unaostahili kufanywa na viongozi wote kuanzia ngazi zote kwa kuwa miradi hii inagusa maeneo nyeti ambayo ndiyo yamekuwa yakilalamikiwa huko nyuma.

Tunahitaji viongozi wafikie mahali waweke uzalendo mbele kuwezesha fedha za walipa kodi ambazo zimeingizwa katika miradi hii mikubwa ya maendeleo zitumike vyema. Viongozi wajipange kwa nafasi zao kuhakikisha miradi hii inasimamiwa kikamilifu iweze kuisha kwa wakati na kwa uimara.

Viongozi wa ngazi zote waone umuhimu wa kufanya maamuzi magumu pale wanapobaini kuna hujuma katika miradi iliyo kwenye maeneo yao.

Tuache siasa, tuchape kazi. Tanzania ya sasa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kuifikisha itawezekana kwa kila kiongozi kutimiza wajibu wake kama walivyoamua mawaziri wa Mkoa wa Pwani kusimamia miradi yote ya mkoa na kitaifa.

MKUTANO wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi