loader
Picha

CCM ya Magufuli ni ya wanyonge

IKIWA jana Watanzania wametimiza miaka 42 ya kuongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM, nitaanza makala haya kwa nukuu hii:

“Mimi naamini CCM sasa imeanza safari ya kuelekea kwenye kifo chake, imekumbatia jambo ovu; rushwa; ambayo imeua viongozi wazuri wengi, vyama vya siasa na serikali makini duniani.”

Hii ni nukuu ya maneno yanayoaminika kusemwa na kada mkongwe wa CCM, Joseph Butiku katika barua aliyomwandikia aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Benjamin Mkapa, siku chache baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Butiku akazidi kusema huku baadhi ya maneno akiyaandika kwa herufi kubwa kuonesha msisitizo:

“CCM imeanza kushindwa kusema na kutetea HAKI na UKWELI; imeanza kuvumilia na kutetea UBAGUZI. Imeanza kuwa CCM ya viongozi wafanyabiashara wanaoonesha nia ya kutaka kubinafsisha CCM na wasioonesha nia thabiti ya kujali MAADILI ya chama chetu na taifa letu. Siyo CCM ya viongozi wa watu wanyonge tena.”

Mtendaji huyo Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere akazidi kuandika: “Badala ya uongozi wa CCM kuheshimu wanyonge na kutetea haki za wote pamoja na wanyonge, chama kimeanza kujenga tabaka la viongozi wenye mali au wanaowekwa katika nafasi za uongozi na wenye mali au kwa kutumia mali zao wao wenyewe, ili wapate nafasi za kufanya mambo yao.”

“Mali imeanza kuchukua nafasi ya uzalendo na kutumiwa na viongozi wengi wa CCM kama nyenzo ya uongozi bora wa kisiasa. CCM imeanza hata kutoona haya, na viongozi wakuu, chini ya uongozi wako sasa wamenyamaza, wanaona haya kukemea uovu.”

Butiku aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi yetu ikiwemo ukatibu mkuu, ukatibu wa rais, ukuu wa mkoa, ubunge, ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na ukatibu wa CCM wa mkoa alitoa angalizo hilo kutokana na kutopendezwa na namna rushwa ilivyodaiwa kutumika kuwapata baadhi ya viongozi wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005.

Hebu tuulizane mimi na wewe. Leo hii CCM inavyotimiza miaka 42, Butiku anaweza kulalamikia mambo kama hayo tena?

Mwenyekiti wa CCM aliyefuatia, Jakaya Kikwete, alikiri uwepo wa tatizo la ufisadi miongoni mwa wanachama na viongozi wa CCM lililokuwa linasababisha, siyo tu matabaka ndani ya chama hicho kikongwe, bali pia kuifanya CCM isionekane ya wanyonge tena. Ndipo akaja na dhana ya ‘kujivua gamba’.

Pengine, kutokana na namna ufisadi ulivyokuwa umekita mizizi katika jamii yote, haikuwa rahisi sana ‘kuwatumbua’ watuhumiwa wa vitendo vya rushwa na ufisadi kwa ghafla ndani ya CCM na ndiyo maana chama kikawataka wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kujitathmini wenyewe na kuondoka.

Pamoja na uongozi wake kuonekana kuelemewa na mafisadi kiasi cha kushindwa ‘kuyavua magamba’ yote isipokuwa baadhi, Jakaya Kikwete ataendelea kukumbukwa sana kwa jinsi alivyopambana kuhakikisha mgombea urais wa mwaka 2015 kupitia CCM hatokani na makundi ya wenye pesa yaliyokuwa tayari kununua uongozi.

Mgombea aliyepitishwa na chama hicho na ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli, aliwahi kukiri kwamba kama rushwa ingeachiwa ichukue mkondo wake, yeye kamwe asingekuwa rais! Wakati anachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM Jumamosi Julai 23, mwaka 2016, Rais Magufili alisema:

“Katika kipindi cha uongozi wangu nitashirikiana na nyie kuhakikisha tunaliondoa tatizo la rushwa… Kikwete hukuwa rafiki wa rushwa, ungekuwa mla rushwa mimi nisingekuwa rais. Ole wao watakaokula rushwa (huku mimi) nikiwa mwenyekiti (wa CCM).” Alichokuwa anakisema Magufuli hapo ndicho alikisema Butiku kwenye barua yake kwa Mkapa kwamba ‘rushwa imeua viongozi wazuri wengi’.

Hata yeye ingeweza ‘kumuua kisiasa’ kama si Kikwete kusimama imara. Wakati CCM sasa ikiadhimisha miaka 42, baadhi ya ahadi alizozitoa Dk Magufuli baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho zinaendelea kuzitimizwa sambamba na hii ya kupambana na rushwa.

Miongoni mwa hizo ni kuendelea kujenga CCM imara kwa kuwa chama legelege, kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, huzaa serikali legelege. Ukichunguza kwa umakini, chama hicho kimeendelea kujipatia viongozi imara, wazalendo na wachukia rushwa, akiwemo Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Bashiru Ally.

Lingine lililofanyika ni chama hicho kuondoa vyeo vyote visivyo na tija ndani ya chama na kufanya tathmini ya rasilimali zake zote katika kuhakikisha zinatumika kwa tija na siyo kunufaisha wachache. Wakati Butiku anaandika barua yake kwa Mkapa, alisema kwamba CCM haiwezi kubaki salama kama hataifanya rushwa kuwa ajenda yake ya kudumu ili kuikomesha ndani ya chama hicho.

“Kama CCM haitafanya rushwa kuwa ajenda ya kudumu, vyama vingine vitadandia ajenda hiyo na dunia itaendelea kutuyumbisha kuwa ni sehemu ya ajenda ya utawala bora.”

“Tusijidanganye pia kuwa CCM itabaki chama salama kwa ajenda ya utawala bora. Tusijidanganye pia CCM itabaki chama salama kama kitaanza kuwa chama cha ubaguzi,” anaandika Butiku.

Ujio wa Magufuli kama Mwenyekiti wa CCM aliyeanza kupambana na rushwa kwa kinywa kipana hata kabla hajakabidhiwa mikoba ya kukiongoza chama hicho, kunamfanya yeye mwenyewe awe ajenda ya kudumu inayokifanya chama hicho kujitenga na rushwa.

Katika muktadha huo, tunashuhudia vyama vingine vya siasa vikiwa vimefilisiwa hoja ya rushwa na ufisadi iliyochangia sana kuvipa umashuhuri au‘kiki’ kama vijana wa sasa wanavyosema.

Tunashuhudia pia namna nchi yetu inavyozidi kujitokeza kimataifa kama inayojitahidi katika suala zima la uongozi bora. Haya yote, yanatokana na kufanikiwa katika suala la uongozi na utawala kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka 42 ya uhai wake. Ikimbukwe pia kuwa, Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa Kitaifa wa CCM alianza kujulikana kwamba si rafiki wa rushwa tangu akiwa waziri.

Akiwa katika uwaziri wake, Magufuli alikuwa akipambana vilivyo na vitendo vya wala rushwa na ufisadi kwa nguvu zake zote.

Magufuli anakumbukwa, kwa mfano, alivyopambana na mafisadi kwenye uvuvi alipokuwa akiitumikia wizara husika kiasi kwamba alisababisha samaki kuongezeka kwenye maziwa, mito na bahari kutokana na kuwakabili vilivyo wavuvi haramu bila kujali mapesa yao haramu.

Taratibu, Watanzania wamerudisha na wanaendelea kurudisha imani yao zaidi kwa CCM kama chama cha kutetea wanyonge wa nchi hii. Hii ndiyo maana CCM kimeendelea kuwafanya watu wengi sasa kujiunga nacho wakiwemo wabunge na madiwani lukuki kutoka vyama vya upinzani waliokuwa wamepoteza matumaini na chama hicho.

Imani iliyopo sasa ni kwamba wanyonge wa nchi hii kupitia chama hicho sasa watakuwa na kauli ya walau kuchagua viongozi wao wanaowataka katika chama na katika vyombo vya uwakilishi serikalini, bila ushawishi wa matumizi ya fedha.

Nikiwa na hakika kwamba huko aliko Mzee wangu Butiku anafurahia kuona kile alichokitaka kifanyike wakati wa Mkapa kinafanyika sasa, nimalizie kwa nukuu yake hii ninayotamani pia iwe inafanyiwa kazi na viongozi wetu wa kitaifa.

“Taifa letu bado ni changa sana, Watanzania bado ni maskini mno, hawajaweza kujenga misingi imara ya utawala bora na kujenga vyombo imara vya utawala wao (Institutional Capacity): Wanaitegemea sana CCM, wanawategemea sana viongozi wakuu wa CCM. Jitahidini kwa pamoja, msiwaangushe Watanzania wenzenu.”

Mwisho niseme, Hongera CCM kwa kutimiza vema miaka 42, bila kuyumba wala kuyumbishwa; hongera viongozi wakuu na wanachama wa CCM na Hongera Watanzania kwa miaka 42 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotokana na muungano wa Tanu (Tanganyika African National Union) na ASP (African Shiraz Party) Februari 5, 1977.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Hamis Kibari

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi