loader
Picha

Marekani yahadharisha raia wake kuhusu ugaidi

UBALOZI wa Marekani nchini Kenya umehadharisha raia wake juu ya uwezekano wa kuwapo shambulio la kigaidi linalosadikiwa kulenga raia wa nchi za magharibi.

Shirika la habari la Aljazeera limenukuu taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa jana ikisema taarifa za kuaminika zinaonesha maeneo yaliyo katika hatari ya kushambuliwa ni Nairobi, Naivasha, Nanyuki na maeneo ya pwani yenye watalii wengi.

Tahadhari hiyo imekuja wiki chache baada ya shambulio lililofanywa na kikundi cha al-Shabab katika hoteli ya DusitD2 Nairobi na kuua watu wapatao 21 wakiwamo raia wa nje. “Ubalozi wa Marekani unakumbusha umma kuwa waangalifu hususani katika maeneo ya watu wengi kama vile kwenye maduka makubwa, hoteli na maeneo ya ibada,”ilisema taarifa hiyo ya ubalozi.

Wakati huohuo , Serikali ya Uingereza imetaka raia wake walioko Kenya kuepuka maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Somalia pamoja na maeneo ya mwambao. Katika mwongozo wake kwa wasafiri, ofisi ya mambo ya nje na jumuiya ya madola ya Uingereza imesema lipo tishio la ugaidi katika maeneo mbalimbali ya Kenya ikiwamo Nairobi , maeneo ya pwani na yale ya mapumziko karibu na Mombasa na Malindi.

Kikundi cha kigaidi, wakiwa na silaha wamekuwa wakielekeza mashambulizi ya mara kwa mara kwa raia wa nje au maofisa wa serikali katika Somalia na Kenya. Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Marekani iliyowekwa kwenye tovuti yake, raia wake wameelekezwa kuripoti kwenye mamlaka shughuli yoyote watakayoitilia shaka. Wametakiwa pia kuwa waangalifu kwenye maeneo ya utalii; kufuatilia vyombo vya habari vya ndani na wakati wote kuwa na nyaraka za safari.

Nchi hiyo imeshauri raia wake wanaosafiri kwenda Nairobi au wanaoishi nchini hapa kujiandikisha kwenye idara yake ya usalama wa taifa (STEP) iwe rahisi kupata taarifa mbalimbali za kiusalama na pia kuwasiliana nao inapotokea dharura.

SERIKALI nchini Canada imeidhinisha kufanyika kwa majaribio ya kwanza ya ...

foto
Mwandishi: NAIROBI, Kenya

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi