loader
Picha

Unavyoweza kutumia jua kupunguza gharama za umeme

WATU mbalimbali wamekuwa wakiingia gharama kubwa kununua mafuta ya petroli au dizeli ili kuzalishia umeme kwa kutumia jenereta au kulipa bili kubwa ya umeme wa gridi ya taifa, bila sababu.

Mkurugenzi wa Ensol Tanzania Limited ambayo ni wakandarasi na wauzaji wa vifaa vitumiavyo nishati ya mionzi ya jua iliyopo Ubungo Dar es Salaam, Mhandisi Hamis Mikate, anasema hii ni kwa sababu hawana taarifa sahihi za kutosha kuhusu teknolojia ya umeme utokanao na mionzi ya jua.

Anasema: “Hata wachache wenye taarifa hizo, wanazo taarifa ambazo ama ni potofu, au hazijitoshelezi na hivyo, hasara kwa watu, taasisi na hata taifa.” Mikate anasema hayo wakati akizungumzia umuhimu wa kutumia nishati mbadala kupambana na uharibifu wa mazingira nchini sambamba na kupunguza gharama za watumiaji umeme ama wa nyumbani, au katika taasisi zikiwamo ofisi.

Kwa msingi huo, anasema ndiyo maana wadau wa vita dhidi ya uharibifu wa mazingira wanajitahidi kusambaza njia na teknolojia mbalimbali zinazoweza kuwaepushia watu dhidi ya tatizo hili ama iwe kwa watumiaji wenye mahitaji makubwa, au ya kawaida ya nishati ya umeme.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mfumo wa umeme utumiao mionzi ya jua una faida zaidi ya mfumo wa kawaida kutokana na teknolojia yake inayosaidia watumiaji kuzalisha umeme mwingi kwa gharama nafuu kwa kuwa mahitaji ya betri yanapungua.

Anasema nishati itokanayo na mionzi ya jua, ukiwamo mtambo wa sola unaochemsha maji kwa kutumia joto la jua ni rafiki wa mazingira. Anatoa mfano wa mtambo wa kuchemshia maji wa sola akisema: “Huu ni mtambo wenye faida sana maana, kwanza, ni rafiki mkubwa wa mazingira kwa sababu hauna uchafuzi wowote wa mazingira maana mtu hahitaji kununua gesi, kuni wala mkaa ili autumie kuchemshia maji na wala, hautumii umeme hivyo, hauna gharama za malipo ya umeme...”

Anaongeza, “Faida nyingine ya mtambo huu ni kwamba, unaweza kutumika mahali popote pale na katika jengo lolote lile kama vile nyumba ya kulala wageni, nyumba ya kuishi, hotelini, katika hospitali, vituo vya afya au zahanati na mahali pengine panapohitaji maji-moto kama vile shuleni, mradi tu kuwe na jua.”

Katika mazungumzo tofauti, Mkurugenzi wa Ufundi wa Ensol Tanzania Limited, Prosper Magali anasema, teknolojia hii inasaidia pia katika pampu za maji za sola ambazo ni maalumu kwa kuvuta maji kwa umbali wa kina cha hadi mita 400 na kuyapandisha katika tangi ili yasambazwe kwa matumizi mbalimbali kama maji kwa ajili ya kunywa, umwagiliaji, mifugo n.k kutoka katika vyanzo mbalimbali kama visima virefu, mabwawa na mito.

Mhandisi Magali anasema zina nafasi na uwezo mkubwa kukabiliana na tatizo la maji linalowaathiri zaidi akina mama na watoto hususan wa kike katika taasisi na meneo mbalimbali zikiwa ni pamoja na shuleni.

“Wanakijiji wanaweza kutumia muda wao mwingi kwa shughuli nyingine za uzalishaji mali na wanafunzi kupata muda wa kutosha na wa ziada kufuatilia masomo yao.”

Kwa nyakati tofauti wataalamu hao wa umeme utokanao na mionzi ya jua wanasema teknolojia hiyo, pia inamwezesha mmiliki wa mfumo wa umeme wa jua, kujua mwenendo wa umeme (mfumo) hata kama yuko mbali kwa kutumia simu ya mkononi au mtandao wa intaneti.

“Kwa kutumia teknolojia hii, ukifunga nyumbani kwako umeme wa sola au ofisini kisha ukasafiri kwenda hata nje ya mkoa; popote, unaweza kutumia intaneti au simu yako ya mkononi, ukapata taarifa kama umeme hata kama ulikatika wakati haupo, au ikakujulisha kama kuna hitilafu katika mfumo na sababu ya hitilafu hiyo,” anasema Mikate.

Akijikita katika mfumo mpya unaopunguza gharama za mafuta ya kuzalishia umeme katika jenereta, Mikate anasema: “Taasisi, mashirika, kampuni na ofisi mbalimbali zinaingia hasara kwa kutumia gharama kubwa kununua mafuta kwa ajili ya jenereta zao kuzalishia umeme hata pale ambapo mahitaji ya umeme yanapokuwa madogo sana.”

“Hii ndiyo sababu tumeleta teknolojia hii ambayo pia licha ya kupunguza gharama za mafuta pia zinapunguza gharama za awali za ufungaji wa umeme wa sola na kwa wale wenye umeme wa kawaida zitawapunguzia bili.”

“Kimsingi, teknolojia hii mpya inawafaa sana watu wa mijini na vijijini wanaotumia umeme mwingi na wanaotumia pesa nyingi kununulia mafuta ili kuendeshea jenereta mfano, nyumba za kuishi, nyumba za ibada, hoteli, ofisi na hospitali.”

Anatoa mfano: “Kwa teknolojia hii mpya ya umeme wa mionzi ya jua, hakuna haja ya kuwa na betri nyingi kwa sababu umeme utakaozalishwa mchana utaweza kutumika moja kwa moja na kiasi kitahifadhiwa kwenye betri kwa ajili ya matumizi ya usiku.”

“Tofauti ni kwamba, umeme mkondo mnyoofu unaozalishwa na solar panel utabadilishwa moja kwa moja kuwa mkondo geu (AC) kupitia ‘inverter’ maalum bila kupitia kwenye kidhibiti chaji kama ilivyo kwenye mifumo tuliyoizoea.

Gharama za awali za mfumo wa solar zinapungua kwa sababu haihitaji betri nyingi.”

Anadokeza: “Kimsingi, teknolojia hii inafaa sana kwa mifumo mikubwa kuanzia watts 1000 (1kWp) na kuendelea au kwa lugha rahisi inafaa zaidi kwa mifumo inayoanzia wastani wa solar panel 10 za watt 100 kila moja; hii haina maana haifai kwa mtumiaji wa watts 500 ila uwiano wa gharama unaweza usiwe mzuri”.

Katika moja ya mazungumzo na Mkurugenzi wa kampuni ya Rex Energy, Francis Kibhisa, anasema umeme utokanao na mionzi ya jua unafaa kwa taasisi au watumiaji walio mbali na umeme wa kawaida toka gridi ya taifa na una manufaa makubwa kwa kuwa unabana matumizi.

“Taasisi kama shule, majengo yaliyoko mbugani kama ofisi, hotel n.k; hoteli kubwa zikiwamo hospitali, hazipaswi kuendelea kubeba gharama kubwa na kukatika hovyo kwa umeme eti mafuta yameisha kwenye jenereta maana mfumo unaotumia kifaa hiki unapunguza bili na gharama za mafuta maana mfumo huu unaruhusu umeme kuzalishwa kwa kupokezana.”

“Unaweza kuzalisha kwa sola kwanza, mahitaji yakizidi ukatumia umeme wa gridi na usiku ukawasha jenereta kwa muda maalumu kulingana na mahitaji husika; hivyo gharama za bili au mafuta ya kuendesha jenereta huweza kupungua wakati huo huo unakuwa na umeme wa uhakika muda wote,” anasema.

Faida nyingine anasema, ni pamoja na kuepusha moshi na kelele za muda mrefu kwani kuna baadhi ya maeneo wanalazimika kutumia jenereta siku nzima, yaani saa 24 jenereta zinapokezana; sasa badala yake, jenereta zitapokezana na sola. Magali anasema: “Uzalishaji huu wa umeme ni rafiki mkubwa wa mazingira jambo ambalo ni manufaa kwa ustawi na usalama wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”

Anaongeza: “Kama ulivyo umeme wa sola wa kawaida, hauna urasimu wala hauhitaji rushwa kuupata; hauhitaji nguzo; hauhitaji maji, upepo, mafuta wala nishati nyingine ili kuuzalisha isipokuwa tu, mionzi ya jua ambayo ipo mahali popote na haiuzwi.”

Anaelezea zaidi mfumo huu mpya akisema, “unajua katika system (mfumo) wa kawaida, bei ya kuanzia hutegemea pia idadi ya betri lakini hapa, ni tofauti maana mchana betri hazitumiki.

Huyu ni mkombozi.” Unavyofanya kazi Wataalamu hao wa teknolojia ya umeme wa jua wanasema wakati wa mchana katika mfumo wa umeme wa mionzi ya jua wenye PV inveta, paneli za sola huzalisha umeme katika mkondo geu na kuupeleka moja kwa moja katika vifaa vinavyotumia huku kiasi kingine kikihifadhiwa katika betri.

“Wakati wa usiku ambapo sola na inveta hazifanyi kazi, betri hupeleka umeme kwa mtumiaji kupitia inveta ya kawaida,” anasema Magali.

Betri inapoisha?

Betri inapoisha na ikiwa jua hamna kabisa (usiku), umeme wa gridi au jenereta huwaka yenyewe na kuanza kuchaji betri na wakati huo huo, ikipeleka umeme mwingine katika matumizi. “Mwanga wa jua ukiwepo na mahitaji ya umeme hayazidi uwezo wa sola, basi jenereta au umeme wa gridi ya taifa huzimwa ‘automatically’; kwani sola kuanza kuchaji betri na kupeleka kwenye matumizi moja kwa moja.

Ndiyo maana tunasema kuwa, mfumo huu hupunguza mahitaji ya betri nyingi…” anasema Mikate.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi