loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Umuhimu wa utii kwa Serikali

Kwa mtumishi wa umma kuitii serikali maana yake ni kutekeleza sera na maelekezo yanayotolewa na viongozi mbalimbali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa mfano, serikali inapoazimia kuinua kiwango cha elimu, azimio hilo linaendana na mikakati mbalimbali ambayo inatumika na kila mtumishi katika kuandaa malengo yake kulingana na taaluma yake ili azma ya serikali iweze kutimia. Ujumbe wa leo wa maadili ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu imo katika mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992.

Kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa kulitoa fursa kwa wananchi wenye uwezo, kuanzisha vyama vya siasa. Katika mustakabali huu, lengo kuu la kila chama cha siasa limekuwa ni kukamata dola kupitia sanduku la kura. Kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, uchaguzi mkuu wa rais na wabunge umefanyika mara tano ukihusisha vyama mbalimbali vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa mfano, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ulimhusisha Benjamin William Mkapa aliyepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Augustine Lyatonga Mrema (NCCR), Ibrahim Haruna Lipumba (CUF) na Moses Cheyo (UDP).

Chaguzi zilizofuatia zimeshuhudia kuongezeka kwa idadi ya vyama vya siasa vikiomba ridhaa ya wananchi kukamata dola. Jambo muhimu la kuzingatia hapa ni kwamba, kila chama kimekuwa na wanachama pamoja na mashabiki wake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma. Jambo muhimu la kuzingatia hapa ni kwamba kila chama kimekuwa na ilani yake ya uchaguzi ikieleza chama hicho kinakusudia kufanya mambo gani kwa ajili ya wananchi endapo kinashinda uchaguzi.

Kama ilivyo ada, chama kinachoshinda uchaguzi ndicho kinachounda serikali na kwa minajili hiyo, kinakuwa kimepata fursa ya kuitekeleza ilani yake. Kwa msingi huu, ilani ya chama tawala inakuwa ndiyo chimbuko kubwa la sera na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi zake. Katika mazingira yote hayo, ikumbukwe kuwa mwandaaji na mtekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali inayolenga kutekeleza ilani ya chama tawala ni mtumishi wa umma.

Ikumbukwe pia kuwa, watumishi wa umma wana haki ya kushiriki kwenye siasa ya nchi na baadhi yao wamekuwa wakivutiwa na ilani za vyama vingine vya siasa. Kimsingi, katiba ya nchi imekuwa inatoa fursa kwa wananchi wote, ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma (isipokuwa wale wanaotakiwa kutoshiriki masuala ya siasa kwa mujibu wa sheria ya nchi) kushiriki katika mambo ya siasa, ikiwa ni pamoja na kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Lakini pia, katiba hiyo hiyo ya nchi inatoa fursa kwa chama kilichoshinda uchaguzi kuunda serikali na kutekeleza ilani yake.

Kwa mantiki hiyo, watumishi wote wa umma wana wajibu mkubwa wa kikatiba wa kuitii serikali iliyopo madarakani ili iweze kutumia fursa yake ya kikatiba ya kutekeleza ilani yake. Wananchi wanaweza kufaidika na mambo mengi sana endapo watumishi wa umma watajenga uwezo wa kuitii serikali iliyopo madarakani na kutekeleza shughuli mbalimbali kwa waledi ili waweze kufikia azma iliyowekwa na serikali husika.

Mfano mzuri katika nchi yetu ni azma ya serikali ya CCM kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami. Watumishi wa umma katika sekta ya ujenzi wa barabara wamekuwa wakiitikia kwa nguvu mwito wa serikali katika kujenga barabara na hivi sasa usafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine umeimarika sana na kurahisisha safari za abiria na usafirishaji wa mahitaji mbalimbali kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Leo hii sehemu kama Singida iliyokuwa ikionekana kame na yenye upungufu mkubwa wa nafaka, inafurahia uwepo wa mazao mbalimbali ya kilimo kutoka mikoa mingine kama Kagera, Mwanza na Kilimanjaro. Vilevile, mikoa yenye nafaka imekuwa ikifaidika sana na kuku bora wa kienyeji na mazao mengine kama alizeti kutoka Singida. Kwa jumla utii wa watumishi wa umma kwa serikali yao umekuwa muhimu siyo tu katika mazingira ya vyama vingi vya siasa, bali pia katika mazingira yenye makundi mbalimbali yenye yenye lengo la kusimamia maslahi yake na kushinikiza mambo mbalimbali. Kubwa zaidi pia, utii wa watumishi wa umma umekuwa muhimu hata dhidi ya maslahi binafsi ya watumishi wenyewe ili kufikia maslahi mapana ya umma mzima wa Tanzania.

IJUMAA iliyopita, tulianza kuangalia manufaa ambayo nchi inaweza kuyapata kupitia ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi