loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hizi ndizo haki za mtumiaji huduma za mawasiliano

Hizi ndizo haki za mtumiaji huduma za mawasiliano

UKUAJI wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika miaka ya hivi karibuni, umekua wa kasi kubwa hali inayodhihirishwa na idadi kubwa ya watumiaji wa huduma mbalimbali za teknolojia hiyo kote duniani.

Kwa mfano, watumiaji wa simu za mkononi duniani kwa mujibu wa mtandao wa statista. com, kwa mwaka huu wa 2019, wanatarajiwa kufika bilioni 4.6 sawa na asilimia 67 ya watu wote duniani kutoka asilimia 62.9 kwa takwimu za mwaka 2016. Kwa Tanzania, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), inasema takwimu za hivi karibuni za usajili wa watumiaji wa simu hadi kufikia Juni 2018, Tanzania ilikuwa na watumiaji wa huduma za simu takribani milioni 42.

Kutokana na kasi ya ukuaji wa matumizi ya Tehama, bila shaka kwamba idadi hiyo hadi leo makala haya yanapoandikwa itakuwa imeongezeka. Ieleweke kwamba watumiaji ni watu wanaonunua bidhaa au huduma kwa matumizi binafsi au kwa ajili ya matumizi ya watu wengine kwa niaba ya mnunuzi. Kwa mfano, mwanamama anayenunua simu ya mkononi kwa matumizi yake, huyu ni mtumiaji wa simu ya mkononi, lakini anaponunua runinga na familia nzima ikanufaika na habari kupitia kifaa hicho cha kielektroniki basi mama huyo na familia wote ni watumiaji wa huduma za mawasiliano.

Jambo la kuzingatia ni kwamba sio lazima mtumiaji awe ni mnunuzi wa kifaa cha mawasiliano husika kwa maana kwamba watoto wanaponufaika na redio au seti ya runinga basi wao pia ni watumiaji wa huduma ya utangazaji kupitia bidhaa au kifaa hicho licha ya kwamba sio wanunuzi wake. Kwenye sekta ya mawasiliano, mtumiaji wa huduma za mawasiliano kama vile simu za mkononi ambazo statista. com wanasema idadi itakaribia bilioni 5 mwaka huu ni mtu yeyote anayetumia huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), huduma za utangazaji na huduma za posta, vifurushi na vipeto.

Kimsingi, unaposema bidhaa za mawasiliano unamaanisha simu, kompyuta, redio, runinga (televisheni) pamoja na visimbuzi kwa ajili ya kunasia matangazo ya kidigiti ya runinga. Huduma za mawasiliano huhusisha utangazaji kupitia redio na televisheni, huduma ya posta, huduma ya kusafirisha vifurushi na vipeto, huduma za mawasiliano kwa njia ya simu kwa maana ya data, sauti, huduma za kifedha na kadhalika. Hata hivyo, maendeleo haya ya kiteknolojia, yana changamoto kadhaa, ambazo kwa namna moja au nyingine ni kikwazo kwa ustawi wa teknolojia ya Tehama duniani.

Changamoto hizo zinaweza kutokana na watumiaji kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki na wajibu wao, hali kadhalika watoa huduma au wauza bidhaa za mawasiliano kutojua au kutozingatia wajibu wao kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano. Katika kukabiliana na changamoto hizo; Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) linachukua jukumu la kuelimisha watumiaji juu ya haki na wajibu wao sambamba na kuwakumbusha watoa huduma na wauza bidhaa kutimiza wajibu wao kwa watumiaji.

Haki ya kwanza na ya msingi ya mtumiaji ni kupata huduma na bidhaa za mawasiliano kwa gharama nafuu na kwa kuzingatia hali ya kipato cha wananchi wakiwamo wa maeneo ya pembezoni. Mtumiaji ana haki ya kupata huduma za mawasiliano ambazo ni pamoja na; utangazaji, mawasiliano ya simu, Intaneti au data na usafirishaji wa mizigo pamoja na vipeto.

Pamoja na kuwepo kwa haki hii, watumiaji waishio kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini hawapati huduma hizi kama wale waishio mijini. Changamoto hii inatokana na watoa huduma kupendelea zaidi maeneo ya mijini yenye watumiaji wengi na miundombinu yenye uhakika hivyo katika kukabiliana na changamoto hii, serikali ya Tanzania ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Lengo la mfuko ni kusaidia kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote hasa waishio vijijini na maeneo mengine ambayo hayajafikiwa na huduma za mawasiliano.

Haki ya pili ya mtumiaji wa huduma za mawasiliano ni upatikanaji wa bidhaa au huduma za mawasiliano zenye ubora wa hli ya juu. “Ni haki ya mtumiaji kupata huduma na bidhaa za mawasiliano zenye ubora unaokubalika kimataifa na inayolingana na gharama,” anaeleza Hilary Tesha, Afisa Elimu na Uhamasishaji wa TCRA-CCC. Pia anasema watoa huduma na wauzaji wa bidhaa za mawasiliano wanapaswa kuhakikisha huduma na bidhaa za mawasiliano zinakuwa na ubora wa viwango vya kimataifa ili kumwepusha mtumiaji kupata hasara au madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa zilizo chini ya viwango.

Madhara haya yanaweza kuwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi kwa sababu bidhaa isiyokuwa na ubora inaharibika haraka na kumwongezea gharama mtumiaji kununua bidhaa nyingine mara kwa mara. Aidha, bidhaa au huduma za mawasiliano zisizo na ubora zina athari za kimwili, kisaikolojia na kiafya pia.

Yote haya yanaweza kusababisha mtumiaji kuingia gharama za ziada katika kutatua madhara yanayotokea pindi anapotumia bidhaa zisizo na viwango vinavyokubalika kimataifa. Hivyo basi, mtumiaji wa huduma pia anapaswa kununua bidhaa kwa wauzaji wenye leseni zinazotambulika na Mamlaka husika ili kuepuka kununua bidhaa zisizo na viwango na kujisababishia matatizo kadha wa kadha.

“Bidhaa nyingi za huduma za mawasiliano ni za kielektroniki, hivyo mtumiaji anashauriwa kuwa makini anaponunua bidhaa hizo. Mtumiaji asinunue bidhaa za mawasiliano zinazouzwa mitaani kwani zinakuwa juani muda mrefu hivyo kupeleka ubora wake kuwa chini ya kiwango na kuweza kusababisha hasara na madhara kwa mtumiaji” anaongeza kusema Bw. Tesha

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/589deea4ce5991b834afa203dc7323f0.jpg

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Mary Msuya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi