loader
Picha

Maendeleo ya teknolojia na wizi wa haki za wabunifu

WAKATI Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ikizidi kuimarika duniani na kuchukua nafasi ya njia kongwe za mawasiliano, tasnia ya ubunifu nayo inajikuta kwenye changamoto ya kuakisi mabadiliko hayo ya wakati.

Tasnia ya ubunifu ni hazina muhimu sana katika taifa lolote linalohifadhi kazi ya uumbaji; ambapo wabunifu (wasanii) wanayo dhamana ya kueneza ujumbe na elimu kwa jamii.

Tasnia hii ni mjumuiko wa hakimiliki bunifu ambazo zinapaswa kulindwa ili jamii iendelee kunufaika na kazi hizi za ubunifu, ambazo sasa zimeenea duniani kote. Kwa kuwa kiini cha sanaa ni “ubunifu” nina kila sababu ya kuamini kuwa kila binadamu ni msanii.

Tofauti huwa iko katika aina za sanaa anazohusika nazo mtu mmoja na mwingine kwani hakuna binadamu anayeweza kujihusisha na sanaa za aina zote. Japo ubunifu mwingine huegemea katika bayolojia na teknolojia, yaani sayansi, lakini ili ukamilike lazima uhusishe sanaa.

Sanaa ni dhana pana inayohusisha mambo mengi. Zaidi ya asilimia 60 ya maisha ya kila binadamu huhusishwa na sanaa kwani hata ubunifu anaoufanya mwanandoa katika ulaji wa ‘chakula cha usiku’ ni sehemu ya sanaa na hata ubunifu anaoufanya mpishi katika chakula anachopika ni sanaa pia.

Katika muktadha rahisi tunaiweka sanaa katika mambo kadhaa yaliyozoeleka kuitwa sanaa ambayo ni pamoja na michezo, utunzi, uandishi, kuimba, kuigiza, ushonaji, uchongaji, uchoraji, ufinyanzi, ususi, kupaka rangi na mengine mengi.

Lengo kuu la sanaa ni kuelimisha, kuburudisha, kuonya na malengo mengine ni pamoja na kutoa ajira, kuhamasisha na kuendeleza tamaduni. Sanaa huboreshwa na ubunifu pamoja na viungo vya sanaa ili iwe sanaa bora.

Viungo vikuu vya sanaa ni taaluma na kipaji, kwa maana kwamba sanaa huanzia kwenye kipaji, kisha ni muhimu kupata mafunzo ya fani husika. Sifa kuu maalumu ya sanaa ni kwamba ina taathira zake kwa mbunifu na mtazamaji au msikilizaji, hata kama katika mambo mengi mbunifu hatalizingatia hilo, na ijapokuwa katika aghalabu ya wakati, mtazamaji au msikilizaji hatalihisi hilo.

Kwa mfano, athari za tungo za kishairi, filamu, michoro na aina nyingine za ubunifu, sauti ya kuvutia na muziki mzuri – ambapo yote hayo ni katika ubunifu – huziathiri nyoyo za wanaofuatilia au kusikiliza bila wenyewe kujua.

Sanaa na ubunifu si kama utajiri ambao unapatikana mara moja kwa kutoka kijasho cha uso na girisi mikononi. Madhali mtu hana kipaji cha sanaa au ubunifu, hata akijitahidi vipi bado ataendelea kubakia katika asili yake ile ile ya kimaumbile. Kila msanii peke yake ni kama dunia nzima na sifa hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake.

Na kama mtu angelipata fursa ya kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani za dunia na maajabu yake. Ndani ya dunia iliyojaa furaha na majonzi, matumaini na wasiwasi ndani yake, ni sanaa (ubunifu) pekee yenye uwezo wa kutibu majeraha na hata kuifanya jamii iwe na furaha.

Si hivyo tu, kwa sasa tasnia ya ubunifu ina nguvu sana duniani, hasa filamu na muziki, na imeenea duniani kote na kusaidia katika ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, japo tasnia hii inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na kuingia katika zama za dijitali (teknolojia) lakini pia imeanza kukumbana na changamoto kubwa na mkwamo.

Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya teknolojia yameiletea sekta hii fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina ya uenezi wa sanaa hizi zimekuwa nyingi, kwa mfano televisheni za kwenye mitandao ya intaneti (online tv); simu za mkononi n.k., zimeingia kwenye soko la televisheni na imekuwa shinikizo kubwa kwa sekta ya ubunifu.

Lakini hiyo ingeweza kuwa habari njema kama teknolojia hii isingekuwa inatumika vibaya kurahisisha ukwapuaji wa kazi hizo adhimu. Ukuaji wa teknolojia umefanya maharamia wa kazi za ubunifu kukwapua kwa urahisi kazi za sana na hivyo kuzidi kuwafukarisha wabunifu.

Utakuta watu wanapakua filamu na miziki kwenye mitandao, kurudufu na hata kutembea nazo kwenye flashi diski, huku wabunifu wakibaki fukara! Kwa kweli hii si haki, hasa ikizingatiwa kuwa Mungu ametoa neema ya kipawa kwa mbunifu ili aweze kuishi kwa kutumia kipawa chake.

Ukitazama hali ya wabunifu wenyewe katika upande wa maisha yao kwa kweli si nzuri sana, na mara nyingi hata huwa si nzuri kabisa. Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya ubunifu huwa mara nyingi wanashindwa hata kurudisha fedha walizowekeza.

Ni vyema tukatambua hali zao kuwa wanahitaji sapoti ili waendelee kueneza ujumbe na elimu kwa jamii, utakapotizama filamu au kusikiliza muziki, wakati mwingine fikiria wabunifu wote walioandaa filamu hiyo na kumbuka kuna hakimiliki inayowawezesha kupata kipato chao. Na pili fikiria changamoto za teknolojia, kwa kuwa huu ni wajibu wa kila mtu na wala siyo wa watunga sera pekee.

Ni vipi tunaweza kutumia fursa hii ya kipekee ya intaneti ya kueneza utamaduni na wakati huo huo kuhakikisha wabunifu wanaendelea kubuni na wanapata kipato chao kwa kuandaa filamu na video zinazoboresha maisha yetu?

Kwa kweli inabidi kuwasaidia wabunifu na kama hawakusaidiwa wanaweza kuamua kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia fedha za kuweza kuendelezea kazi zao.

Ndiyo maana mara nyingi tumeshuhudia wakitumika katika biashara haramu kama ya dawa za kulevya. Wasiwasi wangu tu wasije wakatokea watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwatumia kuleta machafuko, kueneza fikra za maingiliano haramu ya kijinsia na mambo kama hayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 2006, nchini Tanzania kulikuwa na wabunifu milioni 6, ingawa kwa vyovyote watakuwa wameongezeka sana kwani imeshapita zaidi ya miaka kumi na mbili na hata wakati huo huo teknolojia imekua.

Ubunifu ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki za ubunifu ulikuwa zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini.

Pia mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na Hakimiliki za ubunifu ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii.

Pia wasanii ndiyo wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili. Pia kwa mujibu wa utafiti wa WIPO wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa asilimia 4.275.

Hivyo, ni vema tukahakikisha teknolojia haitumiki kukwapua haki za wabunifu, kwa mustakabali wa taifa na jamii yetu.

0685 666964 au bihiluka@ yahoo.com

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi