loader
Picha

Neema kodi ya majengo, madini

BUNGE limepitisha muswada wa sheria ambao pamoja na mambo mengine unaondoa kodi ya zuio la asilimia tano inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini kwa wachimbaji wadogo na kurekebisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kutoa msamaha kwenye madini ya metali na vito yatakayouzwa katika masoko ya ndani ya nchi.

Pia muswada huo umelenga kuanzisha vituo ya ununuzi wa madini katika maeneo ambayo masoko ya madini hayakuwepo, na kuondoa changamoto za wakulima wa zabibu na viwanda vinavyotumia zabibu katika uzalishaji na kuweka vitango vya mfuto vya kodi za majengo.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 wa Mwaka 2019, umekuja siku 17 tangu Rais John Magufuli azungumze na wadau mbalimbali wa madini na kukubaliana kuondoa changamoto mbalimbali kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini zilizowasilishwa kwake.

Muswada huo ulisomwa kwa mara ya pili na ya tatu bungeni chini ya hati ya dharura.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amesema marekebisho hayo pia yanalenga kuondoa changamoto za wakulima wa zabibu na viwanda vilivyotumia zabibu katika uzalishaji na kuweka vitango vya mfuto vya kodi za majengo.

Alizitaja sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Madini, ya Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Mapato, Mamlaka ya Serikali za Mitaa ya utozaji kodi ya majengo, na ya VAT.

Profesa Kirangi alisema lengo la marekebisho ya sheria ya madini ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi ya zuio kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote kwa wachimbaji wadogo, lengo ni kuwahamasisha wachimbaji wadogo kuuza madini yao katika masoko ya madini yaliyoanzishwa na hivyo kuzuia utoroshaji wa madini nje ya nchi.

Marekebisho hayo pia yanakusudia kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo ambako masoko ya madini hayakuwepo, na kuweka utaratibu wa uingizaji madini nchini.

Lakini pia kuweka mfumo thabiti utakaowezesha wachimbaji wadogo wa madini kununua na kuuza madini katika vituo vya ununuzi na masoko ya madini.

Kuhakikisha kodi zinazohusu leseni za madini zinalipwa kabla ya leseni kuhamishwa kwenda kwa umiliki mwingine na kuhakikisha mapato yanayotokana na biashara ya madini yanakusanywa ipasavyo.

Kuhusu marekebisho ya sheria ya bidhaa, yanalenga kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye pombe kali inayotengenezwa nchini kwa kutumia zabibu zinazozalishwa nchini kutoka Sh 3,315 kwa lita hadi Sh 450 kwa lita.

“Marekebisho hayo yanalenga kuhamasisha viwanda vinavyozalisha vinywaji vikali hapa nchini kutumia mchuzi wa zabibu unaozalishwa na zabibu zilizolimwa ndani ya nchi ili kuhamasisha wawekezaji wengi kuwekeza katika uzalishaji wa vinywaji vinavyotumia mchuzi wa zabibu hiyo na hivyo kuongeza ajira, kuchochea kilimo cha zabibu na kuimarisha uchumi wakulima wa zabibu,” alisema Profesa Kilangi.

Lakini pia serikali inalenga kuondoa tatizo la wakulima wa zabibu nchini kukosa soko la kuuza zabibu kutokana na wazalishaji wa vinywaji vikali vinavyotumia zao hilo kutonunua kwa wingi kutokana na ushuru mkubwa wa bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa kwa zao hilo.

Kuweka viwango mfuto vya kodi za majengo badala ya utaratibu wa hivi sasa ambapo kodi ya majengo kwa majengo yaliyofanyiwa uthamini inatofautiana kutokana na thamani ya kila jengo.

“Lengo la serikali ni kuondoa tatizo la ukwepaji kodi ya majengo na kuhamasisha wananchi kulipa kodi hiyo kwa hiari,” alisema Profesa Kirangi.

Katika marekebisho ya sheria ya serikali za mitaa ya utozaji wa kodi ya majengo, yanaweka viwango mfuto vya kodi ya majengo Sh 10,000 kwa nyumba ya kawaida, Sh 20,000 kwa nyumba ya ghorofa kwa maeneo ya makao makuu ya halmashauri za wilaya na mamlaka za miji midogo.

“Shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida na shilingi 50,000 kwa kila sakafu ya nyumba ya ghorofa iliyopo katika maeneo ya majiji, manispaa na halmashauri za miji,” alieleza.

Kutoza kodi ya majengo kwa kila kiwanja badala ya kila jengo lililopo ndani ya kiwanja husika kwa maeneo ya halmashauri za wilaya, mamlaka za mapato kuendelea kukusanya kodi ya majengo katika majiji, manispaa na halmashauri za miji na za wilaya kwa kushirikiana na serikali za mitaa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, George Simbachawene alisema inakubaliana na serikali kutoza adhabu kwa makosa yanayotokana na kufanya biashara ya madini kinyume cha sheria.

Adhabu hizo ni kutoza Sh milioni tano na isiyozidi Sh milioni 10 pamoja na kifungo kati ya mwaka mmoja hadi mitano na Sh milioni 20 na isiyozidi Sh milioni 50 kwa kampuni, hiyo alisema itasaidia wachimbaji wadogo na wafanyabiashara kufuata taratibu na sheria za biashara ya madini.

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) ni moja ya sekta zilizonufaika ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi