loader
Picha

Tutoe ushirikiano ujenzi barabara mwendokasi

UJENZI wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka (BRT) maarufu kama mwendokasi unaohusisha barabara kadhaa ikiwemo ya Kilwa kwenda Mbagala kutoka Gerezani, Dar es Salaam utaanza Machi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DART, Ronald Rwakatare anasema baada ya wakandarasi wa majengo na barabara kupatikana, hivi karibuni watakabidhiwa eneo la mradi waanze ujenzi huo mapema mwezi ujao.

Akasema mkandarasi wa miundombinu ya barabara ni Kampuni ya China ya Sino Hydro Cooperation na mkandarasi mshauri ni kampuni ya Botek inayoshirikiana na APEX na inayojenga majengo ni China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) ya China pia na mhandisi mshauri ni Inter Consult.

Kufuatia ujenzi huo unaosimamiwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) kuanza, Rwakatare ametangaza kuondolewa kwa kituo cha daladala cha Gerezani, Kariakoo kuanzia jana kupisha ujenzi huku akisema tayari watu wote waliopisha mradi huo wameshalipwa fidia na kuwataka wanaohusika wapishe mradi.

Tunaungana na mtendaji huyo wa BRT kuwataka watu wote waliolipwa kupisha mradi huo ili uweze kuanza na ujenzi wake kwenda vizuri na kwa kasi bila matatizo wala mkwamo wa aina yoyote ile.

Mradi huu kama ulivyo ule wa Awamu ya Kwanza wa barabara za Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni na Morocco hadi Magomeni ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii.

Ni kutokana na ukweli huu tunasema iko haja kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa awamu ya pili ya mradi huo unaojengwa kwa awamu ili wakandarasi hawa waweze kumaliza ndani au kabla ya muda.

Ni matumaini yetu kuwa, muda uliotolewa na BRT kwa wananchi waliolipwa fidia kuondoa vitu vyao katika eneo la mradi ulitosha kuwawezesha kuhamisha kila kilicho chao hivyo hatutarajii kilio chochote.

Tunasema hivyo kwa sababu kumekuwa na tabia au mazoea ya baadhi ya watu kung’ang’ania kubaki kwenye maeneo yanayotekelezwa miradi mbalimbali hasa ya barabara kwa madai ya kutolipwa fidia.

Ifike wakati wananchi waelewe vitendo kama hivyo siyo tu vinachelewesha miradi hiyo bali pia vinachangia kuikosesha serikali mapato kama miradi hiyo ingemalizika haraka na kufanya kazi sawia.

Hivyo, tunaungana na BRT kuwaomba wananchi na wakazi wa Dar es Salaam kwa jumla kutoa kila aina ya ushirikiano kwa wakandarasi katika barabara ya Kilwa muda wote watakaokuwa wakitekeleza mradi.

Ushirikiano huo uwe wa kuhakikisha usalama wa mali na nyenzo wanazotumia katika ujenzi kama mafuta, vipuri na magari, kokoto na kuheshimu alama za matumizi ya barabara watakazoweka kuongoza magari kwa zamu ili kurahisisha usafiri wa magari madogo, daladala na magari makubwa yatakayopita.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi