loader
Picha

Ukoma unavyoathiri sehemu za siri

UKOMA ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea (bakteria) wanaoshambulia ngozi na mishipa ya fahamu. Mbali na ngozi, sehemu nyingine zinazoathiriwa na vimelea vya Ukoma ni pua, macho na korodani.

Maambukizi ya Ukoma hutokea zaidi kwenye nchi zinazoendelea kuliko zile zilizoendelea ambako umedhibitiwa.

Hata kwenye nchi zinazoendelea, Ukoma umeendelea kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kinyume na ilivyokuwa siku za nyuma, ugonjwa wa Ukoma hauambukiziki kwa haraka na unatibika kama ilivyo kwa ugonjwa wa kifua kikuu.

Hata hiyvo, ugonjwa wa Ukoma usipotibika unaathiri mishipa ya fahamu.

Ugonjwa wa ukoma hauathiri ubongo au mishipa ya fahamu ya kwenye uti wa mgongo. Ukoma huambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine endapo kutakuwa na kukutana kwa karibu na kwa muda mrefu na mtu mwenye maambukizi ya Ukoma ambae hajapata tiba.

Mara mgonjwa wa Ukoma anapoanza tiba, anakuwa hana uwezo wa kuambukiza.

Ugonjwa wa Ukoma hauambukizwi kwa kushikana mikono au kukumbatiana, kukaa karibu au kula na mtu mwenye Ukoma. Hakuna uthibitisho kuwa Ukoma unaambukizwa kutoka kwa mama mjamzito kwenda mtoto tumboni. Dalili kubwa ya Ukoma ni alama zinazojitokeza kwenye ngozi.

Vimelea vyake huchukua muda mrefu kukua kwenye mwili na dalili zake mwanzoni hazihusishi maumivu, mara nyingi huchelewa kugundulika. Maeneo ya ngozi yalioathiriwa na ugonjwa huu huwa na mabadiliko kidogo ya rangi na sehemu hiyo hukosa hisia ikiguswa na kitu mfano kipini.

Kuthibitisha ugonjwa kunahitaji kuchukua chembechembe sehemu iliyoathirika ili kupima kwa darubini kuona kama vipo vimelea vinavyosababisha Ukoma.

Ukoma hausababishi kuoza na kukatika kwa vidole bali sababu ya kuathirikia kwa mishipa ya fahamu kwa mtu ambae hajapata tiba, vidole havipati hisia na kupata madhara ambayo yanasababisha vikatwe.

Kwa sababu ya kutokuwa na hisia, kunakoletwa na Ukoma, mtu anaweza kuumia au kuungua bila yeye kufahamu. Ukoma unaweza kuathiri mishipa ya fahamu ya macho na kusababisha upofu, na ulemavu wa miguu na mikono.

Vilevile, Ukoma unaweza kuathiri mapigo ya moyo, utokaji wa haja kubwa au ndogo na utoaji wa jasho kwa kuathiri mishipa ya fahamu inayofanya kazi kwenye maeneo hayo.

Ukoma ukigundulika mapema, unatibika na watu walioathirika wanaweza kuendelea na maisha na kazi zao kama kawaida wakati na baada ya tiba.

Usipotibika husababisha ulemavu hasa wa mikono na miguu. Vilevile unasababisha kuharibika kwa uso na pua.

Athari hizi zikitokea huwa hazirudi kwenye hali yake ya kawaida hata baada ya tiba. Hivyo ni muhimu ukigundulika, tiba ianze mapema kabla ya athari kuu.

Matibabu ya Ukoma ni kwa kutumia vidonge vinavyopatika kwenye vituo vingi ya afya na hospitali bila gharama. Dawa hizi hutumiwa kwa muda wa kati ya mwaka mmoja na miaka miwili. Dawa zinatakiwa kutumika wakati wote hadi daktari atakaposema matibabu yamekamilika.

Endapo ukoma umeshaathiri mishipa ya fahamu na kusababisha kutopata hisia kwenye mikono au miguu, ni lazima kuweka umakini mkubwa katika kutunza miguu au mikono.

Utunzaji huu ni pamoja na kuwa mwangalifu katika kutembea ili kuzuia kuumia mfano kujikata, kukanyaga misumari au moto.

Hii ni kwa sababu mtu ambaye mishipa ya fahamu imeathirikia, hatapata hisia akiumia na hivyo kusababisha kupata kidonda kikubwa bila yeye kujua wakati akiumia.

Kwa kuwa tiba ya Ukoma hata kama inaua vimelea vyote, haiwezi kurudisha mwili uliopata ulemavu kwenye hali ya kawaida, mara nyingi watu walioathirika na ulemavu wanapata unyanyapaa kwenye jamii.

Unyanyapaa huu ni kutengwa, kuzuiwa kula na kuchangamana na wanafamilia. Maambukizi ya Ukoma kutoka mtu hadi mtu hayatokei kama amepata tiba.

Ndio maana Kauli mbiu ya siku ya Ukoma Duniani, mwaka huu (27 Januari) ni “Tutokomeze ubaguzi, unyanyapaa na chuki dhidi ya waathirika wa ukoma”. Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni. Simu: 0786587900.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Dk. Faraja Chiwanga

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi