loader
Picha

Magufuli apongezwa kuboresha madini

SHIRIKISHO la Wachimbaji Madini Tanzania limempongeza Rais John Magufuli kwa kuwaboreshea mazingira ya kazi na biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo.

Rais wa shirikisho hilo, John Mabina amesema, Rais Magufuli na serikali yake wamefanya vizuri kwa kuandaa na kufanikisha Muswada uliopitishwa bungeni mwishoni mwa wiki ambao unatoa unafuu kwa wachimbaji wadogo wa madini.

“Kwa kweli tumefurahi sana na kwa kuonesha furaha yetu tumeandaa maandamano Jumamosi hii kumpongeza Rais kwa kutujali sisi wachimbaji wadogo wa madini hapa nchini,” amesema.

Juzi Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ambao pamoja na mambo mengine unaondoa kodi ya zuio la asilimia tano inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini kwa wachimbaji wadogo na kurekebisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kutoa msamaha kwenye madini ya metali na vito yatakayouzwa katika masoko ya ndani ya nchi.

Mabina amesema maandamano hayo yatafanyika nchi nzima katika mikoa yote kuonesha kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara hao ambao ni wachimbaji wadogo wa madini.

Aidha, alisema kwa punguzo hilo sasa wachimbaji wa madini wadogo wamebaki na tozo moja la asilimia sita la ‘loyalty’ pekee, jambo ambalo linatoa unafuu mkubwa kwao.

“Rais wetu ni msikivu amesikia kilio chetu na kutupa unafuu sisi wachimbaji wa madini na sisi tunampongeza sana kwa moto wake huo,” amesema Mabina.

Alisema baada ya unafuu huo wachimbaji wadogo sasa wataingia kuuza madini yao katika masoko rasmi yaliyowekwa na serikali. Marekebisho hayo ya Muswada yanakusudia kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo ambako masoko ya madini hayakuwepo na kuweka utaratibu wa uingizaji madini nchini.

Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana aliishauri serikali kuandaa masoko hayo rasmi haraka ili serikali ikusanye mapato yake.

Alisema maboresho ya Muswada huo yanaonesha wazi kuwa Rais Magufuli anatekeleza kwa vitendo ahadi zake na pia anatekeleza kwa wakati.

“Haijapita wiki tatu tangu Rais azungumze na wafanyabiashara wa Sekta ya Madini na wao kumueleza changamoto zao, lakini tumeona Muswada umeenda bungeni na kupitishwa ni dalili kuwa Rais anatenda tena kwa wakati,” amesema Dk Bana.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imewataka wadau wa habari kufanya utafiti ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi