loader
Picha

Muuguzi apigwa stop kwa ulevi

BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemsimamisha Martin Chama kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa muda wa mwaka mmoja kwa tuhuma za kufi ka kazini akiwa amelewa na kutaka kuhatarisha usalama wa wagonjwa na ndugu zao kwa kushindwa kutoa huduma kwa umakini na weledi.

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Agnes Mtawa alisema hayo katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam.

Mtawa amesema kikao cha baraza hilo cha 196 kilimsimamisha kazi muuguzi huyo Chama kuanzia Februari 7, mwaka huu kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa katika baraza hilo Septemba, mwaka jana.

Amesema awali Ofisi ya Msajili wa Baraza hilo lilipokea tuhuma kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru Arusha kupitia kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Msimamizi wa Maadili wa Mkoa wa Arusha kwa mujibu wa Sheria N0 1 ya Mwaka 2010.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo muuguzi huyo alifika kazini Septemba 26, mwaka jana zamu ya usiku majira ya saa tatu usiku akiwa amelewa na alianza kuwasumbua ndugu waliokuwa wakiwaangalia wagonjwa wao kutaka kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa ili hali akiwa amelewa sana hali ambayo ingehatarisha maisha ya wagonjwa kwa kuwa hakuwa na umakini.

“Tuhuma hizi ziliwasilishwa na walalamikaji wawili waliokuwa wakiuguza wagonjwa wao,” amesema.

Alisema baada ya hapo Ofisi ya Msajili ilituma ofisa kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga ambaye aliungana na timu ya mkoani Arusha ikiongozwa na Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, timu ambayo ilifanya uchunguzi wa awali na kubaini upungufu uliofanywa na muuguzi huyo kinyume na Maadili ya Uuguzi na Ukunga.

“Taarifa hiyo ilipelekwa katika kikao cha dharura cha Bodi cha 195 ambacho pamoja na mambo mengine kilijadili taarifa hii na kuamua shauri hili lisikilizwe katika kikao cha Bodi cha 196 ambayo itahusisha mtuhumiwa na mashahidi ambao ni walalamikaji na watumishi waliokuwepo siku ya tukio,” amesema.

Aliongeza kuwa shauri hilo lilisikilizwa Februari 7, mwaka huu ambapo ushahidi uliotolewa umemtia hatiani mlalamikiwa kwa kulewa na kushindwa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa weledi na kutaka kuhatarisha maisha ya wagonjwa na ndugu zao.

Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka iliyoanzishwa kisheria na kufanya kazi chini ya Sheria inayoitwa The Nursing and Midwifery Act, of 2010.

Baraza lilianzishwa kwa ajili ya kulinda umma kutokana na huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini na linafanya kazi kwa kusimamia ubora katika mafunzo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vilivyowekwa.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imewataka wadau wa habari kufanya utafiti ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi