loader
Picha

Mama ashuhudia mwanawe akiuawa

WATU wawili mkoani Mbeya wameuawa katika matukio mawili tofauti, ambapo katika tukio la kwanza Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwanjilo wilayani Mbeya, Steven Tumpikile kwa mahojiano kuhusu tukio la mauaji ya mkazi wa kijiji hicho.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, Mwenyekiti huyo wa kijiji anashikiliwa kutokana na mauaji ya Zawadi John maarufu kwa jina la Nambariwan (35) mkazi wa Kijiji cha Lwanjilo aliyeuawa kwa kumkata na vitu vyenye ncha kali, kutobolewa macho na kisha kuchomwa moto mbele ya mama yake mzazi.

Kamanda Matei amesema tukio la mauaji ya kijana Zawadi lilitokea Februari 7, mwaka huu saa 1:00 usiku katika kijiji na kata ya Lwanjilo, Tarafa ya Tembela, Mbeya Vijijini ambapo wananchi wa kijiji hicho waliamua kujichukulia sheria mikononi.

Walimtuhumu Zawadi kuvunja nyumba ya Lufi Fungo majira ya mchana wa siku hiyo na kuiba kitanda kimoja cha mbao ukubwa wa futi 4 kwa 5 pamoja na godoro lake.

Pia kuiba tena nyumbani kwa Elizabeth Sanga debe tatu za ngano, tuhuma alizosema hazikuwa zimeripotiwa polisi.

Kamanda huyo aliongeza kuwa mara baada ya wizi huo wananchi waliendesha msako wakiongozwa na wenyeviti wa vitongoji ambao ni Alikado Daudi maarufu kwa jina la Msemwa na Jofrey Langison.

Katika msako huo walimkamata marehemu na vitu hivyo na kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali, hatimaye kufariki dunia na mwili wake kuchomwa moto.

Alisema mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha makubwa kichwani na kutobolewa macho na kisha kuunguzwa kwa moto na kuongeza kuwa tayari mwili huo ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na daktari wa Hospitali Teule ya Ifisi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.

Aidha Kamanda Matei amesema msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa walioshuhudiwa na mama mzazi wa marehemu wakitekeleza unyama huo zinaendelea sambamba na upelelezi wa tukio husika.

Katika tukio la pili, Kamanda Matei alisema jeshi hilo linawashikilia Friday Mwamakula (35) na Boy Ningu (56) wote wakazi katika kitongoji cha Ngisi kijiji cha Kilwa wilayani Kyela kwa tuhuma za mauaji ya ndugu yao aliyekuwa mkazi wa kitongoji hicho aliyefahamika kwa jina la Rashid Mwamakula (67).

Alisema tukio la mauaji hayo lilibainika Februari 8, mwaka huu saa 2:00 asubuhi katika kitongoji cha Njisi kilichopo Kijiji cha Kilwa, Kata ya Kajunjumele, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela ambapo watu wasiojulikana walimvamia marehemu akiwa amelala chumbani kwake peke yake na kisha kumuua kwa kumkata na kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali.

Alibainisha kuwa wakati tukio hilo likitokea, mke wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Nitike Katete (62) mkazi wa Kitongoji cha Njisi alikuwa ameenda kwenye msiba wa mjukuu wake katika kitongoji hicho hicho na aliporudi alikuta mume wake ameuawa.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imewataka wadau wa habari kufanya utafiti ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Mbeya

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi