loader
Picha

Shule iliyoshika mkia Kagera yawaibua madiwani, wazazi

 SHULE ya Sekondari ya Rwemondo ni miongoni mwa shule za umma zilizoko katika Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera. Shule hiyo inayopatikana katika kata ya Ishunju, ikihudimia baadhi ya wanafunzi kutoka kata ya Ishozi imeonekana kutia doa katika Mkoa wa Kagera kwa kushika mkia. Kufutia matokea ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2018, shule hiyo pia ni miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya nchini. Shule hiyo yenye wanafunzi 301 kwa sasa ina walimu 18, miongoni mwao walimu wa masomo ya sanaa ni 14, walimu wa masomo ya sayansi watatu na mwalimu mmoja wa hesabu.

Uchunguzi unaonesha kwamba zipo shule ambazo zina walimu watano au sita zimeendelea kufanya vizuri kwa kupatikana hadi wanafunzi waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza. “Mara nyingi wanasema hatuna walimu wa sayansi lakini wakati huo huo walimu wa masomo ya sanaa wamejaa tele. Sasa kama masomo ya sayansi hayana walimu ni kwa nini wanafunzi wasishinde hata hayo ya sanaa?” Anahoji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho.

Januari 31, mwaka huu, Tegamaisho pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Missenyi, Innocent Mkandara, waliitisha kikao cha baraza la madiwani, walimu wakuu wa shule za sekondari na maofisa elimu kata ili kubaini ni sababu gani za msingi zilizofanya shule hiyo kufanya vibaya. Wengine walioshiriki katika kikao hicho ni wakuu wa idara, viongozi wa chama tawala (CCM) na wadau kadhaa wa elimu. Katika kikao hicho kilichotumia muda wa saa saba kujadili maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo huku suala la shule hiyo likitawala Mwenyekiti Tegamaisho anasema kupitia vikao vya baraza la madiwani amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa diwani wa kata hiyo kuwa baadhi ya waalimu wa shule hiyo ni watovu wa nidhamu na wasiotimiza majukumu yao ipasavyo.

Anasema siku moja alifika shuleni hapo ili kuleta suluhu baina ya viongozi wa kata kupitia kwa diwani huyo na waalimu ambapo aliwataka wakae pamoja na washirikiane ili kuleta ufanisi katika shule hiyo. “Nilishapokea malalamiko na nilifika kuyafanyia kazi. Nataka tu niwaambie sisi kama halmashauri tunatumia nguvu kubwa kuhimiza na kusimamia ukusanyaji wa mapato.

Tunawaletea fedha mnajenga maabara nzuri, mnapokea walimu wazuri sasa kuna haja gani ya kuleta fedha kama mnapata sifuri? Hii inatukatisha tamaaa,” anasema Tegamaisho. Anasema Halmashauri ya Missenyi haijawai kupata nafasi mbaya kielimu na kwamba hii ni mara ya kwanza kwa halmashauri hiyo kuwa ya mwisho mkoani Kagera. Diwani wa kata ya Ishunju ilipo shule hiyo, Msafiri Nyema, anasema amepeleka malalamiko mara nyingi katika sehemu mbalimbali lakini ni wachache waliomwelewa. “Takribani wanafunzi wote wamefeli. Hakuna shule ambayo inaweza kufanya vizuri bila walimu na wanafunzi kuzingatia nidhamu,” anasema diwani huyo. Anadai kwamba kwa miaka mitatu mfululizo shule hiyo imekuwa haifanyi vizuri na kwamba walimu wa shule hiyo wanachangia pakubwa katika kuwafanya wanafunzi kufeli.

Anasema kuna baadhi ya walimu katika shule hiyo ni walevi na wapo wenye mahusino yasiyofaa na wanafunzi wao, jambo ambalo limeshalalamikiwa sana na wazazi bila kupata majibi ya uhakika. “Wazazi wanawatuhumu walimu kuwapa mimba watoto wao lakini pia wanafunzi wanatumia muda mwingi kufanya kazi za walimu, sasa mimi kiongozi ninapokemea wanasema siasa imeingilia shule au diwani amemuingilia mtumishi wa Umma. “Naamini madiwani wenzangu mtanielewa ni kitu gani nilikuwa namaanisha.

Mpaka sasa kuna mwalimu amemuoa mwananfunzi. Lakini mtakumbuka kuwa siku chache zilizopita walimu wawili walipigana na kuumizana wakigombea mwanafunzi mmoja wa kike,” anasema. Anasema katika shule hiyo ni kawaida walimu kuja kazini wakiwa wamechelewa na wengine wanapitia baa kwanza.

Diwani hiyo anaomba ukaguzi uwe unafanyika mara kwa mara katika shule hiyo ili kuabini vitendo viouvu vinavyofanyika na pia anawataka wakuu wa shule kuacha tabia ya kusingizia viongozi waliochaguliwa na wananchi kuwa wanaleta siasa shuleni wanapokuwa wanasimamia nidhamu za utendaji kazi katika taasisi za umma. William Ruta, Diwani wa kata ya Ishozi anasema nguvu kubwa inahitajika ili kuhakikisha watoto wanafaulu vizuri masomo yao ya sekondari wilayani humo. Anasema katika halmashauri hiyo hata wanafunzi wakifanya vizuri ni asilimia 30 ambao wamekuwa wakiendelea na masomo ya kidato cha tano.

“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri. Ninachoweza kusema ni kuhakikisha tunatumia nguvu kubwa kusimamia elimu na tutumie nafasi yetu ya kufanya vibaya kama mwanzo wa kugundua tumeanguka wapi na tuanze moja kwa moja kufanya vizuri zaidi,” anasema Ruta. Saverina Misinda, Afisa elimu wa Wilaya ya Missenyi anasema tayari ameshapokea malalamiko mbalimbali kutoka kwenye Kamati ya Shule ya Sekondari Rwemondo hivyo ameunda tume itakayochunguza hali iliyopelekea shule hiyo kufanya vibaya na kwamba baada ya uchunguzi huo hatua stahiki zitachukuliwa.

Anasema shule hiyo kwa sasa amepelekwa mwalimu mkuu mpya ambaye ametakiwa kurudisha umoja na mshikamano wa kazi na kuhakikisha shule hiyo inarudi katika nidhamu bora. Mwalimu huyo mkuu, Eliberius Leopord anasema kwa muda wa mwezi mmoja ambao amekaa katika shule hiyo amebaini madudu kadhaa na kwamba nidhamu katika shule huyo haijakaa vyema. Anasema alipofika shule hapo siku ya kwanza alishindwa kutofautisha walimu na wanafunzi kwani alikuta mwonekano wa walimu na wanafunzi ukiwa wa kufanana.

“Napenda niwahakikishie madiwani kuwa nyie ni sehemu ya kuboresha shule yetu. Shule ina miundombinu mizuri, lakini vitendo vya ulevi na utovu wa nidhamu vimesababisha shule yetu kufanya vibaya. Ninachoweza kusema nitahakikisha nasimamia nidhamu na nina imani shule itarudi katika ubora na walimu watovu wa nidhani tutawachukulia hatua,” anasema Mwalimu Leopord. Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Mkandara, anaahidi kufanya ziara maalumu katika shule zote kwa kushirikiana na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, jambo ambalo litawasaidia kubaini changamoto mpya zinazowakabili walimu na wanafunzi.

Hata hivyo, anatupa lawama zake kwa wakaguzi wa shule ambao mara nyingi wanatoa taarifa kabla ya mwezi mmoja kwenda kukagua shule hivyo walimu wanajiandaa katika kuandika majibu ya uongo. Ni kwa mantiki hiyo anasema ni vema warudishe mfumo wa zamani wa mkaguzi kuja ghafula na kubaini kinachoendelea shuleni ili walimu wawajibishwe pale inapobainika hawatekelezi wajibu wao. “Naweza kusema kuwa hata hapa tuna mkaguzi, nimekuwa nikimwambia nitampa mafuta lakini saa nyingine ananiomba posho na hizo posho hakuna.

Hata sisi tunashinda vijijini hatupewi posho kwa hiyo namwomba mkaguzi tuliye naye afanye kazi yake ipasavyo,” anasema Mkandala. Kufuatia shule hiyo kufanya vibaya viongozi wa Shama cha Mapinduzi wilayani Missenyi wakiongozwa na Katibu wa chama hicho wa wilaya, Mwajuma Mboha, wamefanyia maadhimisho ya miaka 42 katika shule hiyo ambapo walikutana na kamati ya wazazi ya shule ili kuona namna bora ya kuinusuru shule hiyo kitaaluma.

Wana-CCM hao wanasema wao kama wazazi, wako tayari kushirikiana kikamilifu na kamati ya shule ili kuifanya shule hiyo kuwa bora. Viongozi hao hawakusita pia kutupa lawama kwa waalimu kwamba ndio wamechangia sana kuifanya shule hiyo kufanya vibaya.

“Tumepigana sana lakini walimu wanatujibu vibaya. Unakuta mwanafunzi wa kike anamiliki simu aliyonunuliwa na mwalimu. Shule haiwezi kushinda katika mazingira kama hayo,” anasema mmoja wa wazazi katika shule hiyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini. Nao wazazi kupitia kamati yao walimhakikishia katibu wa CCM kuwa watashiriki kutoa chakula na kuchangia gharama za watoto ili muda wa masomo uongezeke badala ya kutoka saa 9:00 hususani kwa wanafunzi watahiniwa. Mbunge wa jimbo la Misenyi, Dk Diodorus Kamala alipotembelea Shule ya Sekondari Ya Rwemondo miaka ya nyuma. Mwaka jana shule hiyo imekuwa miongoni mwa shule 10 zilizoshika mkia kitaifa.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi