loader
Picha

Wabunge wataka mpango kuboresha biashara

WABUNGE wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki wameikumbusha serikali kuhakikisha inakamilisha Mpango wa Kuboresha Biashara nchini (Blue Print) na pia kuunda Kamati ya Biashara ili kuboresha mazingiraya biashara kwa Mtanzania katika soko la Afrika Mashariki.

Wabunge hao mwishoni mwa wiki walitoa tamko hilo baada ya kutembelea taasisi za serikali, kukutana na wafanyabiashara pamoja na makundi mbalimbali ya watu na asasi za kiraia.

Mwenyekiti wa wabunge hao tisa kutoka Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema kwa kuwepo na ‘Blue Print’ na kamati ya biashara kutatoa fursa kwa wafanyabiashara hapa nchini kufanya biashara kwa uhuru na kutumia fursa zilizopo za kibiashara.

Dk Makame alisema wafanyabiashara wa Tanzania wanakosa ushindani kutokana na vikwazo mbalimbali vinavyokuwepo hapa nchini ambapo suluhisho lake ni mambo hayo mawili pamoja na elimu ya kutosha kuwafanya watambue fursa zilizopo ndani ya jumuiya.

Wabunge hao pia walihoji kwanini visitokomezwe vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru ndani ya jumuiya kama ambavyo imeelekezwa katika mkataba wa Afrika Mashariki na mkataba wa umoja wa forodha ndani ya jumuiya.

“Bunge limeagiza kuundwa kamati ya biashara ndani ya Afrika Mashariki na hiyo ni kwa mujibu wa ibara ya 24 ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki kwani ilitungwa sheria na nchi zikaahidi kuundwa kamati hiyo ya kusimamia biashara.

“Vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru ndani ya Afrika Mashariki vimejadiliwa sana katika mikutano mbalimbali ndani ya Afrika Mashariki miaka mingi tangu Itifafaki ya Umoja wa Forodha ianze 2015 na juzi kwenye mkutano wa wakuu wa nchi ilijitokeza,” alisema Dk Makame kwa niaba ya wabunge wenzake.

Amesema wao kama wabunge wanasimamia sheria na makubaliano hawawezi kukubali kuona kamati haijaundwa mpaka sasa na wametoa mwito kwa mamlaka husika ndani ya serikali pamoja na baraza la mawaziri kuona kamati hiyo inaundwa.

Aidha, amesema kamati hiyo itasaidia kusimamia migogoro, mivutano na kusimamia mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wote ndani ya jumuiya hiyo.

Dk Makame alisema wabunge walipotembelea Bandari ya Dar es Salaam walipongeza baadhi ya mambo katika bandari hiyo na hasa kwa ongezeko kubwa la mizigo inayopita hapo lakini waliitaka mamlaka hiyo kukabiliana na ongezeko hilo kwa kuondoa ucheleweshaji wa kutoa mizigo.

Amesema baada ya ongezeko la mizigo hiyo, bandari haikua imejipanga kuboresha mifumo pamoja na kuwa na watumishi kuendana na ongezeko hilo jambo ambalo likasababisha ucheleweshaji wa mizigo kutoka bandarini.

MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi