loader
Picha

Mahakama Kuu Mwanza: Mpe raha mteja, mahakama ing’are

UTOAJI haki kwa wakati ni moja ya hitaji la kikatiba na moja ya haki za msingi za binadamu. Kwa mujibu wa Ibara ya 107 A (2) (b) ya katiba, mahakama ndicho chombo kilichopewa jukumu la utoaji haki. Wananchi wengi, hususani wanyonge wamekuwa na vilio vya muda mrefu vya kutafuta haki kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuporwa viwanja vyao, kudhulumiwa mali zao, kuibiwa na kadhalika na kadhalika. Hata hivyo, mahakama imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kuzidisha madhila kwa wananchi kwa kutopewa nakala za hukumu kwa wakati, kesi kuchukua muda mrefu, kufichiwa mafaili yao ya kesi na mengine kama hayo.

Wananchi wamekuwa wakilalamikia kuwekwa mahabusu bila dhamana, kupigwa, kubambikiziwa kesi na changamoto nyingine kadha wa kadha. Wakati huu nchi yetu inapokusanya nguvu kuelekea uchumi wa kati, utoaji haki kwa wakati unaelezwa kuwa na umuhimu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote. Katika hili kila mtu anayetoa haki ana wajibu wa kuhakikisha kwamba katika eneo lake hakuna haki inayocheleweshwa. Ni kutokana na umuhimu na msingi huo wa utoaji haki kwa wakati, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza imekuja na kampeni maalumu itakayohakikisha kuwa haki inatendeka na kupatikana kwa wakati.

Ingawa kaulimbiu ya kitaifa ya mahakama ya mwaka huu ni ‘Utoaji haki kwa wakati; wajibu wa mahakama na wadau’, mahakama hiyo imekuja na kampeni hiyo inayojulikana kama: “Mpe raha mteja, mahakama ing’are.” Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Sam Rumanyika, anasema kampeni hii ilianzishwa miezi mitano iliyopita, misingi yake ikiwa mikuu mitatu ambayo ni haki yako wajibu wangu, kila hakimu aingie mahakamani na kuamua mashauri na kwamba mlundikano wa kesi ni sumu kwa taifa.

Akizungumza katika kilele cha Siku ya Sheria wiki iliyopita, Jaji Rumanyika anasema mahakama katika kanda hiyo imeamua kuanzisha kampeni hiyo ili kuwawezesha wateja kupata huduma bora, stahiki na ambazo hutolewa kwa wakati.

Anasema endapo mwananchi anayekwenda mahakamani kutafuta haki hatohudumiwa shauri lake kwa wakati, mahakama haiwezi kung’ara. Kwamba endapo malalamiko au kesi yake itakaa mahakamani kwa muda mrefu, mteja atakosa raha na kama atalazimika kusafiri kwa umbali mrefu akisaka huduma ya mahakama na bado ikacheleweshwa atazidi kuichukia mahakama. “Mteja atakosa raha kama atakwenda mahakamani na kuahirishiwa kesi yake bila sababu. Yote hayo yakitokea, mahakama haitang’ara, itabaki imefubaa,” anaeleza. Anasema tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo utendaji wa shughuli za mahakama Kuu Kanda ya Mwanza umeboreshwa na kwamba mahakama imeendelea kutekeleza dhana ya huduma ya haki, ambayo kimsingi inamlenga mwananchi. Anasema dhana ya huduma ya haki ambayo iko kwenye Mpango Mkakati wa Mahakama ina

msingi wake kwenye dhana ya uimarishaji wa utawala na sheria, ushirikishwaji wa wadau katika kutoa huduma ya haki na fursa ya kupata haki sawa na kwa wakati. Anasema dhana ya utoaji huduma ya haki ni wajibu wa mahakama na wadau. Anawataja wadau hao wengine kuwa ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, mawakili, viongozi wa dini, serikali, bunge na wananchi kwa ujumla.

Anawataja wadau wengine kuwa ni pamoja na asasi za kijamii za kutoa msaada wa kisheria, mabaraza ya ardhi na nyumba, maofisa ardhi, mabaraza ya usuluhishi, madalali wa mahakama na wandishi wa habari.

MAFANIKIO

Anasema kutokana na kuanzishwa kwa kampeni hiyo, matunda yameanza kuonekana na kwamba takwimu za umalizwaji mashauri mahakamani katika ngazi mbalimbali kwa wakati ni nzuri. Anasema hadi kufikia Januari 31 mwaka jana, Mahakama Kuu kanda hiyo ilikuwa na jumla ya mashauri 1978 ambapo 513 yalikuwa ya mauaji. Anasema wastani wa kesi 190 zinapokelewa kwa mwezi lakini kwa sasa wastani mashauri ya kesi 380 humalizwa kwa mwezi.

“Maana yake ni kwamba tunamaliza kesi nyingi kuliko zinazoingia, kwetu haya ni mafanikio makubwa,” anasema. Kwa upande wa mahakama za mwanzo, ambazo kwa mujibu wa tafiti, anasema, ndiko kwa siku husajiliwa asilimia 70 ya mashauri yote nchini, hali ya uendeshaji wa kesi pia ni mzuri katika kanda hiyo. Anasema mahakama nyingi, hususani katika wilaya ya Chato mkoani Geita hadi kufikia Desemba mwaka jana, wilaya hiyo ilikuwa ilikuwa na kesi sifuri.

“Tumedhamiria mahakamani kusiwe tena mahali pa wananchi kupoteza muda wao mwingi kutafuta haki na badala yake muda wao wautumie katika kuzalisha mali,” anasema. Anasema kupitia katiba, sheria, kanuni na miongozo iletwayo na viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, imesaidia sana katika kuboresha huduma za Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza. Anasema kupitia miongozo hiyo, mashauri mahakamani hupaswa kuanza kusikilizwa saa tatu asubuhi.

Kwa upande wa mahakama kuu kesi zinapaswa kuisha ndani ya miaka miwili, mahakama za mkoa na wilaya mwaka mmoja na nusu na zile za mwanzo kesi zinapaswa kuisha ndani ya kipindi cha miezi sita. Anasema Jaji wa Mahakama kuu anapaswa kusikiliza 220 kwa mwaka, hakimu wa mahakama ya mkoa na wilaya kesi 250 na hakimu wa mahakama ya mwanzo kesi 260. “Nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi vinapaswa kutolewa ndani ya siku 21 na 90,” anasema Jaji Rumanyika.

Anawakumbusha mahakimu kujua kwamba wanapokuwa na majalada ya kesi, kwa mfano 50 mezani kwao kwa mwaka au hata zaidi bila ya kuyatolea uamuzi, bai wajue muda wote huo zaidi ya watu 100 watakuwa kwenye foleni mlangoni kwao, jambo ambalo halikubaliki. Anasema kama ni kiwanda, shamba, duka au shule ndiyo inayohusika kwenye mgogoro na hivyo kufungwa badi hakimu au jaji atambue kuwa kwa mwaka mzima atakuwa ameshimamisha uzalishaji. Jaji hiyo anasisitiza: “Haki siyo bidhaa wala huduma inayoweza kuuzika.” Anasema ndiyo maana zile mahakama chache za mwanzo na mabaraza ambayo kinyemela, huwachangisha wateja gharama za huduma wanakemewa sana na mahakama kuu. Anasema, endapo mtu ataamuriwa kulipa Sh 20,000 za kutembelea eneo la tukio lenye mgogoro, kati yao atakayeshindwa kesi atamshuku mwenzie, kwa kudhani alitumia huo mwanya na kupenyeza fedha zaidi kama mlungula.

“Utoaji haki kwa wakati na kwa usawa pia huzingatia makundi maalumu kwenye jamii kama vile watu wenye ulemavu, yatima na wale waishio kwenye mazingira magumu, wajane na wazee,” anasema Jaji Rumanyika.

Anaongeza kuwa mahakama itaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma na kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati. Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela anasema serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na mahakama kwa kutatua baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa ni kikwazo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya mahakama.

Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mwanza, Casutuce Ndamugoba anasema katika utekelezaji wa dhana ya utoaji haki kwa wakati, mahakama nchini bado zinakabiliwa na changamoto zinazoifanya kushindwa kutenda haki kwa wakati. Anazitaja changamoto hizo kuwa ni majaji na mahakimu kutumia muda mrefu kuandika ushahidi au mwenendo wa kesi kwa mkono, wakifanya kazi mbili kwa wakati mmoja, wakisikiliza mashahidi na kuandika ushahidi.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imewataka wadau wa habari kufanya utafiti ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi