loader
Picha

Yanga yapata zawadi ya bethidei Tanga

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga leo wanasheherekea bithidei ya miaka 84 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1935.

Yanga wanaikumbuka siku hiyo wakiwa na raha ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Ushindi huo unahitimisha mwenendo wa matokeo yasiyoridhisha ikiwa ni baada ya kufungwa bao 1-0 na Stand United, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union na sare ya bila kufungana na Singida United.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 58 huku Azam ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 48 na Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36, lakini yenyewe ina michezo minane mkononi.

Lakini pia ni faraja kwa timu hiyo kuelekea mchezo dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Simba utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Jumamosi ijayo.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilionesha dhamira ya kuibuka na ushindi tangu dakika za mwanzo za mchezo huo lakini mara kadhaa washambuliaji wake Amis Tambwe, Mrisho Ngassa na Pius Buswita walikosa umakini katika kutumia nafasi hizo.

Hali ya uwanja wa Mkwakwani haikuwa rafiki kwa timu zote mbili kwani mara kwa mara walionekana kupoteza mipira au kushindwa kumiliki mipira vizuri.

Hata hivyo Yanga walifanikiwa kuandika bao pekee katika mchezo huo lililofungwa na kiungo Feisal Salum kwenye dakika ya 27 akimalizia krosi nzuri ya beki Gadiel Michael.

Kipindi cha pili, JKT Tanzania walionekana kutawala mchezo kwa kiwango kikubwa na kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto alionekana kuwazidi uwezo viungo wa Yanga walioongozwa na Papy Kabamba Tshishimbi.

JKT walipata nafasi kadhaa za kufunga kama washambuliaji wake wakiongozwa na Ally Shiboli wangekuwa makini basi wangeweza kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alifanya mabadiliko kwa kumtoa Mrisho Ngassa na kuingia Mohamedi Issa ’Banka’ na huo ukiwa mchezo wa kwanza kwa kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania baada ya kumaliza adhabu ya kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Zahera pia aliwatoa Ibrahim Ajibu na Pius Buswita na kuwaingiza Deus Kaseke na Kelvin Yondani na kuimarisha safu ya ulinzi ya Yanga.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya KMC dhidi ya Alliance uliopigwa Uwanja wa Uhuru na kumalizika kwa sare ya mabao 1-1, hivyo KMC kubaki nafasi ya nne na Alliance nafasi ya nane.

KIPA wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Aishi ...

foto
Mwandishi: Rahimu Fadhili

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi