loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vifo vya wajawazito vyaongezeka Songwe

JINAMIZI la vifo vya wajawazito limezidi kuukumba Mkoa wa Songwe ambapo wakati maeneo mengine nchini vikiendelea kupungua, mkoani vinaongezeka kwa kasi.

Takwimu zinaonesha kuwa bado vifo hivyo vya uzazi mkoani hapa vinaongezeka mwaka hadi mwaka kwani mwaka 2016 vilikuwa 26, mwaka 2017 vikawa 27 na mwaka 2018 vikaongezeka zaidi na kufikia 32.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemus Mwangela alibainisha hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga mkoani humo ya kupitia Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama, Maneno Basi Sasa Vitendo’.

“Tumeamua kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kupitia kampeni hii. Hatufanyi vizuri katika kutokomeza vifo vya wajawazito kwani takwimu zinazidi kupanda,” alisema.

Alitaja baadhi ya sababu zinazosababisha vifo hivyo kuwa ni pamoja na kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba, maambukizi ya virusi vya Ukimwi, upungufu wa damu na kuharibu mimba.

Hata hivyo alisema iwapo wakuu wa wilaya wakisimama vema kuwasimamia na kuwawajibisha watendaji walioko chini yao, mkoa unaweza kupunguza vifo hivyo.

Pia aliwataka wataalamu wa tiba, familia na wananchi kuhakikisha mama mjamzito anapumzika, anapata chakula kinachostahili na pia kuimarisha mfumo wa utoaji elimu ya masuala ya uzazi.

“Mkoa unayo kazi kubwa ya kutokomeza vifo hivi na leo tumezindua kampeni hii ambapo wakuu wa wilaya zote mkoani Songwe wamesaini hati ya makubaliano ya kutoa kipaumbele katika afya ya uzazi na mtoto,” alisema.

Mwangela alisema makubaliano hayo yanalenga kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto, kuwezesha asilimia 50 ya vituo vya afya kutoa huduma ya upasuaji wa akinamama wajawazito na huduma ya damu salama.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Kheri Kagya alisema kampeni hiyo inalenga maeneo tisa ikiwa ni pamoja na kutoa huduma rafiki kwa vijana, elimu na ushauri nasaha, vipimo na matibabu stahiki na kuhakikisha mjamzito anajifungulia katika kituo ambacho kina wataalamu wenye ujuzi, vifaa tiba muhimu na dawa.

Maeneo mengine ni huduma za dharura kwa matatizo yatokanayo na uzazi, damu salama na ya kutosha, ushirikishwaji wa jamii, taarifa ya kifo cha uzazi na mtoto mchanga pamoja na huduma za rufaa.

Aliitaja mikakati iliyowekwa ili kufikia malengo ya mpango huo kuwa imelenga kuboresha huduma kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, huduma kwa mtoto mchanga, huduma baada ya kujifungua na huduma kwa vijana.

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Mbozi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi