loader
Picha

Hifadhi za bahari, maeneo tengefu ni mgodi ambao haujachimbwa (2)

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) zinapatikana kwenye maeneo yote ya Hifadhi za Bahari kutokea pwani ya Mashariki ya Mafi a hadi kwenye fukwe ndefu zenye mchanga safi za Msimbati huko Mtwara na kwenye matuta ya mchanga wa kisiwa cha Maziwe huko Tanga, na Visiwa vya Dar es Salaam.

Maeneo yote hayo yanafaa sana kwa utalii. Fursa ya kuona viumbe aina ya kasa wakianguliwa kutoka kwenye viota vyao na kuelekea baharini. Viota hivyo hulindwa na kuhifadhiwa kwa kushirikiana na jamii ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya Pwani. Mfano ni Kijiji cha Ushongo – Tanga na maeneo mbalimbali ya Kisiwa cha Mafia. Kuangalia aina ya popo wanaokula matunda katika Kisiwa cha Mafia. Popo hao hutembea kwa makundi makubwa wajulikanao kitaalamu kwa jina la (Pteropussychellensis comorensis) na hupatikana tu katika visiwa vya Mafia (Tanzania), Seychelles na Comoro.

Pamoja na vivutio hivyo tajwa sehemu za hoteli zilizoko katika fukwe na visiwa pamoja na huduma zake ni vivutio vikubwa kwa wageni. Hoteli hizo ni kama Shungimbili, hoteli ya nyota tano kule Mafia, safu za hoteli pwani ya Ushongo Pangani –Tanga pamoja na Dar es Salaam. Aidha, mpango madhubuti wa serikali kuanzisha chaneli ya Utalii katika Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) utaongeza fursa za utalii zilizopo katika Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu katika nchi yetu kuyatangaza maeneo haya na vivutio vilivyopo badala ya kuendelea kutangaza maeneo ya nchi kavu pekee.

Kwa mtazamo wangu, chaneli hii ya Utalii italeta mageuzi makubwa ya utalii wa majini na kuongeza mapato ya serikali kwa kuchangia kukuza utalii wa; kuogelea kwa kutumia vifaa maalumu, utalii wa kuogelea na samaki wakubwa kama nyangumi wanaohama na samaki mkubwa kuliko wote duniani ‘whale shark’.

Kuvinjari kwa kutumia boti katika bahari, mito na maziwa “cruising”, kuota jua katika fukwe, utalii wa kutembelea magofu katika mwambao na visiwa vilivyoko baharini, utalii wa uvuvi wa burudani au mchezo maarufu kama sport fishing, utalii wa kula vyakula vya pwani na hata utalii wa kushuhudia utotoaji wa kasa.

Katibu Mkuu wa Uvuvi, Dk Rashid Tamatama anasema, Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ni Kitengo kilicho chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta Kuu ya Uvuvi) na kimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Namba 29 ya Mwaka 1994 chini ya usimamizi wa Bodi ya Wadhamini. Bodi hii imepewa jukumu la kuanzisha, kusimamia, kudhibiti na kuongoza shughuli za uhifadhi katika maeneo yaliyotangazwa kuwa Hifadhi za Bahari (Marine Parks) na Maeneo Tengefu (Marine Reserves). Taasisi hii ilianza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mwaka 1995 kwa kuwatumia watumishi wa Idara ya Uvuvi.

Hadi kufikia Julai, 2000, kitengo kilipopata ikama na kuajiri watumishi wake na hivyo, kupanua wigo wa utekelezaji wa majukumu yake. Anasema wazo la kuanzishwa Hifadhi za Bahari Tanzania, lilianzia katika miaka ya 1960 baada ya watafiti kutoa mapendekezo kwa serikali ya awamu ya kwanza kuwa, kutokana na uharibifu uliokuwa umeanza kujitokeza ni vema serikali ikatenga baadhi ya sehemu za ukanda wa pwani na bahari ili zihifadhiwe kutokana na umuhimu wake kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mapendekezo hayo yaliwezesha maeneo saba ya bahari kutangazwa kuwa ni maeneo tengefu chini ya Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 1970 na Kanuni zake za mwaka 1975. Maeneo hayo ni pamoja na Ghuba ya Chole na Mwamba wa Kitutia (yaliyopo Mafia ambayo kwa sasa ni sehemu ya Hifadhi ya Bahari ya Mafia), Visiwa vya Bongoyo, Mbudya, Pangavini na Fungu Yasini (yaliyopo Dar es Salaam) na Kisiwa cha Maziwe (kilichopo wilayani Pangani katika mkoa wa Tanga).

Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa sasa kinasimamia maeneo 18 ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwenye Bahari ya Hindi yenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 2,000. Maeneo yaliyohifadhiwa kupitia Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu yanajumuisha Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (Mafia) iliyoanzishwa mwaka 1995 (Eneo la kilomita za mraba 822) na Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (Mtwara) iliyoanzishwa mwaka 2000 (Kilomita za mraba 650).

Mengine ni Hifadhi ya Bahari ya Silikanti ya Tanga (Tanga) iliyoanzishwa mwaka 2009 (kilomita za mraba 552) na maeneo Tengefu saba ya Dar es Salaam ambayo ni Visiwa vya Mbudya, Bongoyo, Pangavini na Fungu Yasini (yaliyoanzishwa mwaka 1975). Yapo pia maeneo ya Sinda, Kendwa na Makatube (yaliyoanzishwa mwaka 2007), maeneo tengefu matatu kwenye Kisiwa cha Mafia ambayo ni Visiwa vya Nyororo, Shungimbili na Mbarakuni (yaliyoanzishwa mwaka 2007) na Maeneo Tengefu matano yaliyopo mkoani Tanga yanayojumuisha Visiwa vya Maziwe (iliyoanzishwa mwaka 1975), Ulenge, Kwale, Mwewe na Kirui (yaliyoanzishwa Juni, 2010).

Dk Tamatama anataja baadhi ya majukumu ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kuwa ni kulinda na kuhifadhi maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa bioanuai pamoja na mifumo ikolojia ya baharini na mwambao wa pwani. Mengine ni kuhamasisha wananchi kutumia kwa busara rasilimali ambazo hazitumiki kabisa au hazitumiki kikamilifu kwa sasa; kusimamia maeneo ya bahari na mwambao wa pwani ili kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali (ikiwemo utalii endelevu) na ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa.

Anakwenda mbali na kuyataja mengine kuwa ni kuhakikisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi wanashirikishwa katika nyanja zote za upangaji, uendelezaji na usimamizi wa hifadhi na maeneo tengefu, wananufaika, wanashirikishwa katika manufaa yatokanayo na hifadhi na pia, wanapewa kipaumbele katika matumizi ya rasilimali na fursa za kiuchumi zinazojitokeza. Mengine ni ukuzaji wa elimu ya mazingira na usambazaji wa taarifa kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali kwenye hifadhi za bahari na maeneo tengefu pamoja na na kuwezesha kufanyika kwa tafiti, ufuatiliaji na kutathmini hali ya matumizi ya rasilimali.

Mbali na hayo, pia lipo suala la kuhifadhi na kulinda maeneo ya malikale minara ya kihistoria na rasilimali za kihistoria zilizotambuliwa kuwa na thamani kihistoria na kuhamasisha uendelezaji wa utalii unaozingatia mazingira. Anasema Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ni taasisi ya huduma ya serikali iliyopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayohusika na uhifadhi wa rasilimali za uvuvi na za bahari, mwambao wa pwani na mazingira yake ili kuboresha maisha ya Watanzania kwa jumla.

Taasisi hii inatekeleza Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015; Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997; Sera ya Taifa ya Utalii ya Mwaka 1999; Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002; Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998; na Sera ya Taifa ya Wanyama Pori ya mwaka 2007. Ili kutekeleza sera zilizotajwa awali, Kitengo kinatekeleza Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake, Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Namba 29 ya Mwaka 1994 na Kanuni zake pamoja na Sheria zote zinazosimamia mazingira na maliasiri za taifa.

Aidha, kitengo kina Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kutoka 2014 – 2019, miongozo ya kusimamia hifadhi kama vile Mipango ya Jumla ya Usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, Mwongozo ya Uwekezaji na Mwongozo wa Tathimini ya Athari kwa Aazingira. Kitengo kwa kushirikiana na Wizara na Mradi wa Swiofish kimefanikiwa kukamilisha utengenezaji wa Mpango wa Biashara utakaokuwa dira ya utekelezaji wa mikakati uwekezaji katika maeneo yaliyohifadhiwa na ukusanyaji wa makusanyo wa maduhuli ili kuongeza mapato ya kitengo na serikali.

Mwandishi wa makala haya ni Kaimu Katibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi anapatikana kwajmapepele1@ gmail.com au 0784 44 11 80.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi