loader
Picha

Polisi geukieni elimu kukomesha uhalifu

UAMUZI wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata) wa kuanzisha ziara katika wilaya zote za mkoa huo kwa nia ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili kwa watoto, ni mzuri ambao haunabudi kuwa mfano ili na mikoa mingine iweze kuiga.

Ikumbukwe kwamba Jeshi la Polisi moja ya kazi yake ni kutoa elimu ya kuzuia uhalifu na si kweli kwamba kazi yake kubwa ni kukamata waliofanya uhalifu kwa kuwa jeshi hilo likiweza kufanikiwa kutoa elimu ya kutosha, uhalifu utapungua na kazi ya kukamata wahalifu itakuwa nyepesi pia.

Ipo dhana kwamba polisi kazi yake ni kukamata na pengine kutoa adhabu kali kwa waliofanya au wanaokusudia kufanya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ni kweli kwamba uhalifu ukifanyika, hamna namna nyingine zaidi ya polisi kuingilia kati ili kuwakamata waliotenda uhalifu huo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Lakini kimsingi, kukamata wahalifu haliwezi kuwa fundisho pekee la kumaliza uhalifu nchini. Kubwa zaidi ni kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kwa kuwa wahalifu wako ndani ya jamii husika. Mfano halisi ni mauaji ya watoto mkoani Njombe.

Upo ukweli usiothibitika kwamba unaotokana na dhana ya ushirikina. Hii inamaanisha, kama wahalifu wa mtandao mzima wataelimishwa juu ya madhara makubwa wanayosababisha, kwa kiasi kikubwa itapunguza uhalifu huo na kulinda maisha ya watoto.

Tujifunze kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei ambaye anasema msukumo wa ziara hiyo unatokana na vitendo mbalimbali vya uhalifu vilivyotawala ndani na nje ya mkoa huo ikiwemo mauaji ya watoto yaliyotokea kwa mfululizo hivi karibuni katika mkoa jirani wa Njombe.

Anasema wamekuwa wakipeleka wahalifu mahakamani, lakini haisaidii sana, ni muhimu jamii ikatambua athari zitokanazo na vitendo hivi ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili na watu kujichukulia sheria mikononi.

Haya yote jamii inapaswa ielimishwe ili itoe ushirikiano.

Pia polisi wa usalama barabarani, kazi yao kubwa sio kukamata madereva kwa kufanya makosa bali pia kuwapa elimu ili wasisababishe ajali.

Lakini imekuwa ni kawaida kuona trafiki anajali zaidi kutoa adhabu kali ikiwa ni pamoja na kutoza faini bila hata kumuelimisha mhusika na jinsi ya kukwepa kutenda kosa hilo kwa siku nyingine.

Tunaamini, Jeshi la Polisi lina nafasi kubwa ya kuisaidia jamii isiingie kwenye uhalifu pale ambao litaamua kutoa elimu ya kutosha kabla ya uhalifu, kwa kuwa lina nyenzo za kutosha katika kazi hiyo kutokana na ukweli kwamba linapambana na uhalifu kila kukicha.

Ni vema uamuzi uliofanywa na Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya likaigwa na makamanda wengine kwa kuwa litaleta manufaa kwa jamii ya Watanzania hasa wale wanaoumia na vitendo vya uhalifu vikiwemo vya kuuliwa na watoto na watu wasiojulikana.

Wakati tukiamini Polisi wanao wajibu wa kutekeleza hili kwa nchi nzima, jamii nayo iwe tayari kufuata sheria bila shuruti.

Hii ni muhimu ili kulisaidia jeshi hilo kutotumia nguvu nyingi kiutendaji kwa kuwa jamii ikifuata sheria, uhalifu ama una pungua au unaisha kabisa.

Wote kwa pamoja, tunaweza kuifanya Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani kwa kila mmoja kuishi bila hofu ya kuibiwa, kuuliwa wala kukamatwa na Polisi kwa uhalifu.

TAARIFA ya kwamba idadi ya vifo vya waendeshaji bodaboda kwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi