loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ligi ya Mabingwa hakuna kulala

MCHUANO mkali wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya 16 bora utaendelea tena leo wakati timu nne zitakaposhuka kwenye viwanja tofauti ili kusaka nafasi ya kujiweka katika hatua nzuri ya kucheza robo fainali.

Katika mechi hizo za leo, Liverpool watakuwa na kibarua kigumu wakati watakapoikaribisha Bayern Munich ya Ujerumani, huku Wafaransa Olympique Lyonnais wakiwakaribisha Barcelona katika mchezo mwingine wa michuano hiyo.

Liverpool wenyewe watawakaribisha Wajerumani Bayern Munich katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Anfield, huku ikihitaji kwa nguvu ushindi ili kuvunja matumaini ya Ujerumani kuwa na timu katika hatua ya robo fainali.

Tangu msimu wa mwaka 2005-06, angalau timu moja ya Ujerumani imekuwa na mazoea ya kucheza katika hatua hiyo ya robo fainali inayoshirikisha jumla ya timu nane.

Umwamba huo unaweza kuwa katika tishio endapo Bayern itapokea kichapo kikubwa kutoka kwa Liverpool katika hatua hiyo ya 16 bora katika mchezo huo wa kwanza kabla timu hizo kurudiana Machi 13.

“Huwezi kufanya makosa katika mechi hizi, lakini nafikiri tunaweza kuisababishia Liverpool matatizo”, alisema kiungo wa Bayern Munich, James Rodriguez. “Tuna timu imara inayoweza kufanya vizuri na kupenya, endapo mambo yataenda vizuri.”

Ushindi wa mbinde wa Bayern katika mchezo wa Bundesliga baada ya timu hiyo kutoka nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya timu inayochechemea ya Augsburg, ambako Rodriguez alibadilishwa baada ya kucheza vizuri dakika 56, unaiongezea nguvu timu hiyo ya Ujerumani.

Licha ya kuwa katika hatari ya kushuka daraja, Augsburg ndio timu ya hivi karibuni kabisa katika Bundesliga kudhihirisha udhaifu wa safu ya ulinzi ya Bayern dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza, baada ya kuifunga timu hiyo.

Baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Tottenham Hotspurs, Schalke 04 itawakaribisha mabingwa wa Uingereza Manchester City, huku Bayern ikibeba matumaini ya Ujerumani katika michuano hiyo.

Dortmund ndio wanaoongoza Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga ikiwa juu ya Bayern Munich, lakini kwa Ulaya vijana hao wa Bavarians ndio wenye mazoea ya kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Katika mechi zilizopita za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya 16 bora, Tottenham Hotspurs iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dortmund, huku mabingwa watetezi Real Madrid wakishinda 2-1 dhidi ya Ajax, Paris Saint German wakiiadabisha Man United kwa mabao 2-0 na Roma wakishinda 2-1 dhidi ya Porto ya Ureno.

Michuano hiyo itaendelea tena kesho Jumatano kwa Schalke 04 ya Ujerumani kuwakaribisha mabingwa wa England, Man City huku Atletico de Madrid ya Hispania ikiwa mwenyeji wa Juventus ya Italia katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

OFISA Mtendaji Mkuu wa Liverpool, Peter Moore, anatarajia kuachiwa wadhifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi