loader
Picha

Binti aliyeolewa ISIS ajifungua kambini

MMOJA wa wasichana watatu wa Uingereza waliotoroka kwao miaka minne iliyopita na kwenda kuolewa na wanamgambo wa dola la Kiislamu nchini Syria (ISIS), Shamima Begum (19) amejifungua katika kambi ya wakimbizi nchini Syria.

Shamima ambaye wiki iliyopita akiwa mjamzito alisema anataka kurudi nyumbani akihofia usalama wa mtoto aliyetarajiwa kuzaliwa wakati wowote, amekaririwa katika mahojiano na BBC akiomba msamaha kuwa karibu na kundi hilo la kigaidi lililosababisha maafa katika maeneo mbalimbali.

Februari 2015, Shamima na wenzake; Amira Abase akiwa na umri wa miaka 15 na Kadiza Sultana aliyekuwa na miaka 16 walisafiri kutoka London kwenda Istanbul, Uturuki Februari 17 kisha kuvuka mpaka na kwenda Syria ambako waliolewa na wapiganaji wa kikundi hicho.

Taarifa ya familia iliyochapishwa na BBC kwenye mtandao inasomeka:

“Sisi wanafamilia ya Shamima Begum tumejulishwa kwamba Shamima amejifungua mtoto wa kiume na yeye na mtoto wake wana afya nzuri. Kwa kuwa hatuna mawasiliano ya moja kwa moja na Shamima, tunatarajia kuyatafuta ili tuthibitishe hili”.

Awali, mwanasheria wa familia ya binti huyu, Mohammed Tasnime Akunjee, aliiambia Radio 4 katika kipindi chake cha The World This Weekend kuwa wana furaha kwa kuwa Shamima amejifungua, ana afya njema hivyo wanataka arudi nyumbani.

Alisema familia ilisikitishwa na taarifa juu ya vifo vya watoto wake wawili .

Alisema watoto hao; wa kike mwenye mwaka mmoja na wa kiume mwenye miezi mitatu walifariki dunia kutokana na matatizo yanayohusishwa na utapiamlo na ukosefu wa dawa katika eneo hilo la vita.

Akizungumza na Sky News, Shamima alisema jamii haina budi kumhurumia kwa mambo yote aliyopitia.

Alipoulizwa kama alifanya makosa kusafiri hadi Syria, alisema, “kwa namna moja, ndiyo, lakini sijuti kwa sababu imenibadilisha mimi kama binadamu. Ilinifanya kuwa imara na jasiri. Niliolewa na nisingeweza kupata mtu kama huyu nchini Uingereza,” alisema.

Aliendelea kusema: “Nilipata watoto, nilikuwa na wakati mzuri hapa. Ni kwa sababu tu mambo yamekuwa magumu na siwezi kuvumilia tena.” Gazeti la The Times ndilo lilimuibua Shamima kwa mara ya kwanza kupitia mahojiano yaliyofanyika Februari 13 mwaka huu na kukaririwa akisema ni mjamzito na kwamba watoto wake wawili walifariki.

Mwandishi wa gazeti hili, Anthony Loyd alisema alimgundua katika kambi ya wakimbizi baada ya kusikia lafudhi yake.

Shamima alipoulizwa na Sky News kama alikuwa anafahamu vitendo vya mauaji vilivyokuwa vikiendelea kufanywa na kundi la ISIS, alisema alifahamu mambo hayo yote na hakuwa na tatizo juu ya hayo.

“Kwa sababu nilishakuwa mcha dini kabla ya kuondoka nchini, nilisikia kuwa katika uislamu hayo yanaruhusiwa,” alisema.

Pamoja na Shamima kuomba msamaha kwa mauaji yaliyofanywa yakihusishwa na ISIS ikiwamo tukio la Manchester, lakini alisema anaona ni aina fulani ya kulipiza kisasi kwa kuwa pia kundi hilo la kigaidi lilikuwa linalengwa.

Alijitetea kwamba kipindi chote alichokaa nchini humo alikuwa mama wa nyumbani na hajawahi kutoa usaidizi kwa kundi hilo.

Binti huyo alisema wiki mbili zilizopita, alitoroka kutoka Baghuz; yaliyokuwa makao makuu ya IS, Mashariki mwa Syria. Mumewe, ambaye ni Mholanzi, inasadikiwa kwamba alijisalimisha kwa makundi ya wapiganaji ya serikali.

Tangu wiki iliyopita, kumekuwa na mjadala kuhusu endapo Shamima aruhusiwe au asiruhusiwe kurejea nchini Uingereza.

Miongoni mwa waliohojiwa ni pamoja na wakazi wa eneo la Bethnal Green ambako alikuwa akisoma, ambao baadhi walitaka aruhusiwe kurudi nchini huku wengine wakihoji kama serikali itakubali.

Baba yake Shamima alishutumu maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano akisema wapo vijana wanaokuwa waathirika wa dunia ya kidijitali hivyo mambo mengi yanaweza kutokea.

SERIKALI nchini Canada imeidhinisha kufanyika kwa majaribio ya kwanza ya ...

foto
Mwandishi: LONDON, Uingereza

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi