loader
Picha

Simba haijutii kumsajili Kagere

MOJA kati ya usajili ambao Klabu ya Simba wameufanya mwanzoni mwa msimu huu na ambao hawaujutii kabisa ni ule wa mshambuliaji Meddie Kagere kutoka Klabu ya Gor Mahia ya Kenya.

Klabu nyingi za Tanzania zimekuwa zikisajili wageni, ambao hawana tija kwa klabu zao na kusababisha wapenzi wa soka kuhoji sababu za wachezaji hao kusajiliwa na kulipwa fedha nyingi kuliko wale wazawa, ambao wakati mwingine hufanya kazi kubwa.

USAJILI WA KAGERE

Mchezaji huyo raia wa Rwanda alisajiliwa kwa dau la dola za Marekani 50,000 na mara moja akaja kuanza maisha mapya ndani ya wekundu hao wa Msimbazi.

Huku akiwa na umbo lililojengeka kwa mazoezi na mtindo wake wa kucheza kwa kutumia akili nyingi uwanjani, amekuwa mshambuliaji matata kwani amekuwa akiamua matokeo kwenye mechi ngumu. Hilo limeonekana akilifanya kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika na kufikisha mabao 21 toka alipoanza kukipiga ndani ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

MSAADA KWA TIMU

Hadi sasa mchezaji huyo ameifungia timu hiyo mabao sita kwenye michuano ya ligi ya mabingwa akishikilia nafasi ya pili katika orodha ya ufungaji. Kwenye mchezo dhidi ya Al Alhly uliopigwa Jumanne iliyopita, aliifungia timu yake bao pekee na kuifanya timu hiyo kufufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali. Katika mchezo huo Simba walihitaji zaidi ushindi ili kujiweka katika mazingira ya kufanya vizuri kwenye michezo yao inayokuja na Kagere akafanya hivyo.

Ushindi huo umeisaidia timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo baada ya kufikisha pointi sita wakiwa nyuma ya kinara Al Ahly wakiwa na pointi saba.

MSIMAMO WA KUNDI

Hadi sasa kundi liko wazi kwa kila mmoja kufuzu kwenye hatua inayofuata kama watafanya vyema kwenye mechi mbili zilizobaki. Simba wanahitaji wastani wa pointi nne ili kujihakikishia kutinga robo fainali kwa kuwa wana hazina ya pointi sita mkononi na michezo miwili ikiwemo wa ugenini dhidi ya JS Saoura na ule wa nyumbani dhidi ya AS Vita Club. Mabao sita aliyoyafunga mpaka sasa mshambuliaji huyo Mnyarwanda, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yamemfanya avunje rekodi katika michuano hiyo iliyodumu kwa miaka mitano.

KUVUNJA REKODI

Aidha, Kagere kwa sasa anashika nafasi ya pili katika orodha ya ufungaji wa mabao mengi katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika, akiwa nyuma ya Moataz Al Mahd wa Al Nasr. Kwa kufikisha idadi ya mabao sita kwenye ligi hiyo kumemfanya mchezaji huyo kuvunja rekodi ile iliyowekwa mwaka 2014 na mshambuliaji wa Klabu ya Yanga, Mrisho Ngassa ya kuwa mchezaji pekee wa klabu ya Tanzania kufikisha idadi kubwa ya mabao katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi za klabu, alifikisha mabao sita.

MABAO YA KAGERE

Simba Vs Mbabane Swallows ya eSwatini. Mshambuliaji huyo aliifungia timu hiyo mabao mawili kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Alifunga bao dakika ya 83 ya mchezo huo kwenye mchezo wa pili uliofanyika ugenini nchini eSwatini, Kagere alirejea tena kambani dakika ya 62 kwa kiki kali kutoka nje ya eneo la hatari.

Simba Vs Nkana FC Ya Zambia

Kwa mara nyingine mshambuliaji huyo aliifungia tena timu yake bao kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika katika Uwanja wa Taifa kwenye dakika ya 45 kipindi cha kwanza baada ya mchezo wa awali uliopigwa Kitwe Zambia timu hiyo kupoteza kwa mabao 2-1

Simba v JS Saoura ya Algeria

Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao ya 3-0. Katika mchezo huo mabao ya Simba yalianza kupatikana kipindi cha pili, ambapo Kagere aliifungia timu yake mabao mawili dakika ya 51 na 66 na kuifanya timu yake kuibuka na ushindi huo mnono. Mchezo huo ulikuwa wa awali kwenye hatua ya makundi mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Taifa, ambapo Simba walibuka na ushindi wa idadi ya mabao hayo.

Simba v Al Ahly ya Misri

Mchezo huo ulikuwa wa raundi ya nne katika hatua ya makundi ulikuwa mchezo mgumu kwao kutokana na kutoka kupoteza michezo miwili mfululizo wakianza na As Vital kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mabao 5-0 kabla hawajafungwa tena idadi kama hiyo na Al Ahly. Kagere alifungia tena timu yake bao la ushindi dakika ya 65 baada ya kumchambua mlinda mlango wa wapinzani wao hao na kuachia kiki kali na Simba kufufua matumaini ya kusonga mbele.

Pamoja na kuonesha mchango mkubwa kwenye ligi hiyo ya mabingwa, mshambuliaji huyo ameonesha mchango mkubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa upachikaji wa mabao kwani hadi sasa anaongoza kuifungia timu hiyo mabao hadi sasa amefikisha idadi ya mabao tisa. Na kumfanya kuwa kinara wa upachikaji mabao kwenye timu hiyo na kuendelea kuzungumzwa na mashabiki wa timu hiyo wakiamini anafanya kazi yake vile inavyotakiwa. Kagere amegeuka kuwa lulu kwenye kikosi hicho baada ya kufunga bao kwenye mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga ni moja ya mechi inayotawaliwa na hisia kali kutokana na historia zilizojibebea toka kuanzishwa kwa timu hizo miaka kenda huko nyuma.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi