loader
Picha

Agizo la Majaliwa liguse mipaka yote

HALI ya usalama katika mpaka wa Holili baina ya Tanzania na Kenya imeelezwa kuwa haiko sawa kiasi cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza kutoridhishwa kwake na hali hiyo alipotembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki.

Kutokana na hali hiyo ya kutoridhisha, Waziri Mkuu Majaliwa akasisitiza vyombo vya usalama vya Tanzania na Kenya kujipanga upya katika mpaka huo ili kudhibti uingiaji holela wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani wakiwemo wa nchi za jirani pamoja bidhaa za magendo.

Tunapenda kuunga mkono agizo la Waziri Mkuu katika mpaka wa Holili lakini pia tunavisihi pia vyombo vya usalama katika mipaka mingine inayozunguka nchi yetu vichukulie agizo hili kama linawahusu ili kila eneo la mipaka ya nchi hii liwe salama.

Tunasema hivyo kwa sababu, mbali na kujivunia amani, upendo na usalama wa nchi yetu, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba nchi yetu inazungukwa na baadhi ya nchi jirani ambazo usalama ndani mwa nchi hizo ni tete, hivyo kutokuwa makini, baadhi ya makundi yanaweza kutumia nafasi hiyo kujipanga ama kushambulia nchi zao kutokea ndani ya nchi yetu au pia kuleta madhara ndani ya nchi yetu.

Tumeshuhudia misitu iliyoko katika mikoa ya Kigoma na Kagera ambavyo imekuwa ikisumbua kuwa na wahalifu wa kila namna kutoka nchi za jirani ambapo wapo Watanzania wamepoteza maisha na mali au viungo vyao vya mwili kutokana na kuvamiwa na vikundi vilivyokuwa vikijificha katika misitu hiyo hadi vyombo vya usalama vilipoimarisha ulinzi.

Tunaamini, agizo la Waziri Mkuu mbali na kutakiwa kutekelezwa katika eneo la mpaka wa Holili, lakini pia litachukuliwa kwa uzito mpana katika maeneo mengine ya mipaka yote ili kulinda usalama wa nchi na wananchi wake.

Akizungumza na vyombo vya usalama na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wake, Waziri Mkuu alisema anazo taarifa kwamba mpaka huo huingizwa baadhi ya bidhaa na watu ambao huingia kwa njia tofauti, jambo ambalo alisema linakuwa tishio la kiusalama.

Akasema lazima majeshi yetu kwa nchi za Tanzania na Kenya kwa kushirikiana na idara ya Uhamiaji wakajiridhisha kuhusu utendaji wao na kuanzisha mfumo wa pamoja wa kiusalama ili kuhakikisha hakuna mtu anayeingia Kenya ama Tanzania na kufanya uhalifu wa aina yoyote.

Pia akataka kitengo kinachohusika na ukaguzi na mizigo na vifurushi katika mpaka wa Holili kuwa waadilifu na wenye kutumia teknolojia kubaini bidhaa na silaha ambazo zingeweza kupitishwa kwa ujanja ujanja katika mpaka huo na kwenda kuleta athari Tanzania au Kenya.

TAARIFA ya kwamba idadi ya vifo vya waendeshaji bodaboda kwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi