loader
Picha

‘Nilitikisa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa Hesabu’

“NILITIKISA Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye somo la Hesabu … Bado wananiheshimu mpaka leo.” Ndivyo anavyosema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anapozungumzia siri ya mafanikio yake kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana wenye vipaji maalumu ya Kilakala.

Maelezo hayo ya Profesa Ndalichako yanatokana na mwanafunzi Tabashamu Mtogo wa Kidato cha Pili aliyemuuliza swali lililolenga kujua siri ya mafanikio yake hadi kuweza kufikia nafasi ya kuwa waziri.

“Kuna mwanafunzi mwenzenu nimekutana naye baada ya kunisalimia akaniuliza swali, anataka kujua siri ya mafanikio yangu kwani imekuwaje hadi nimefikia hapa; nimekuwa waziri,” anabainisha Profesa Ndalichako. “Mnatamani na nyie siku moja mfike kama hapa nilipo, ngoja niwatie moyo … Penye nia pana nini; …pana njia, ndiyo tunaanza hivyo,” anawaambia wanafunzi hao na kuwafafanulia kuwa, kwanza kabisa alikuwa na nia na malengo yake aliyolazimika kuyawekea mipango na kuisimamia kufikia malengo yake.

Anasema: “Jambo la kwanza, ni mwanafunzi kuwa na bidii katika kuzingatia masomo; kwa lugha ya siku hizi vijana mnasema, kama ni kitabu ukomae kweli kweli.” Waziri Ndalichako anawataka wanafunzi hao na wengine walio katika shule mbalimbali kutokubali kudanganyika na kujidanganya kuwa wana akili za kuzaliwa, na hivyo kubweteka. “Hakuna kitu kama hicho, unakuwa na akili ya kuzaliwa sawa, lakini akili hiyo lazima iendelezwe kwa kusoma kwa bidii,” anasema Ndalichako.

Anaongeza: “Na hata ukisoma sana kuna kosa gani; msione aibu kusoma sana, kuna shida gani wakati umekuja hapa kusoma? Msione aibu; someni kwa bidii kabisa..” Anapobainisha siri ya masomo yake, Profesa Ndalichako anasema kutokana na kuweka kwake bidii katika masomo yote tangu awali, akiwa sekondari baadhi ya wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania wakisema eti ametumwa na kijiji, jambo analosisitiza kuwa, alilipuuza na kuongeza bidii.

Anaeleza kuwa, siri ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii na nidhamu kwa kila jambo, na kwamba hata baada ya kujiunga na Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), aliendeleza utamaduni kiasi kwamba, katika maktaba ya chuo kikuu hicho, alikuwa na muda maalum wakati wa kujisomea. Kwa mujibu wa Ndalichako, katika mwaka wa kwanza wa masomo chuoni hapo masomo yote ya hesabu alipata daraja la kwanza (A), hali iliyowashangaza wanafunzi wenzake hasa wanaume. “Walikuwa wakiulizana kuwa huyu ni mwanamke; amewezaje wakati Hesabu ni somo la kiume?” anasema.

Anasema katika somo la Hesabu, alikuwa zaidi ya mwanaume na walikuwa wakimwogopa na hakuna mwanaume aliyekuwa akimpata kiasi kwamba, mpaka sasa wanamheshimu. “Pale Maktaba ya Chuo Kikuu nilikuwa na kiti changu maalumu, nikisoma naenda kula na ninaacha vitabu vyangu na nikirudi naendelea kusoma,” anasema na kuongeza:“ Katika kusoma, kwa kweli siwadanganyi kama ni siri, basi siri yangu ilikuwa katika kusoma kwa bidii na nidhamu…” Profesa Ndalichako anasema aliendelea kusoma kwa bidii na kwamba katika kipindi cha mitihani, aliweza kusoma hadi saa tisa usiku.

“Nilikuwa nasoma hadi nafikia hatua naanza kujiuliza, hivi mwalimu atauliza kitu gani kitakachonishinda na hii ilijidhihirisha mwaka wangu wa kwanza chuoni, ambapo masomo yote hesabu nilipata A,” anasema. Anasema kutokana na juhudi za kusoma alimaliza masomo ya shahada ya kwanza na kupata daraja la kwanza. “Nilibakia chuoni hapo upande wa elimu na kutokana na kufanya kwangu vizuri, nilitafutiwa ufadhili wa kwenda kusoma nje ya nchi kwa shahada ya pili na ya tatu nchini Canada,” anafahamisha.

Kulingana na historia yake, Profesa Ndalichako alipata elimu ya sekondari katika shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora na kufaulu kwa daraja la kwanza. Kisha alichaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule hiyo akisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM ); akafaulu vizuri. Mwaka 1987 alijiunga na UDSM na kumaliza mwaka 1991 kwa kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Sayansi na Elimu katika Hisabati. Mwaka 1993 hadi 1997 alikuwa katika Chuo Kikuu ya Alberta nchini Canada akisomea Shahada ya Uzamili na kuendelea na Shahada ya Uzamivu (PhD).

Baada ya kuhitimu PhD alirejea nchini na kuwa mhadhiri mwandamizi katika UDSM akifundisha elimu ya upimaji na tathmini, mbinu za utafiti na takwimu za elimu, pamoja na kusimamia utafiti wa wanafunzi. Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, akiwa nchini Canada, alisoma kwa bidii zaidi kuliko alipokuwa UDSM na hivyo, kufanya vizuri zaidi katika masomo yake hadi alipohitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu na kurudi nyumbani.

“Nikiwa naendelea kufundisha UDSM, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliniteua na kunipa moja ya vitengo nyeti katika Baraza la Mitihani na baadaye, Rais John Magufuli kuniteua kuwa waziri mwaka 2015. Anawasihi wanafunzi wa kike nchini kuzingatia kuwa nidhamu, juhudi katika masomo na kumtanguliza Mungu ili wayafikie malengo yao.

“Mimi nimepitia magumu mengi, na hata nikiwa Baraza la Mitihani nilipitia magumu, lakini nilimtanguliza Mungu akanisaidia nikavuka…” anasema. Kesho ni Siku ya Wanawake Duniani ikiwa na kaulimbiu ya kitaifa ya Mwaka 2019 isemayo: “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”.

 

 

Katika mwendelezo wa makala haya kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila Machi 8, kesho tutakuwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi