loader
Picha

Watanzania tupambane kulinda faru

TAARIFA kwamba taasisi isiyo ya kiserikali ya Grumeti inatarajia kuingiza faru 10 hapa nchini, hivyo kufanya idadi ya faru waliongizwa na taasisi hiyo kufi kia 12 inafurahisha, ikizingatiwa umuhimu wa wanyama hao katika sekta ya utalii.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof Adolf Mkenda pamoja na kwamba inaleta tumaini jipya katika hifadhi zetu hapa nchini, inadhihirisha uaminifu tulionao katika dunia wa utunzaji wa wanyama.

Pamoja na kuwashukuru wadau hao kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii hapa nchini, kitendo chao wao kuongeza faru kinapaswa kupongezwa na watanzania wote wanaopenda maendeleo, kwa kuhakikisha kwamba hawauawi na majangili.

Sote tunajua kwamba miongoni mwa wanyama wakubwa watano wanaofuatiliwa na watalii hapa nchini, faru ni mmojawapo na hivyo kuongezwa kwa idadi yao kunaweza kukuza idadi ya faru hapa nchini.

Tunapaswa kutambua kwamba faru wanaoletwa nchini ambao ni sehemu ya aina ya faru wanaotambuliwa kama faru weusi ndio walio hatarini kutoweka japo ni wenyeji wa mashariki na Kusini mwa Afrika katika nchi za Botswana, Kenya, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Ingawa wanaitwa faru weusi kitaalamu, faru hawa ambao huwa na rangi tofauti kuanzia hudhurungi hadi kijivu; tunapopokea faru hawa tunapaswa kuangalia umuhimu wao kwetu na kuwatunza.

Hii inatokana na ukweli kuwa wanyama hawa duniani wamekuwa wakitoweka kwani katika karne ya 20 kwa mujibu wa taarifa za kitafiti, faru weusi walikuwa wengi wa kutosha.

Lakini tunaambiwa kuwa katika nusu ya mwisho ya karne hiyo walibaki 70,000; wakati katika miaka ya 1960 inakadiriwa walikuwa 10,000 na mwaka 1981 idadi yao ilifikia 15,000.

Mapema kwenye miaka 1990 idadi iliporomoka kuwa chini 2,500, na mwaka 2004 ilielezwa kuwa walikuwa faru 2,410. Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya faru (International Rhino Foundation) idadi ya faru weusi iliongezeka kufikia 4,240 ilipofika mwaka 2008 .

Hapa nchini kwetu Mhifadhi wa Ngorongoro (NCA) Freddy Manongi anasema mwaka jana idadi ya faru ilikuwa imeongezeka na kuwa zaidi ya 50 katika hifadhi hiyo, hivyo kuja kwa faru hao kutasaidia kuongeza idadi zaidi katika mbuga nyingine.

Kama tulivyopambana kuongeza idadi ya faru, Hifadhi ya Ngorongoro kutoka 25 waliokuwapo mwaka 1977 kufikia 50 ,basi wananchi nao watoe ushirikiano kuhakikisha kwamba faru hao wanaokuja wanalindwa na kuzaliana pia.

Tutambue kwamba wenzetu wa Cameroon ambao mwaka 2002 walikuwa na faru 10 lakini walipotafutwa tena mwaka 2006 hawakuonekana tena, hivyo si sawa kama watanzania wote hawatashiriki kuhakikisha usalama wa faru hao kwa manufaa yetu na dunia kwa ujumla.

Tunatambua kwamba kutoweka kwao si kwa bahati mbaya kwani wapo watu waliojiaminisha kuhusu pembe zake, hivyo hata wanapoletwa nchini mfumo wa ulinzi ni lazima uimarishwe na wananchi wawe wazalendo kwa kutoa taarifa za siri kuhusu ujangili na hasa wa faru.

Kwa kufanya hayo tutaweza kuwapa nafasi faru wetu waongezeke na kuishi kwa amani wakitupatia heshima duniani ya kuwa watunzaji wazuri, hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaotaka kuona mandhari zetu na wanyama wetu.

TAARIFA ya kwamba idadi ya vifo vya waendeshaji bodaboda kwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi