loader
Picha

Lindi tajiri madini ya ndege, nakshi za majengo

WAKATI baadhi ya watu wakielekeza nguvu katika mikoa mingine ya Tanzania ikiwemo Arusha, Shinyanga na Mara kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya madini, Lindi huwa haikumbukwi licha ya ukweli kuwa ni miongoni mwa sehemu zinazopatikana rasilimali hiyo inayopatikana ardhini.

Mkoa huo kwa sasa unafahamika zaidi kuingiza pato lake kupitia kilimo hususani cha mazao ya korosho na ufuta huku sekta ya madini ikichangia chini ya asilimia moja tu ya pato kwa baadhi ya wilaya zilizopo mkoani Lindi.

Hata hivyo, hali hiyo inasababishwa na kutokuwepo kwa taarifa za kutosha kwa wawekezaji juu ya upatikanaji wa madini ya aina mbalimbali katika mkoa huo wa Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi anabainisha kuwa Lindi, kwa sasa, ni mkoa unaokuja kasi si tu kwa ugunduzi bali pia kwa upatikanaji wa madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, grafaiti (graphite), vito, madini ya jasi na hata madini ya mabo (marble).

Akizungumzia maandalizi ya jukwaa la fursa za biashara na uwekezaji mkoani Lindi linalotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 25 hadi 27, mwaka huu na kufunguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, RC Zambi anasema mkoa huo “umebarikiwa na Mungu” kwa kuwa na madini mengi ya kila aina.

Anaeleza kuwa kutokana na baraka hizo, yapo maeneo ambayo kwa sasa yako katika uangalizi maalumu baada ya kugundulika kuwa na madini ya dhahabu ambayo tofauti na maeneo mengine yanachimbwa tena kwa kutumia zana za kisasa lakini kwa katika baadhi ya maeneo, madini yanaokotwa tu juu ya ardhi.

Aidha, anabainisha kuwa pamoja na madini hayo ya kuokotwa juu juu, maeneo ya Wilaya za Lindi Vijijini, Ruangwa na kidogo Nachingwea yamebainika madini aina ya grafaiti yanayotumika kutengeneza betri za simu, kalamu na injini za ndege.

“Tayari kuna kampuni mbili zimeonyesha interest (nia) ya kujenga migodi wilayani Ruangwa. Pia kuna kampuni zinafanya utafiti wa madini Lindi vijijini,” anasema.

Zambi anataja madini mengine yanayopatikana kwa wingi Lindi kuwa ni chokaa, makaa ya mawe ambayo yamebainishwa kuwa bora kuliko yanayotoka sehemu zingine na nikeli.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa, anasema katika wilaya hiyo ndiko yanakopatikana kwa wingi madini ya grafaiti ambapo mwaka huu pekee, tayari maeneo sita yameshafanyiwa utafiti na kazi iliyosalia ni ujenzi wa wa migodi.

Anasema wilaya hiyo inatarajia kuwepo kwa uwekezaji na biashara ya kutosha katika eneo hilo la madini ya grafaiti kutokana na matumizi yake katika mambo muhimu kama vile betri za simu na kalamu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, Geofrey Nnauye anabainisha kuwa wilaya hiyo pia imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali ambapo tayari utafiti wa madini unaendelea katika maeneo ya Mpinduka, Himba, Nditi na Makakoyi.

Alitaja madini yanayopatikana kwa wingi kuwa ni dhahabu na nikeli ambayo kwa sasa yamekuwa na ongezeko la mahitaji duniani hususani nchi zenye viwanda. Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Madini, madini ya nikeli yana matumizi makubwa ikiwemo kutengeneza betri za simu na kutengenezea pesa za fedha (silver-coins).

Nikeli pia hutumika katika glasi kuipa rangi ya kijani; aidha hutumika kama kichochezi cha kuhifadhi mafuta ya mimea na katika mitambo ya kielektroniki pamoja na kulinda vifaa mbalimbali vya chuma visipate kutu ikiwa ni pamoja na kutumika katika vifaa mbalimbali vya umeme kama vile nyaya.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga anasema halmashauri yake inaongoza kwa kuwa ndiko kwenye madini ya dhahabu ambayo “hayachimbwi bali yanaokotwa tu.”

Aidha, anasema pamoja na madini ya dhahabu pia wana madini ya grafaiti, makaa ya mawe na chumvi na wanachosisitiza kwa sasa ni uwekezaji zaidi katika maeneo hayo na viwanda ikiwemo viwanda vya chumvi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai anasema wilaya hiyo imebarikiwa kuwa na madini mengi lakinimadini ya jasi ndio yanayopatikana kwa wingi hasa katika maeneo ya vijiji vinne vya Nanjilinji, Hoteli Tatu, Kirangerange na Makangaga.

Anasema madini ya jasi yaliyopo wilayani humo yanaweza kutumiwa hadi miaka 1,000 ijayo.

“Gypsum inayotoka Kilwa ina ubora wa hali ya juu kuliko inayotoka maeneo mengine. Kama tungeweza kuwa na uwekezaji mkubwa kwa kuiprocess (kuichakata) kama raw material (malighafi) ingekuwa na faida kubwa,” anaeleza Ngubiagai.

Anasema madini hayo ya jasi kwa sasa ni muhimu kwa kuwa huwezi kutengeneza saruji bila kuwa na gypsum lakini pia yanatumika kuweka nakshi katika dari la nyumba.

“Kupitia jukwaa hili la fursa za biashara na uwekezaji, hii ni fursa kwetu Kilwa, kukaribisha wawekezaji na wafanyabiashara katika eneo hili la madini,” anasisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Anaeleza kuwa pamoja na madini hayo ya jasi, Kilwa ina madini ya gesi eneo la Songosongo ambayo kwa sasa yanazalisha asilimia 25 ya umeme. Takribani asilimia 30 ya umeme unaozalishwa Lindi ni umeme wa gesi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, taifa lina akiba ya gesi asilia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 iliyoko kwenye visima mbalimbali vinavyotumika na visivyotumika.

Kisiwa cha Songosongo kilichopo Kilwa mkoani Lindi na Mnazi Bay iliyopo Mtwara ni miongoni mwa maeneo kunakopatikana gesi hiyo. Teknolojia ya kisasa ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ilianzia kisiwa cha Songosongo.

Aidha, Ngubuagai anafafanua kuwa Kilwa pia inazalisha madini ya chumvi yanayosafirishwa kwenda nchi jirani za Rwanda, Uganda na Congo na kuongeza:

“Jambo linalotakiwa ni kuhamasisha ujenzi wa viwanda ili iongezewe thamani kwa kuifunga vizuri na kisasa.” Tryphone Rwegasira ni miongoni mwa mmoja wa wachimbaji wadogowadogo katika kijiji cha Makangaga, wilayani Kilwa.

Anabainisha kuwa kuwa ukanda huo wa madini katika kijiji hicho na sehemu nyingine una kiwango kikubwa cha madini ya jasi (gypsum) ambacho hakiwezi kumalizwa na kizazi cha sasa pekee.

Kwa mujibu wa mchimbaji huyo, uzalishaji wa madini katika eneo hilo ni mkubwa kwani kuna takribani migodi ya jasi 22 yenye wachimbaji wakubwa nane na wadogomajengo20.

“Huku changamoto tuliyonao ni barabara tu, kwani kipindi cha msimu wa mvua migodi hulazimika kufungwa kwa kuwa barabara hazipitiki. Lakini pia soko mpaka tulifuate barabarani ingawa kwa kweli lipo,” anasema.

Anasema madini hayo ya jasi pindi wanapoyazalisha husafirisha kwa malori hadi barabara kuu umbali wa takribani kilometa 50 mpaka 64 na gharama za uzalishaji hufikia hadi Sh 15,000 hadi 20,000 hadi barabarani ambako wanapoyauza viwanda huuza mpaka Sh 100,000 kwa tani lakini barabarani huuza kwa Sh 40,000 kwa tani.

“Hatunufaiki sana kwa kweli kwa sababu tunatumia gharama kubwa kuyachimba madini haya. Kwanza hatuna vifaa vya kisasa, tunatumia milipuko. Tunaomba serikali itupangie bei elekezi tuliyoomba ya Sh 60,000 kwa tani ili nasi tunufauke,” anasisitiza.

Mwenyekiti Mtendaji wa kijiji cha Makangaga, Said Njenga anaeleza kuwa madini hayo yana faida kubwa kwa serikali ya kijiji kwani kwa mwaka huingiza mpaka Sh milioni 100 zinazotumika kwa shughuli za maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sara Chiwamba anasema, katika wilaya hiyo, kuna madini mengi yakiwemo ya marble ambayo uwekezaji wake bado ni mdogo. Madini ya marbe hutumika kutengenezea vito vya thamani ikiwemo nakshi za nyumba na tiles za kisasa.

Ofisa Mazingira wilaya ya Liwale, Aziz Mshamu anabainisha kuwa katika wilaya hiyo, madini ya marbe ni mengi na yanachimbwa kwa kufuata mkondo ila changamoto ni vifaa vya uchimbaji na uwekezaji mdogo lakini yana soko kubwa katika nchi ya Italia.

Kupitia Jukwaa hilo la uwekezaji, fursa hiyo ya madini ikitangazwa vyema na kuvutia uwekezaji ni wazi kuwa Lindi itaungana na mikoa mingine mashuhuri nchini kwa uchimbaji wa madini na mchango wa madini hayo katika pato la mkoa huo utaongezeka.

Mawasiliano Tanzania Standard Newspapers Ltd, Daily News Building, Plot No. 11/4 Mandela Express Way.

Po. Box 9033, Dar es Salaam. Simu: +255 286 4862; 0712 516 169; 0655 332 866.

Baruapepe: info@tsn.go.tz advertising@dailynews.co.tz. Website: www.tsn.co.tz; www.dailynews.co.tz.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Lindi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi