loader
Picha

Sababu Siku ya Pai kuadhimishwa Machi 14

MACHI 14 kila mwaka, ni Siku ya Pai ambayo sasa inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Hisabati. Wanaofuatilia maandiko yangu au kuniangalia kwenye televisheni au kunisikiliza kwenye redio nikielezea hiyo siku, watakuwa wameshaelewa dhana yenyewe.

Mwaka huu sherehe za Siku ya Kimataifa ya Hisabati zinatimiza miaka 15 tangu zianzishwe nchini Tanzania. Sherehe hizi kwa mara ya kwanza zilifanyika hapa nchini mwaka 2004. Kwa wale ambao jambo hili ni jipya ni kwamba, wataalamu walipendekeza siku hiyo kutokana na thamani ya pai kukadiriwa kuwa 3.14 katika nafasi mbili za desimali.

Tatu (3) inawakilisha Mwezi wa Tatu yaani Machi; na 14 inawakilisha siku yenyewe. Fasili ya pai ni mzingo wa duara gawanya kwa kipenyo chake au mduara gawanya kwa kipenyo. Mduara ni umbali wa mzunguko mmoja wa duara. Fasili hiyo ya pai huweza ku- ongeze- wa nakshi kwa kuimba ule wimbo maarufu wa ‘Maua mazuri yapendeza’.

Tunauongezea ubeti: Zum-zum, nyuki lia we x2 Ukitaka kutafuta thamani ya pai Gawanya mzingo kwa kipenyo chake x10. Baadhi yenu mlielezwa kuwa pai ni 22 gawanya kwa 7. Ni vizuri kujua kwamba, hili ni kadirio tu la pai kwa kutumia sehemu.

Kadirio bora zaidi hupatikana kwa desimali. Hii ni kwa sababu ukigawanya mzingo wa duara kwa kipenyo chake, ni rahisi zaidi kuandika hisa hiyo kwa desimali kuliko kwa sehemu. Hii huwezesha pia thamani hiyo kutafutwa kwa nafasi nyingi za desimali.

Ni nadra kupima mzingo wa duara ukawa kipimo cha urefu 22 na wakati huohuo kipenyo kuwa 7. Hiyo inafanyika kwa kukusudia au kwa kupanga. Tukitoka nje na kuitazama Siku ya Wapendao (Valentine Day) inayosherehekewa Februari 14, mwezi mmoja kabla ya Siku ya Hisabati, tunaonana hiyo ni siku maarufu sana na ina mbwembwe nyingi huku ikigusa jamii zote ndiyo maana siku hizi, hata baadhi ya madhehebu ya dini yameikubali kwa kuwa inakutanisha watu ili kuendeleza upendo.

Vyombo vya habari navyo vimekuwa mstari wa mbele kuitangaza na kuandaa programu. Siku ya Wapendanao ilianza taratibu na hatimaye kufikia kiwango cha juu cha sasa. Uchunguzi na uzoefu unaonesha ni matamanio ya wengi pia, Siku ya Pai nayo ifuate mkumbo huo. Kwanza watu waijue, waone umuhimu wake na kisha waienzi. Baadhi ya watu wamekuwa wakiishuhudia kwa miaka 15 tangu ianzishwe nchini mwaka 2004, lakini bado haijawapa ule msisimko wanaohitaji.

Ni vyema basi kuikazania siku hii kwa wadau kuunga mkono jitihada za kuiboresha ili walau kwa kiwango fulani, itambulike, ifanane na ‘kuchangamkiwa’ kama ilivyo Siku ya Wapendanao. Baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwanini kuwe na Siku ya Pai, wakichukulia kwamba, kuna namba nyingine ambazo zingefaa pia kupewa siku. Ukweli ni kwamba, hakuna namba ambayo imesisimua, imewasumbua na imewaacha hoi wanahisabati kama pai.

Hii ni namba inayohusiana na duara zilizo katika maisha ya kila siku. Inahusika katika kutafuta mizingo na maeneo ya violwa mbalimbali. Kadhalika, pai hujikuta ikihusianishwa na nyuzi katika jometri kwa mfano, nyuzi 180 ni pai. Siku ya Pai pia ni siku ya kuzaliwa kwa mwanasayansi mkongwe, Albert Einstein. Hii ni siku ambayo baadhi yetu tunakumbuka siku yetu ya kuzaliwa au siku tuliyofanya jambo la kukumbuka.

Kwa mfano, mjukuu wangu alizaliwa usiku wa kumkia siku ya pai na tumempa jina la utani la “Bi Pai”. Kwa vyovyote, unaweza kutafuta mwenyewe namna ya kuikumbuka siku hiyo ili uungane na sehemu nyingine duniani kuienzi.

Hata hivyo, kuna baadhi ya alama za Hisabati na Sayansi zilizokwishashatengewa siku. Kwa mfano, Februari 27, ni siku ya ‘e’ inayotokana na mgunduzi wake Euler ambapo thamani yake inakadiriwa kuwa 2.27. Oktoba 23 imetengwa kwa ajili ya namba iitwayo Avogadro ambayo thamani yake iko kwenye kiwango cha 10 kipeo cha 23. Siku hizo bado hazijajengewa umaarufu wa kutosha kwa kuwa dhana zake ziko katika elimu ya juu.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu wanafunzi wengi kufanya vibaya katika mitihani ya Hisabati katika ngazi zote za elimu. Inatarajiwa kwamba, siku kama hii inaweza kuwakutanisha wadau mbalimbali kutafuta mikakati ya kupambana na tatizo hilo. Chama cha Hisabati Tanzania (MAT / Chahita) kinajizatiti kuifanya siku hiyo iwe na matukio ya kuendeleza juhudi zake za kuinua kiwango cha ufanisi wa Hisabati hapa nchini. Inashauriwa kila shule au chuo kutenga muda fulani katika ratiba ya siku hiyo kufanya shughuli za Hisabati. Siku ya Pai huwa na matukio mbalimbali.

Tukio la kwanza huwa ni matembezi ya hisani yanayoambatana na kikundi cha tarumbeta kinachoongoza nyimbo za kuhamasisha Hisabati. Kwa mfano, “iela iela, iela iela, iela iela, hisabati nambari wani.” Matembezi hayo hufanyika barabarani na kuongozwa na askari wa usalama barabarani wanaohakikisha magari yanatoa fursa kwa washiriki kutoa ujumbe wao.

Yanakuwepo mabango yaliyoandikwa kwa unadhifu kuwapa raha wapita njia na walioko kwenye magari huku wakitafakari matatizo ya Somo la Hisabati. Matembezi hayo hupokewa na mgeni rasmi wa sherehe ambaye hupitishwa kwenye maonesho mbalimbali yanayoelezea dhana kadhaa za Hisabati, michezo na mbinu za kukokotoa. Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali hupewa fursa za kutoa salamu zao na jinsi wanavyoitumia pai katika maeneo yao.

Nyimbo za kusisimua kuhusu pai huimbwa na hatimaye mgeni rasmi hukaribishwa kutoa nasaha zake. Sherehe hiyo hufikia kilele chake saa 7:59 ambayo kwa mtindo wa Kiingereza, huandikwa 1:59 ambayo ni Saa Saba na Dakika 59. Hii inatokana na pai kukadiriwa kuwa 3.14159 kwa nafasi tano za desimali. Umeshaelezwa kuwa nafasi tatu za mwanzo ni za mwezi na siku ya pai. Tarakimu ya nne ni saa kwa mtindo wa kiingereza (1pm) na tarakimu mbili zinazofuata ni za dakika.

Kwa hiyo inapofika saa saba dakika 59 ambayo huitwa Saa ya Pai (pi hour), huimbwa wimbo wa kuipongeza kwa Kiingereza kwa sauti iliyozoeleka: Happy pi day to you Happy pi day to you Happy pi day every body Happy pi day to you Tukio hilo huambatana na kujipongeza kwa kuithamini pai. Wengine hushikana mabega ambayo ni ishara ya kimataifa ya kuthamini siku ya pai. Wengine hugongeshana glasi zao za kinywaji. Bado tunakumbuka mwaka 2009 sherehe hiyo ilipofanyika Taassi ya Elimu Tannzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli alikuwa mgeni rasmi wakati huo akiwa Waziri wa Uvuvi. Katika hotuba yake, aliunga mkono MAT / Chaita na wote wanaoendeleza Somo la Hisabati na kumpongeza mwanzishaji wa Siku ya Pai Tanzania. Mwaka 2012, Shereke za Siku ya Pai kitaifa zilifanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani jijini Dar es Salam.

Matembezi yalianzia Shule ya Sekondari Tambaza na kuelekea Shule ya Sekondari Jangwani ambapo yalipokelewa na mgeni rasmi, Majaliwa Kassimu Majaliwa. Majaliwa ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwatakia watu wote kupenda Hisabati ili tufanikishe malengo yetu. Maadhimisho ya Siku ya Pai nchini mwaka huu (Machi 14), yanafanyika Kijitonyama katika Kitengo cha ICT cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Mwandishi wa makala haya ni Profesa mstaafu wa Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa: sekabeniel@ yahoo.com.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Beniel Seka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi