loader
Picha

Aliyebambikizwa kesi ya mauaji aokolewa na JPM

RAIS John Magufuli amemuokoa mkazi wa Tabora, Musa Adam Sadiki aliyebambikiziwa kesi ya mauaji na polisi na kuwa baada ya kukamatwa, alinyang’anywa Sh 788,000, simu ya mkononi na mali nyinginezo.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alipozungumza na vyombo vya habari jijini hapa jana. DPP alithibitisha kwamba Sadiki alibambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika Mahakama ya Tabora. Alisema baada ya kufuatilia na kubaini ukweli huo, Machi 8, mwaka huu, aliwafutia Mashtaka Sadiki na Edward Matiku (Nduli) na Mahakama ya Tabora Mjini ikawaachia huru.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa, Mganga alisema ofisi ya Taifa ya Mashtaka imebaini kuwa malalamiko ya Sadiki ni ya kweli baada ya Rais kusoma barua ya wasomaji katika gazeti la Majira la Machi 6, mwaka huu. Mganga alisema Rais baada ya kusoma barua hiyo kwenye magazeti la Majira, aliagiza ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya Sadiki kwa haraka ili kujua ukweli.

“Katika kufuatilia malalamiko hayo, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imebaini kuwa malalamiko hayo ni ya kweli,” alisema. Tukio linaonesha kwamba Sadiki aliandika barua ya wazi kwa Rais katika gazeti la Majira la Machi 6, mwaka huu akilalamika amebambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika mahakama ya Tabora na kuwa baada ya kukamatwa, askari polisi walimnyang’anya Sh 788,000, simu ya mkononi na mali alizokuwa amenunua kwa ajili ya wakulima.

Sadiki baada ya kukamatwa aliwekwa kwenye Kituo cha Polisi Tabora Mjini kwa kubambikiziwa kesi ya kuvunja na kuiba na alikaa kituoni kwa wiki moja alipopelekwa mahakamani alisomewa mashtaka ya mauaji. Baada ya maagizo ya Rais, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilifuatilia mashtaka na kufanya mahojiano na kusoma hadidu za rejea nyaraka zilizipo katika kituo cha Polisi cha Tabora Mjini.

Ofisi hiyo ilibaini kuwa malalamiko hayo ni ya kweli kutokana na kitabu cha kuzuia uhalifu kilichopo katika kituo cha Polisi Tabora Mjini kinachoonesha kuwa Sadiki alikamatwa Juni 21 mwaka jana kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na aliingizwa mahabusu ya polisi saa 9.00 alasiri. “Vile vile kitabu hicho kinaonesha kuwa Juni 29, mwaka jana, mlalamikaji alitolewa mahabusu saa 2.00 asubuhi na kupelekwa mahakamani.”

Mganga alisema, kitabu hicho kinaonesha kwamba tarehe hiyo hiyo, alifunguliwa kesi ya mauaji namba 8/2018 ikionesha kuwa Mei 6, mwaka jana, akiwa katika barabara ya Kazima Tabora Mjini alimuua Jackson Thomas. Aidha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilibaini kwamba Julai mosi, mwaka jana pia alikamatwa Edward Matiku a.k.a Nduli kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na Julai 16, mwaka jana, aliunganishwa katika shauri la mauaji ya Thomas. Baada ya Rais kupokea ukweli huo wa malalamiko kutoka kwa DPP, kwanza akampongeza Sadiki kwa ujasiri aliouonesha kuweka wazi malalamiko hayo.

Pia alipongeza gazeti la Majira kwa kufanya uchunguzi na kuchapisha habari hizo zenye ukweli. Aidha, Rais akavishauri vyombo vingine vya habari kuchunguza na kuchapisha habari zenye ukweli na kwa kuzingatia maslahi ya taifa. Rais pia ameagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa wale wote waliohusika na tukio hilo kwa lengo la kukomesha tabia kama hizo zinazoichafua serikali kwa wananchi wake na dunia nzima.

Mganga aliwataka mawakili wote wa serikali wanaofanya kazi katika ofisi ya taifa ya mashtaka, waendesha mashtaka wote nchini waliokasimu mamlaka ya kuendesha kesi za jinai na vyombo vya upelelezi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kumwonea mtu na kuzingatia mslahi ya Taifa.

Alisema hatua za kinadhamu na kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka maadili ya kazi zao. Alisema kutokana na kitendo hicho, jeshi la polisi linawachukulia hatua polisi waliohusika, ofisi yake itawapa adhabu mawakili waliosimamia kesi hiyo na waendesha mashataka wawe makini katika kusaini hati hizo na wafuatilie mwenendo wa kesi kutoka polisi hadi mahakamani. Baada ya kubainika ukweli huo, polisi wanatakiwa kurudisha fedha na vifaa vya Sadiki vilivyochukulia.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi