loader
Picha

Mabasi mwendokasi sasa kaa la moto

WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umesema serikali inazifanyia kazi kwa juhudi kubwa changamoto wanazokumbana nazo abiria wanaotumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Umesema tatizo lililotokea juzi asubuhi katika kituo cha mabasi hayo cha Kimara ni kosa wanalokiri kulisababisha, kwa kuwa walijaribu kuondoa mabasi ya haraka yasiyosimama kila kituo (express), kutokana na malalamiko ya abiria wa vituo vya katikati.

“Ni kweli, jana (juzi) utaratibu wa express ulisimamishwa, mabasi hayo yalisimama kila kituo ili kuwachukua abiria wa vituo vya katikati, lakini tulipoona tatizo limekuwa kubwa, tuliruhusu baadhi yaendelee kuwa express,” alisema Msemaji wa DART, William Gatambi. Juzi katika kituo cha Kimara, mabasi hayo yalichelewa kufika kubeba abiria na kusababisha msongamano mkubwa wa abiria kuanzia saa 12 hadi saa 2 asubuhi yalipoanza kufika.

Gazeti hili likiwa eneo la tukio, lilishuhudia wingi huo wa abiria usio wa kawaida na baada ya kuona mabasi hayaji, walishuka kutoka eneo la kusubiri magari na kuvamia baadhi ya mabasi yaliyokuwa kwenye foleni ya kuingia kituoni hapo kubeba abiria. Baadhi ya abiria walianza kugonga milango ya mabasi hayo, wakitishia kuvunja vioo huku wengine wakiingia kwenye mabasi kwa kupitia madirishani.

Madereva walivyoona hali hiyo, walifungua milango ya upande wa kushoto na abiria waliingia kwa kusukumana na wengine kuumia. Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Hussein, alisikika akilalamika ameumia mguu na alipohojiwa na gazeti hili, alisema amesukumwa na katika kujizuia asianguke ili asikanyagwe na kuumia zaidi, ameumia mguu.

Pamoja na mabasi yanayofanya safari kutoka Mbezi kwenda Kimara kubeba abiria wanaokwenda Gerezani, lakini hali ilikuwa mbaya kituoni hapo, kwani watu walikuwa wengi mpaka katika milango ya vyoo na kusababisha adha kubwa kwa abiria wenye kuhitaji huduma maalum kama wazee, wajawazito, wagonjwa, walemavu na watoto.

Mzee Gidion Faustine aliyekuwa ameshika fimbo ya kumsaidia kutembea, alisema alifika kituoni hapo na mjukuu wake anayemsaidia saa 12 kamili akiwa na safari ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu; na alitakiwa afike hospitali saa moja asubuhi, lakini mpaka saa mbili kasoro alikuwa bado kituoni hapo ; na hakujua atafanikiwa kusafiri saa ngapi.

Baadhi ya abiria walisikika wakitaka daladala za kawaida, zirejeshwe huku wengine wakiitaka serikali iingilie kati kama mwekezaji ameshindwa, aondolewe na aletwe mwingine. Akifafanua kuhusu kadhia hiyo kwa abiria na wananchi wanaotumia usafiri huo na ambao hawana usafiri mbadala wa umma wa kuwafikisha Kariakoo, Magomeni, Posta, Morocco na Muhimbili, Gatambi alisema Serikali haipendi kuona abiria wanapata shida na inaendelea kuchukua hatua kumaliza tatizo.

Alisema mradi huo una mabasi 140, lakini mengi yameharibika na juhudi za kuyatengeneza zinaendelea. Juzi mabasi mawili marefu, yalionekana yameharibika, moja lilikuwa Kimara na lingine karibu na kituo cha Bucha. Gatambi alisema lengo ni kuwa na mabasi 305 ili kumaliza kabisa tatizo la usafiri, ila kwa kuwa mradi bado upo kwenye kipindi cha mpito cha kumtafuta mwekezaji mpya, akipatikana tatizo litakwisha. Msemaji wa UDART, Deus Bugaywa jana hakuwa tayari kuzungumzia kilichotokea Kimara na suala la kushikiliwa mabasi hayo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bandarini na kumuelekeza mwandishi awasiliane na DART.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu wa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa, bado mabasi hayo yanashikiliwa na mamlaka hiyo kwa kuwa wahusika hawajakamilisha taratibu za kuyalipia kodi.

Kuhusu mwekezaji mpya ambaye ilielezwa awali mchakato wa kumpata ulikuwa uanze Machi, mwaka huu, Gatambi alisema mwekezaji wa sasa ni wa mpito na hatua zinaendelea za kumpata mwekezaji wa kudumu na kwamba wananchi wawe na matumaini ya kumalizika kwa kero wanazopata sasa. Akizungumzia migomo ya chini chini inayodaiwa kusababishwa na wafanyakazi kutolipwa mishahara kwa wakati na wengine kwa miezi kadhaa, Gatambi alisema Serikali inajitahidi kuendelea kulipa mishahara na kwenye tatizo kunafanyiwa kazi.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi