loader
Picha

Waziri atishia kufuta Wakala wa Chakula

SERIKALI imetishia kufuta Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kama hataukuwa na uwezo wa kununua tani 500,000 za mahindi kutoka kwa wakulima.

Pia, imesema inakwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye utendaji wa wakala huo ili uweze kununua mazao yote ya ziada kutoka kwa wakulima na kuyauza ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua mashine ya kusafisha mahindi, iliyotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Alisema kama wakala huo utashindwa kununua tani 500,000 za mahindi kutoka kwa wakulima, utafutwa kwani sasa unatakiwa kujiendesha kibiashara zaidi na si kuhifadhi tu chakula, bali kutafuta masoko ya nafaka nje ya nchi ya kuuzia nchi hizo kulingana na mahitaji yao.

“Katika mabadiliko makubwa yanayokwenda kufanyika NFRA hawatakuwa na kazi tu ya kuhifadhi chakula, lazima tununue mazao yote ya ziada yaliyopo kwa wananchi, tunaanza kufanya biashara, mahindi yanayozagaa mitaani wakati nchi za Misri, Syria kuna mahitaji makubwa ya mahindi, eti nyie mnahifadhi tu. “Nunua uza kama utauza suala la mtaji halipo tena, pia lazima muwe na maghala kwani uhifadhi wa sasa ni miaka miwili hadi mitatu.”

Aliwataka kutafuta maghala mazuri kama Marekani, ambao wanaweza kutunza chakula kwa miaka 10 hadi 15. Pia aliwataka kubadili mfumo wa ununuaji nafaka, kwani mfumo unaotumika una gharama kubwa, na kusema kuna mifumo mizuri ya kielektroniki ambayo inaweza kutumika.

Aliwataka kuangalia suala la gharama za kusafirisha mahindi, kwani ni kubwa, tofauti na gharama wanazotumia watu binafsi na wasipofanya hivyo atawaondoa maofisa wanaohusika na suala hilo. “Gunia moja mnasafirisha kwa shilingi 7,500, lakini watu binafsi wanasafirisha kati ya shilingi 2,500 na Sh 3,000, mbadilishe mfumo na fikra zenu lasivyo tutazibadilisha kwa lazima,” alisema.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kupongeza WFP kwenye masuala ya chakula na lishe. “Lishe bado ipo chini tuwahimize watu kula inashangaza kuona wanaoumwa kwa kukosa lishe ni wakulima wanaozalisha,” alisema. Akizungumzia mashine hiyo, Waziri Hasunga alisema ina thamani ya Sh milioni 400 na itakuwa na uwezo wa kusafisha tani 100 za mahindi kwa siku.

Waziri huyo alisema kilimo kina changamoto nyingi hivyo inahitajika kupata teknolojia ya kukiboresha na kubadili kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha biashara. Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikanbuba alisema wamekuwa wakishirikiana kwa muda mrefu na Shirika la WFP. Mwakilishi wa WFP Tanzania, Michael Dunford alisema WFP inaangalia namna ya kumtoa mkulima katika kilimo kidogo na kuwa na kilimo kikubwa.

Alisema dola za Marekani milioni 330 zimeingizwa nchini Tanzania na tangu mwaka 2010 zimenunuliwa tani 500,000 za chakula, kati ya hizo tani 200,000 zimetoka NFRA. Wakala huo wa Chakula umejitahidi kununua chakula katika msimu wa mwaka 2018/19. Kwa mfano kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Ruvuma anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Jeremiah Sendoro hadi sasa NFRA imenunua tani 14,000 za mahindi.

Alisema msimu wa ununuzi ulipoanza Agosti mwaka jana, NFRA ilipangiwa kununua tani 7,000 katika mkoa wa Ruvuma , lakini baadaye iliongezewa kununua mahindi hadi tani 15,000. Alisema hadi sasa imenununua tani hizo 14,000 na itamalizia kununua kiasi kilichobaki cha tani 1,000 hivi karibuni. Sendoro alisema NFRA imekuwa ikinunua mahindi kwa wakulima kwa bei ya Sh 430 kwa kilo, wakati watu binafsi na walanguzi wanalipa wakulima Sh 300 hadi Sh 350 kwa kilo.

Mahindi mengine yananunuliwa na vyama vya ushirika. Alieleza kuwa mahindi yanayonunuliwa na serikali, yanahifadhiwa katika maghala ya Wakala huyo, wakati vyama vya ushirika na watu binafsi wana maghala yao ya kuhifadhi mahindi.

Kwa upande wake, NFRA Kanda ya Sumbawanga inayojumuisha mikoa ya Katavi na Rukwa, imekwishanunua tani 9,000 za mahindi hadi sasa, ambapo awali ilipangiwa kununua tani 5,500, lakini baadaye iliongezewa tani 3,500, hivyo kuwa jumla tani 9,000. Ilielezwa kuwa mahindi mengi yaliyonunuliwa ni kutoka mkoa wa Rukwa, lakini kwamba tani 2,500 za mahindi ya mkoa wa Katavi hazikununuliwa, kutokana na mahindi hayo kuwa machafu.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi