loader
Picha

Lukuvi acharukia waficha mafaili

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametaka wafanyakazi wa wizara hiyo kuacha kuficha mafaili ya watu na kuwataka watoe chochote ili wayatafute.

Amewataka watendaji wake katika wilaya, kanda na wizarani kuhakikisha wamekusanya kodi yote ya ardhi ifikapo Mei 30, mwaka huu. Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jijini hapa jana, Waziri Lukuvi alisema, wafanyakazi wa wizara hiyo wasio waaminifu wanatakiwa kujipima wenyewe kama wanafaa.

Alisema kumekuwa na mfumo na tabia mbaya ya baadhi ya watendaji ya ufichaji mafaili ya watu (chini ya uvungu) na kuomba chochote (fedha) wayatafute, kitendo ambacho si kizuri. Alisema watendaji wenye tabia hiyo hawatakiwi kuwepo wizarani, wanatakiwa kuchujwa ili hadi Mei 30, mwaka huu, wawe wametolewa na kubaki na watendaji wanaojituma na wabunifu.

Alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo, kufanya mabadiliko ya kuwapanga watendaji katika wizara hiyo katika muda huo, ili Julai mosi watakapoongezeka wafanyakazi wa ngazi ya wilaya, wawe wamebaki watendaji bora. Alimtaka Katibu Mkuu kuwajibisha watendaji wote wasiowajibika na kuwapanga upya watumishi kadiri ya utendaji kazi, sifa na uwajibikaji wala si uzoefu au mafaili yao ni makubwa akisema hata vijana wanaruhusiwa kupandishwa vyeo maadamu ni wachapakazi.

Lukuvi alisema wafanyakazi wasipandishwe vyeo kwa kujuana, au kwa kuwa karibu na watendaji wakuu. Alisema wapo watendaji wengi wazuri ambao wamekuwa wakifichwa kona au kupigwa chenga wakati wana uwezo, lakini wamekuwa wakipandishwa vyeo wasiostahili, utendaji wa namna hiyo hauleti motisha kwa wafanyakazi.

Lukuvi alisema hatakubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia, hasa baada ya kutembelea wilaya na kuona wachapakazi, atafuatulia na kuona wanaopandishwa vyeo ni wale wanaowajibika. Alisema anataka wizara iongozwe na watu wenye weledi, wabunifu na walio mstari wa mbele kutekeleza kazi yao na kufanya vizuri kukusanya kodi ya watu wanaomiliki ardhi.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi