loader
Picha

CUF yaja na sera mpya, Maalim Seif matatani

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba amezindua sera yao mpya ya Furaha na Haki Sawa (Fuhasa) na kumtaja Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Hamad kuwa mtu hatari kwa chama na nchi.

Lipumba alibainisha hayo jana kwenye hotuba yake aliyoitoa kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe juzi na mkutano mkuu wa CUF ulioitishwa na Baraza Kuu la chama hicho. Alitumia saa moja kuelezea masuala ya chama, mikakati yake na changamoto kilichopitia.

Aliwatahadharisha wanachama wa CUF kama wanataka ushindi wa kishindo kwenye chaguzi zijazo za serikali za mitaa au uchaguzi mkuu wajiepushe na kuchukua tahadhari dhidi ya Maalim Seif kwani ni mtu hatari kwao.

Alisema Malim Seif ameirudisha nyuma CUF tangu ilipojiunga na Umoja wa Wabunge wa Katiba (Ukawa) uchaguzi uliopita mwaka 2015 ambapo alimkataa yeye kuwania uraisi bara na badala yake akamuunga mkono aliyekuwa mgombea kupitia Chadema, Edward Lowasa. Alisema Maalim Seif ameifungulia CUF kesi 39 mahakamani kuzuia isiendelee kupigania maendeleo ya siasa na kuwataka wajumbe wajue hizo ni baadhi ya sababu za kumwogopa.

Alisema:”ni vema mkatambua hata huu mkutano wa leo Maalim Seif aliuwekea pingamizi usifanyike. Yeye alipinga mimi kuandaa mkutano huu. Alituwekea pingamizi mimi na Kaimu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya akidhania tumeuitisha, lakini kumbe Wajumbe wa Baraza Kuu la chama ndio wenye mamlaka ya kuuitisha na ndio wameuitisha.” Alisema ingawa amerejea kwenye chama hicho kama Mwenyekiti, amekuwa kwenye ugomvi mzito na Maalim Seif anayehadaa baadhi ya wabunge wa CUF kutomsikiliza na kumtii.

Alisema, kwa miaka yake mitano ya uenyekiti atahakikisha anakilinda chama kwa kila hali akihakikishia wanachama wake na Watanzania wanajaa furaha muda CUF itakuwa ikiendesha uongozi kwenye ngazi mbalimbali nchini. Lipumba alisema sera ya Fuhasa inarejesha hali ya furaha na haki sawa kwa watu na itaiinua Tanzania kutokea kuwa moja kati ya nchi tano za chini duniani watu wake kuwa na furaha hadi kuwa moja kati ya nchi tano bora zenye furaha. Aliwataka wanachama wa CUF kuwa na mikakati ya kusaidia upatikanaji huduma bora za chakula, elimu, afya, furaha na kila huduma muhimu kwa wananchi ili wawe na furaha.

Alisema atazilinda rasilimali za nchi kwa kupanga matumizi bora na kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika nazo na kukabili wachache ambao wamekuwa wakijinufaisha. Aliipongeza serikali ya Rais John Magufuli kwa kutekeleza sera za CUF za kuwakabili mafisadi waliokuwa wakifuja rasilimali hizo za nchi. Lipumba aliwahakikisha wanachama na wafuasi wa CUF amejipanga kuikabili Chadema isipate wasaa wa kuivuruga CUF kwa namna yoyote ile kama ilivyofanya kwenye uchaguzi uliopita.

Akizungumzia Chadema ilivyowahujumu, alisema kiliwaomba majina ya maeneo yote ambayo CUF ina nguvu kisiasa ili Chadema isisimamishe mgombea kwenye maeneo hayo lakini bado Chadema imesimamisha wagombea. Alisema kama vile haitoshi Chadema imekuwa ikihadaa viongozi wa CUF kwa kuwataka wagombee nafasi za uongozi kwenye serikali za mitaa, udiwani na nyinginezo kubwa kwa kutumia tiketi ya chama chao na mwisho wa siku walikuwa wanaelekea kukiua chama hicho.

“Nimeshangaa ni kwa nini Chadema waligeuka kwenye mambo mengi, kwanza ifahamike hata hilo jina la Ukawa mie ndio nililiunda wakati tukiwa kwenye mchakato wa kupata katiba mpya na tukaamua kuwa na umoja wa wabunge wa katiba nikawatajia jina la Ukawa,”alisema.

Alisema Chadema ilitaka kutumia Ukawa kuchukua nchi ikitaka serikali tatu ichukue serikali ya bara na ile ya visiwani iwe chini ya Maalim Seif kupitia CUF wakati yeye Lipumba akitaka kwanza maslahi ya muungano na hasa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Lipumba amechaguliwa kwa mara ya tano kwa kura 516 sawa na asilimia 88.9 akifuatiwa na Zuberi aliyepata kura 36 sawa na asilimia 6.2 huku Diana akipata kura 16 ambazo ni sawa na asilimia 2.8. Kura za jumla zilizopigwa ni 598. Makamu Mwenyekiti wa CUF kwa Zanzibar ni Abas Juma Muhuzi aliyepata kura 349 sawa na asilimia 60.9 na bara ni Maftah Abdi Nachuma kura 231; asilimia 40.9.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi