loader
Picha

Manyara yaongoza kwa ukeketaji

MKOA wa Manyara unaongoza katika ukeketaji dhidi ya wasichana nchini kwa asilimia 58 ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma kwa asilimia 47.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Atupele Mwambene katika kikao cha wadau wa kupitia rasimu ya mkakati wa kitaifa wa ukeketaji nchini jijini hapa.

Kwa mujibu wa taarifa za Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto na viashiria vya Malaria ya mwaka 2015/16, mikoa mingine kati ya 10 inayoongoza nchini ni Arusha kwa asilimia 41, Mara (32), Singida (31), Tanga (14), Kilimanjaro (10), Morogoro (9) na Iringa (8) na Njombe (7).

“Kati ya mikoa hiyo 10, ni mikoa mitatu tu ambayo ipo chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 10 na inayobaki yote saba ipo juu ya wastani wa kiwango hicho cha kitaifa,” alisema. Mwambene alisema hiyo, inamaanisha kwamba tatizo la ukeketaji nchini bado lipo kinachotakiwa ni kuweka mkakati wa makusudi kuongeza jitihada katika kukabiliana na tatizo hilo.

“Mkakati huo mnaopitisha ni nyenzo muhimu na madhubuti inahitajika katika kukabiliana na tatizo hilo, ni vema wakati mpikitisha mkakati huo mkazingitie hilo,” alisema Mwambene. Alisema katika kukabiliana na ukeketaji nchini, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa na kutekeleza sera, sheria na mikakati shirikishi ikijumuisha sera ya wanawake na maendeleo ya jinsia ya mwaka 2000.

“Pia sera ya mtoto ya mwaka 2008, sheria ya mtoto na. 21 ya 2009, na mwaka 2016, ilizindua Mpango kazi wa Taifa wa miaka mitano 2016/17-2021/22 wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA),” alisema.Alisema mpango huo uliandaliwa kwa lengo la kuunganisha mipango nane iliyokuwepo awali iliyokuwa inashughulikia suala la ukatili kwa wanawake na watoto.

Mwambene alisema tunaamini kuwa utekelezaji wa mpango huu ipasavyo utawezesha serikali na wadau wa maendeleo kupunguza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa zaidi ya asilimia 50 ifikapo mwaka 2020/21.

Awali Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwajuma Magwiza alisema, mchakato wa kuandaa mkakati wa kitafa wa kutokomeza ukeketaji ulianza Agosti, 2017. Alisema mchakato huo ulianza kwa kufanya majadiliano na wadau ili kufikia lengo la kupunguza ukeketaji kwa asilimia 50 ifikapo 2022.

Alisema Takwimu za taarifa ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria nchini ya mwaka 3015/16, zinaonesha kwamba kitaifa hali ya ukeketaji imeshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 10 mwaka 2015/16 ingawa baadhi ya mikoa takwimu za ukeketaji bado zipo juu.

Alisema hadi sasa wameshuhudia madhara ya vitendo vya ukeketaji kwa wasichana na wanawake, ikiwa ni pamoja na madhara ya kiafya, kiuchumi na kielimu. Magwiza aliwashukuru AMREF Tanzania na Hodari Tanzania kwa kuwezesha kuandaliwa kwa mkakati huo maalumu, ambao ukikamilika kutasaidia kuratibu na kuboresha ushiriki wa wadau katika kutokomeza ukeketaji.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi